ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 24, 2013

Vifo, maombolezo

Moshi mzito uliotanda angani juu ya Kituo cha Biashara cha Westgate Jijini Nairobi jana, uliashiria mapambano makali kati ya vyombo vya usalama vya Kenya dhidi ya kikundi cha kigaidi cha al Shabaab.

Mapigano hayo yalifanyika ili kulikomboa Jengo hilo kutoka mikononi mwa Al Shabaab ambao waliliteka Jumamosi iliyopita na kuwaua raia na kuwashilika wengine mateka katika tukio la kutisha kuwahi kutokea nchini humo.

Hadi jana taarifa rasmi za kiserikali zilisema watu 62 wameuawa na magaidi hao, 175 kujeruhiwa huku vyombo vya usalama vikifanikiwa kuokoa zaidi ya watu 1,000.
Mtanzania mmoja akiwa miongoni wa majeruhi hao.

Aidha, serikali ya Kenya ilithibitisha jeshi lake kuua magaidi wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa. Taarifa za awali zilisema idadi ya magaidi ilikuwa imekadiriwa kuwa kati ya 10-15.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa taarifa juu ya kadhia hiyo, na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa,Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Joseph Ole Lenku, alisema majeshi ya Kenya yalifaulu kulikomboa jengo hilo, baada ya operesheni ya kutwa nzima.

“Ninachoweza kusema mpaka sasa ni kwamba, tayari majeshi yetu yamekwisha lidhibiti jengo lote la Westgate, na kwa sasa yanafanya safisha safisha ya chumba hadi chumba, ili kusaka kama kuna mabaki ya magaidi kwa ajili ya kuwaangamiza,” alisema.

Alisema, mateka wote walikuwa wameokolewa na kuwa askari 10 walioshiriki kwenye operesheni hiyo, wamejeruhiwa.

Ole Lenku alisema, idadi ya waliojeruhiwa katika uvamizi huo wa al Shabaab walikuwa 175 na kuwa wengi wao walitibiwa katika hospitali mbalimbali na kuruhusiwa kuondoka.
Aidha alisema, watu 63 hawajulikani walipo.

Akijibu swali lililokuwa likiuliza endapo kuna msaada wa kijeshi kutoka mataifa ya nje, yakiwemo ya nchi za magharibi na Israel kwenye operesheni hiyo, kama ilivyokuwa imetangazwa na msemaji wa kundi la al Shabaab, Sheikh Ali Mohamud, Ole Lengo alisema:

“Operesheni hii ni ya kwetu na inafanywa na watu wetu, kwa maana kutoka katika Jeshi la Kenya, Polisi na Usalama wa Taifa.Hawa ndiyo wako kwenye uwanja wa mapambano.”

Ole Lenku alithibitisha kuwa magaidi wote walikuwa wanaume, ila baadhi yao walikuwa wamevaa kike, kwa lengo la kupoteza watu ‘maboya’ tofauti na ilivyokuwa imeripotiwa na vyombo vya habari kuwa, kulikuwa na wanawake miongoni mwa magaidi hao.

MTANZANIA AJERUHIWA
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Batilda Burian, alisema Mtanzania Vedastus Nsanzugwanko ambaye ni meneja wa Ulinzi wa Watoto wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje Nsanzugwanko amejeruhiwa kwa gruneti miguu yake na amelazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi hali inaelezwa kuimarika.

Kwa mujibu wa mahojiano aliyoyafanya jana na kituo cha Televisheni ya Taifa cha TBC cha jijini Dar es Salaam, Dk. Burian alisema:

“Hadi sasa tuna taarifa ya Mtanzania mmoja kujeruhiwa na amelazwa katika hospitali ya Agha Khan ya hapa Nairobi. Tunaendelea kufuatilia kama kuna wengine waliojeruhiwa na kama wapo, tutatoa taarifa.”

HALI ILIVYOKUWA
Pilika pilika za hapa na pale zilishuhudiwa jana karibu siku nzima huku milio ya risasi ya hapa na pale, na milipuko mikubwa ikisikika.

Kwa muda wa saa mbili kuanzia saa 10:00 jioni, risasi zilisikika kwa muda mrefu kati ya majeshi na magaidi

Majeshi ya ulinzi ya Kenya yalionekana kulizingira eneo hilo lote yakiwa na magari ya deraya.
Aidha magari ya zimamoto yalionekana vile vile, ikiwa ni pamoja na magari ya kubeba wagonjwa yakiwa tayari kufanya kazi hiyo.

Helikopta za kijeshi ziliendelea kupiga doria zikilizunguka eneo ili kuhakikisha kwamba hakuna gaidi anayetoroka.

Aidha, moshi uliendelea kuonekana ukifuka kwa muda mrefu katika jengo hilo, ambapo taarifa kutoka kwenye vyombo vya ulinzi zilisema, Al Shabaab walichoma moto magodoro yaliyokuwa ndani, kwa lengo la kuwapoteza maboya askari.

WAJITOLEA DAMU
Wananchi karibu 1,500 wa nchi hiyo walikusanyika kwa wingi katika viwanja vya Uhuru Park, vilivyoko jijini Nairobi, kwa ajili ya kutoa damu ya kuwasaidia wenzao waliojeruhiwa.

KESI YA RUTO YAAHIRISHWA
Kufuatia kadhia hiyo, Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) ilikubali kuaihirisha kesi ya Naibu Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto, kwa wiki moja, kufuatia ombi lililotolewa na wakili wake, Kharim Khan.

Ruto aliomba kesi yake iahirishwe ili akatimize majukumu yake ya kusaidia kutoa uongozi utakaosaidia kupambana na magaidi walioliteka jengo la Westpark.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya ombi hilo kukubaliwa na mahakama, Ruto alisema kuwa inasikitisha kwamba magaidi walipanga kufanya hujuma hiyo, wakati yeye na Rais Uhuru Kenyatta wakiwa hawapo ndani ya nchi hiyo.

“Shambulio hili limefanyika nikiwa the Hague, nje ya nchi yangu, lakini ilikuwa ni wakati ambao Rais Kenyata awe yuko safarini nje ya nchi huko Brussels, kwenye mkutano uliokuwa ukiihusu Somalia,” alisema.

Alisema Kenyatta vilevile alikuwa akahudhurie mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN), hivyo kama asingeahirisha kuondoka, ina maana shambulizi hilo lingetokea wakati viongozi wote wa juu wa Kenya wakiwa hawapo.

AL SHABAAB WANENA.
Awali al Shabaab walikuwa wameonya kuwa wangeua mateka wote ikiwa majeshi ya ulinzi ya Kenya, pamoja na wataalamu wa kijeshi toka nchi za Magharibi na Israel wangelivamia kwa nguvu jengo hilo.

“Majeshi ya Israel na ya Kenya yalijaribu kuingia kwa nguvu ndani ya Jengo hili la Westgate tunalolishikilia lakini hayakuweza,” alisema Sheikh Ali Mohamud Rage, kwenye taarifa iliyotumwa kwenye mtandao

“Mashujaa wa Mujahideen wataua mateka wote endapo adui watatumia nguvu,” alisema.

Al Shabaab walikuwa wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuondoa majeshi yake toka Somalia ambayo yalikuwa yamewapiga na kuwafanya wakimbizi wasio na makazi maalum katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Majeshi hayo yalienda kupigana na al Shabaab nchini Somalia, yakiwa kama sehemu ya Misheni ya Umoja wa Afrika nchini humo, ambapo Rais Kenyatta alikataa.

VIFO NA MAJERUHI
Mbali na Wakenya, wananchi kutoka mataifa mbalimbali pia wameuawa na kujeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya kimataifa, na kuthibitishwa na viongozi wa nchi zao, wananchi hao wanatoka, katika nchi za Uingereza (4), Ufaransa, Canada, Australia (1), Uchina na Marekani.
Aidha, Mshairi maarufu kutoka Ghana, Kofi Awoonor, ni miongoni mwa waliouawa.

SALAMU ZA RAMBIRAMBI
Salamu za rambi rambi ziliendelea kutumwa kutoka pande zote za dunia, ikiwa ni pamoja na karibu bara zima la Afrika, Marekani, Ulaya, Asia na Australia.
Pamoja na viongozi wengine, ni Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

MATEKA ANENA
Shambulizi hili la al Shabaab linaonyesha uwezo wa kundi hilo wa kusababisha hasara kubwa, pamoja na upungufu wa rasilimali, hata baada ya kuwa limefukuzwa Somalia na Majeshi ya Kenya na yale ya Umoja wa Afrika.

Mmoja wa mateka aliyeokoka, anayeitwa Cecilia baada ya kuibuka toka alikokuwa amejificha ndani ya gari katika maegesho yaliyo chini ya jengo, aliliambia Reuters kuwa, aliwaona mateka watatu.

“Walikuwa wakishambulia kote kote, niliona watu wakipigwa pande zote, wengine wakivuja damu kutokana na majeraha. Nilikuwa nikiomba Mungu anisaidie nibaki mzima,” alisema.

Mashahidi wanasema magaidi yalikuwa yamebeba bunduki aina ya AK-47, yakiwa yamevaa mikanda yenye risasi. Mmoja wa magaidi alipigwa risasi na kukamatwa mapema na baadaye alifariki.
Kwa saa nne baada ya kuanza kwa shambulio, maiti zilikuwa zimetapakaa kwenye meza pamoja na vyakula walivyokuwa wameagiza.

Katika mgahawa mmoja, mwanaume na mwanamke walikufa wakiwa wamekumbatiana mpaka miili yao ilipoondolewa.

Kenya ilipeleka majeshi yake Somalia mwaka 2011, kwa ajili ya kuwashambulia al Shabaab, iliyowatuhumu kuwateka watalii na kushambulia vikosi vyake vya ulinzi

Shambulio kubwa la mwisho kufanywa na kundi hilo lilikuwa ni lile la mabomu nchini Uganda, lililowalenga wananchi waliokuwa wakiangalia mechi za kombe la Dunia kwenye televisheni nchini Uganda mwaka 2010, ambapo liliua watu 77.

MANUMBA AZUNGUMZA
Jeshi la Polisi nchini, limewaondolea hofu Watanzania kuhusiana na vitendo vinavyotishia usalama wa uhai wao ikiwa ni pamoja na vile vinavyohusiana na ugaidi na kuwa limejipanga vya kutosha kudhibiti

Akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, alisema kuwa, Watanzania wasiwe na wasiwasi wowote kuhusiana na matukio yanayofanana na hilo la Kenya kwani jeshi hilo linayo mipango kwa ajili ya usalama wa raia wake.

“Watanzania wasiwe na wasiwasi wala hofu, waendelee na shughuli zao kama kawaida. Nawaomba Watanzania kuwa makini kuangalia kitu chochote chenye kutia mashaka. Ishu kubwa ni ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi muda wowote wanapokiona kitu kinachotia mashaka,” alisema Manumba.

DCI Manumba, aliongeza kuwa, wanaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini Kenya na lile la kimatifa kuhusiana na udhibiti wa vitendo hivyo vya kigaidi likiwamo hilo la kinyama katika nchi hiyo ya jirani ya Kenya.

Hata hivyo hakutaja hatua zozote za haraka ambazo jeshi hilo limezichukua kukabiliana na magaidi ili kulinda uhai wa Watanzania katika maeneo ya mikusanyiko mikubwa kama vile kwenye mikutano ya hadhara na masoko makubwa kwa madai ya kuwa ni kutokana na taratibu za kiulinzi na usalama.


Imeandikwa na Raphael Kibiriti na Isaya Kisimbilu
CHANZO: NIPASHE

No comments: