ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 24, 2013

MTANZANIA ALIYEJERUHIWA WESTGATE MALL NCHINI KENYA AENDELEA KUPATA NAFUU

Vedasto Nsanzugwanko ambaye alijeruhiwa kwenye shambulio la Kenya akipumzika Hospitali ya Chuo Kikuu Cha Aga Khan mjini Nairobi. PICHA | FILE

Nairobi. Raia wa Tanzania, Vedastus Nsanzugwako ambaye alijeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotokea katika jengo la biashara la Westgate, Nairobi, Kenya ameanza mazoezi ya kutembea baada ya kupata nafuu.
Mtanzania huyo ambaye ni Meneja wa Kinga ya Watoto kwenye Shirika la Maendeleo ya Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Agha Khan, Nairobi alikolazwa baada ya kujeruhiwa katika shambulizi hilo Jumamosi iliyopita.
Nsanzugwako alipigwa risasi miguu yote miwili alipokuwa katika harakati za kujiokoa kwenye shambulio hilo la kigaidi.
Akizungumza jana hospitalini hapo, mke wa majeruhi huyo Jane Nsanzugwako alisema hali ya mumewe inaridhisha tofauti na ilivyokuwa awali kuongeza kwamba endapo mazoezi yataendelea vizuri, anaweza akaruhusiwa kurudi nyumbani.
“Tunaendelea kupata ushirikiano kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya. Hii inatufanya tujisikie kama tupo nyumbani licha ya kuwa ni nchi ya watu,” alisema Jane.
Hata hivyo, Jane alikemea vikali juu ya baadhi ya vyombo vya habari nchini (siyo Mwananchi), vinavyoandika habari za uongo na kupotosha juu ya hali ya mumewe.
Alisema miongoni mwa taarifa zilizosambaa sasa ni kuwa mumewe amefariki, wengine wakiripoti kuwa amekatwa miguu yote miwili habari ambazo alisema si za ukweli.
“Tumekuwa tukipigiwa simu na baadhi ya ndugu na jamaa zetu walioko Tanzania wakisikitishwa na taarifa hizo za uongo. Nasisitiza kuwa mume wangu ni mzima na anaendelea vizuri na tiba ya mazoezi,” alisema.
Mwananchi

No comments: