ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 19, 2013

Meli iliyokamatwa na shehena ya bangi Italia yafutiwa usajili

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, Abdi Maalim

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imeifutia usajili meli ya MV Gold Star iliyosajiliwa Zanzibar mwaka 2006 kwa namba 340232.

Aidha, usajili wa meli hiyo ulithibitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa na kupewa namba IMO 7393860, na hivi karibuni ilikamatwa katika Bahari ya Mediterranean nchini Italia ikiwa imebeba shehena ya tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi.

Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake mjini Zanzibar, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, Abdi Maalim, alisema mamlaka yake imewasiliana na wakala wa kampuni ya Philtex yenye ofisi zake Dubai ambayo ndiyo iliyopewa idhini na serikali ya Zanzibar kusajili meli, kufuta usajili wa meli hiyo kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kufanya biashara haramu.


Alisema  ukubwa wa mzigo uliopakiwa na meli hiyo,  unaonyesha kuwa tukio hilo yawezekana limefanywa na mmiliki wake kwa kushirikiana na mabaharia, na ilikuwa ikitokea nchini Uturuki kuelekea Misri.

Amewaagiza wamiliki wa meli mbalimbali kuheshimu sheria na mikataba ya usajili inavyoelekeza kwa kufanya kazi halali.

Maalim alithibitisha kuwapo kwa wimbi kubwa la mabaharia wanaoshutumiwa kujihusisha na ubebaji wa dawa za kulevya.

Kwa msingi huo aliwataka mabaharia wa Tanzania wawe makini na kujiepusha na vitendo vya kihalifu.

Hata hivyo, alisema kati ya mabaharia tisa waliokuwamo kwenye meli hiyo ambao sasa wanashikiliwa na polisi wa Italia, hakuna hata Mtanzania mmoja.

Alieleza kuwa, saba kati ya wafanyakazi wa meli hiyo ni raia wa Syria na wawili wa kutoka India.

Aliyataja majina ya mabaharia saba ambao ni raia wa Syria kuwa ni Balkis Ahmad (50), Othman Hani (30), Jalloul Abdulrahman (26), Dalileh Ahmad (42), Alfran Bachar (26), Suleiman Shadi (32) na Juma Mustafa (26).

Aidha, raia wa kutoka India ni Chauhan Anuj (19) na mmoja aliyemtaja kwa jina moja, Munish (24).
Meli hiyo ilikamatwa Septemba 7, mwaka huu katika mwambao wa Cicily nchini Italia baada ya kubainika imepakia bangi ingawa mabaharia waliokuwamo walijaribu kuitia moto na kujitosa baharini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: