ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 29, 2013

NGASSA AREJEA YANGA KWA MAKALI, YANGA 1 RUVU SHOOTING 0, MBEYA CITY YATOA SARE TENA NA WAGOSI WA KAYA, MOROCCO AWAFAGILIA CITY

Hamisi-Kiiza
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Mbeya
LIGI kuu soka Tanzania bara imeendelea kutimua vumbi jana, huku mechi iliyokuwa na mvuto zaidi kutokana na matokeo ya mechi za nyuma na urejeo wa Ngassa baina ya mabingwa watetezi, klabu ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ikimalizika kwa wanajangwani kuibuka kededea kwa bao 1-0.

Bao hilo pekee limefungwa katika dakika ya 63 kupitia kwa Mganda, Hamis Friday Kiiza aliyeunganisha krosi murua iliyochongwa na winga machachari aliyekosa mechi 6 za mwanzo kutokana na kifungo, Mrisho Halfan Ngassa ambaye alipokea pasi ndefu kutoka kwa kiungo mahiri, Athmani Idd `Chuji`.


Nimekuja kuchinja: Hamisi Friday Kiiza leo ametumia vizuri kazi nzuri ya Ngassa. Ngassa mwenye mapenzi makubwa na Yanga imekuwa kama neema kwake kwani tangu ligi ianze hajawahi kuitumikia timu yake na leo hii amecheza baada ya jana jioni kulipa deni la milioni 45 alilokuwa akidaiwa na Simba SC.

Kikosi cha Yanga SC: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo/Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza na Mrisho Ngassa.
Kikosi cha Ruvu Shooting: Abdul Seif, Michael Pius, Stefano Mwasyika, George Michael, Shaaban Suzan, Gedion David, Ayoub Kitala/Said Madega, Hassan Dilunga, Cossmas Lewis, Elias Maguri na Reuben Lambele/Kulwa Mfaume.

Mechi nyingine iliyokuwa na mvuti wa aina yake kutokana na ubora wa timu hizo kwa sasa, ilikuwa baina ya Mbeya City waliokuwa uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine kukabiliana na Coastal Union kutoka jijini Tanga.
Mechi hiyo imemalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 ambapo Coastal walikuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 7 kupitia kwa Haruna Moshi `Boban`, lakini dakika ya 70 Mbeya City walisawazisha bao hilo kupitia kwa mtaalamu wa kupiga ndosi, Mwagane Yeya.
Katika mchezo huo Coastal Union walianza kucheza soka la Uhakika kipindi cha kwanza na kudhibiti zaidi eneo la kiungo ambapo Mkenya Jerry Santo, Abdi Banda, na Haruna Moshi `Boban` waliwatawala viungo wa Mbeya City wakiongozwa na Antony Matogolo, Steven Mazanda na Deus Kaseke.

Licha ya Coastal kucheza kwa ufundi, City walionesha ukomavu mkubwa huku Kaseke akihaha huku na huku kuwaletea shida kubwa mabeki wa Coastal walioongozwa na Mbwana Hamis, Othman Tamimu, Juma Nyoso na Marcus Ndeheli.
City walipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini wachezaji wake, Paul Nonga, Deus Kaseke walishindwa kuzitumia na kubadili kuwa mabao.
Picture 030Kikosi cha Wagosi wa Kaya.

Mchezo huo ulitawaliwa na ubabe kiasi Fulani na katika dakika ya 89, Richard Peter wa City na Marcus Ndeheli wa Coastal walioneshwa kadi nyekundu baada ya kuzozana mbele ya mwamuzi wa kati Odern Mbaga kutoka Dar es salaam.

Dakika 4 baadaye, Haruna Moshi alioneshwa kadi nyekundu baada ya kutumia lugha mbaya kwa mwamuzi msaidizi na Mbaga kufanya kazi yake. Baada ya mchezo huo, Kocha wa Mbeya City Juma Mwambusi hakutaka kuongea na waandishi wa habari, lakini alitamka jambo moja tu kuwa mpira umekwisha, wamepata sare, hakuna linginei.

Kwa upande wa kocha wa Coastal Union, Hemed Morocco alisema mechi ilikuwa nzuri, walipanga kushinda lakini mipango yao imeshindwa kutimia, hivyo wanajiandaa na mchezo mwingine. Akiizungumzia Mbeya City, Morocco alisema ni timu nzuri, ina wachezaji waliofiti dakika zote na wanajua kujipanga, lakini akatahdharisha kuwa inatakiwa kupewa muda na wasilazimishe kufika mbali kwani wakati wake utafika tu.

Pia aliwatupia lawama waamuzi kuwa wanatakiwa kukaa chini na kuwa na utu kwani nao wachezaji ni binadamu kama walivyo wengine, hivyo si kila wanapokosea wanatakiwa kupewa adhabu kubwa kama ilivyokuwa.
Picture 044Niacheni nikapumzike jamani: Mlinda Mlango wa Coastal Union, Shaban Hassan Kado alitoka dakika za mwisho za kipindi cha kwanza baada ya kupata majeruhi. (Picha na Rashid Mkwinda)

Mbeya City: David Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Yohana Morris, Antony Matogolo, Alex Seth, Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke, Francis Casto.

Wachezaji wa akiba: Geofrey Jackson, Baraka Haule, Yusuph Willson, Peter Mapunda, Richard Brown, Mwagane Yeya, Richard Peter.

Coastal Union: Shaban Kado, Mbwana Hamis, Othman Tamimu, Juma Nyoso, Marcus Ndeheli, Jerry Santo, Uhuru Seleman, Abdi Banda, Pius Kisambale, Haruna Moshi, Crispine Odula.

Wachezaji wa Akiba: Said Lubanda, Hamad Hamis, Yusuph Chuma, Razak Halfan, Yayo Lutimba, Keneth Masumbuko, Daniel Lyanga. Mechi nyingine ya ligi hiyo iliwakutanisha Rhino Rangers katika dimba lao la A.H. Mwinyi dhidi ya Kagera Sugar na mchezo huo umemalizika kwa wanajeshi hao wa jeshi la wananchi la Tanzania, (JWTZ) kulala bao 1-0. Bao hilo pekee kwa wakata miwa wa Kaitaba limefungwa na Themi Ferlix katika dakika ya 66.

Ligi hiyo itaendelea kesho ambapo JKT Ruvu watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Taifa jijini Dar es salaam kuvaana na Simba, Ashanti United watakuwa na kibarua mbele ya Mtibwa Sugar uwanja wa Azam Complex, wakati huo huo Tanzania Prisons watakuwa Sokoine kula sahani moja na Azam fc.

No comments: