ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 24, 2013

Masikini Mrisho Ngasa

Uwezekano wa winga wa Yanga, Mrisho Ngassa kuonekana Uwanja wa Taifa Jumamosi akiwa amevalia uzi wa kijani na njano wakati timu yake itakapokuwa ikivaana na Ruvu Shooting, sasa ni majaliwa baada ya klabu yake kususa kumlipia faini ya Sh. milioni 45 alizotakiwa kuilipa Simba.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto aliliambia NIPASHE jijini Dar es Salaam jana kuwa, suala hilo kwa sasa haliko chini ya klabu yao, bali ni la Ngasa mwenyewe.

"Maamuzi yaliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), yanamtaka Ngassa na si klabu ya Yanga kulipa fedha hizo. Klabu ilikata rufaa kupinga maamuzi ya kumfungia mechi sita na si suala la kulipa fedha.

"Rufaa yetu tayari ilishatupwa na mchezaji amekosa mechi zote sita, hivyo hayo mengine ni juu yake," alisema Kizuguto.


Kwa upande wa TFF, ilisema Ngassa bado hajalipa fedha za Simba kama ilivyomtaka kutekeleza hilo kabla ya kumruhusu kuanza kuitumikia Yanga msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema licha ya kukosa mechi sita ikiwamo ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Azam FC na tano za Ligi Kuu ya Bara msimu huu, Ngassa hajamaliza adhabu aliyotakiwa kuitumikia.

"Ngassa bado hajamaliza adhabu kwa kuwa hajalipa fedha za Simba. Mpaka sasa (jana saa 6:12 mchana) bado hajalipa fedha za Simba, hivyo haruhusiwi kucheza licha ya kwamba tayari ameshakosa mechi sita kama ilivyoamuliwa na kamati. Hawezi kucheza mechi ya Jumamosi kama hatalipa fedha hizo," alisema Osiah.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilimpa Ngassa adhabu hiyo baada ya usajili wake kuleta utata kutokana na kujisajili klabu mbili tofauti, Simba na Yanga.

Hata hivyo, kamati hiyo ilitumia busara na kumwidhinisha Ngassa kuichezea Yanga msimu huu huku ikimtaka kuilipa Simba jumla ya Sh. milioni 45, kati ya hizo Sh. milioni 30 ni alizopewa kama ada ya usajili, wakati ambapo Sh. milioni 15 zikiwa ni asilimia 50 ya faini ya kiasi hicho cha fedha alichopokea.

Mbali na kutakiwa kulipa kiasi hicho, kamati hiyo ilimfungia kucheza mechi sita msimu huu. Kadhalika ilieleza wazi kwamba, Ngassa hataruhusiwa kuichezea Yanga kama atakuwa hajailipa Simba hata kama atamaliza kifungo cha kutocheza mechi sita.

NGASA
Kwa upande wa Ngassa ambaye aliwahi kuichezea Kagera Sugar, Azam FC na Simba, NIPASHE lilipomtafuta jana kuzungumzia sakata hilo, kwanza alikataa kulitolea ufafanuzi kwa madai kuwa liko chini ya uongozi wa klabu yake ya sasa, Yanga.

"Waulize viongozi wa Yanga maana wao ndiyo walikuwa wanafuatilia suala hilo," alisema kwa kifupi mzaliwa huyo wa jijini Mwanza, huku akikataa kuendelea kuzunguza licha ya mwandishi wetu kumfahamisha kuwa Yanga imesema haihusiki na kulipa fedha hizo.

Agosti 23, mwaka huu Yanga iliwasilisha rufaa TFF kupinga maamuzi ya kumfungia winga huyo huku ikitishia kulipeleka suala hilo katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Hata hivyo, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, shirikisho hilo liliitupa rufani hiyo ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kuwa haikubainisha kamati ya rufaa iliyolengwa na mrufani (Yanga).

"TFF ina kamati tatu za rufaa: kamati ya rufaa ya maadili, kamati ya rufaa ya nidhamu na kamati ya rufaa ya uchaguzi. Barua ya Yanga haikueleza rufaa yao ilitakiwa kupelekwa kwenye kamati ipi kati ya hizo tatu," alisema Wambura katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, maamuzi yanayotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji (iliyomhukumu Ngassa) ni ya mwisho nchini.

Ilielezwa kwamba kamati hiyo ilitumia busara badala ya kumhukumu Ngassa kwa mujibu wa Kanuni ya 44 (3) cha Kanuni za Ligi za TFF na Sura ya IV Ibara ya 17 (4) cha Kanuni za Fifa, ambapo winga huyo alitakiwa afungiwe kucheza soka kwa mwaka mzima huku klabu ya Simba ikistahili kifungo cha misimu miwili mfululizo pasipo kusajili wachezaji wa ndani na nje.

"Klabu inayomshawishi mchezaji kumsajili wakati akiwa na mkataba na timu nyingine kwa kusaini au kuvunja mkataba wake na klabu hiyo pasipo kuitaarifu klabu husika, itafungiwa na chama cha soka cha nchi husika kusajili wachezaji wa ndani na nje kwa misimu miwili mfululizo," inaeleza Sura ya Nne Ibara ya 17(3) cha Kanuni za Fifa.
  
CHANZO: NIPASHE

No comments: