THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais
Kikwete: ICC inaharibu mahusiano yake na Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mwenendo wa Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuhusu Bara la Afrika na viongozi wake, unainyima
Mahakama hiyo nafasi kubwa ya kuungwa mkono na Bara la Afrika.
Rais Kikwete pia amelaani vikali
mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya vikosi vya kimataifa vya kulinda amani
katika nchi mbali mbali duniani wakiwamo walinda amani wa Tanzania.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo wa
Tanzania mwishoni mwa wiki wakati alipohutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa (UNGA) mwaka huu, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New
York, Marekani.
Katika hotuba yake fupi na
iliyowavutia wasikilizaji, Rais Kikwete alisema kuwa ni dhahiri kuanzishwa kwa
ICC kutokana na Mkataba wa Rome kulikuwa ni hatua muhimu sana katika mfumo wa
kimataifa wa kupambana na makosa ya jinai.
“Kwa hakika kuundwa kwa Mahakama hiyo
kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai na kuweza
kuepukana na kuwajibika kwa vitendo hivyo na Mahakama hiyo ilianzishwa kwa kuungwa
mkono kwa kiasi kikubwa na Afrika.
“Hata hivyo, muongo mmoja tu
baada ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, ni dhahiri kuwa mvutano umezuka kati ya
ICC na Bara la Afrika. Sasa Mahakama hiyo inaonekana kama taasisi isiyojali maoni
na msimamo wa Afrika, kwa mambo ambayo kwa maoni yangu, ni hofu halali ya
Waafrika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Bado
Mahakama hiyo inaendelea kupuuza maombi ya mara kwa mara ya Umoja wa Afrika. Ni
jambo la kutia huzuni kuwa maombi ya kubadilisha muda wa kuanza kusikilizwa kwa
kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Naibu Rais William Ruto yalipuuzwa
na hata hayakujibiwa kabisa.”
Ameongeza
Rais: “Tabia hii imekuwa ni hitilafu kubwa ambayo inaleta kikwazo kwa ICC
kushindwa kutimiza wajibu wake wa kupambana na tabia ya watu wanaofanya makosa
ya jinai kutokuchukuliwa hatua. Kwa hakika, kugangamara kwa ICC hata katika
masuala yaliyo wazi, kumethibitika kuwa kunainyima Mahakama hiyo nafasi ya
kuendelea kuungwa mkono Barani Afrika.”
Rais
Kikwete alisema pia kuwa Tanzania sasa imekuwa moja ya nchi ambazo zinashiriki
zaidi katika shughuli za kimataifa za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Tanzania ina zaidi ya walinda amani 2,500 katika Darfur, Sudan; Lebanon na
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuwa ni nchi ya sita katika Afrika na
ya 12 duniani kwa kutoa walinzi wa amani duniani.
“Kwa
hakika tunaridhishwa na mchango wetu mdogo katika shughuli hii. Na tunajua kuwa
wakati mwingine tunalipa gharama kubwa na maisha ya vijana wetu kwenye shughuli
hizi kama ilivyotokea majuzi katika Darfur na DRC. Waliopoteza maisha yao ni
mashujaa wa taifa letu ambao maisha yao hayakupotea bure.”
Aliongeza
Rais Kikwete: “Vifo vya walinda amani wetu ni ukumbusho wa kutosha wa hatari zinazowakabili
walinda amani wote duniani. Ni jambo la kuudhi, kwamba vikundi vyenye silaha na
waharibifu wa amani duniani wanaongeza mashambulizi hayo dhidi ya watumishi wa
amani. Ni lazima tulaani mashambulizi haya kwa nguvu zetu zote kwa sababu
hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha mashambulizi
haya ya kinyama ambayo ni kosa la kimataifa la jinai chini ya Sheria za
Kimataifa.”
Alisisitiza:
“Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo wajibu wake mkuu ni kulinda amani na
usalama wa kimataifa lazima liwe mstari wa mbele katika kulaani vitendo hivyo
vya kinyama na haraka tu vinapotokea.”
Rais
Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi katika Marekani na Canada
ameondoka New York usiku wa leo, Jumamosi, Septemba 28, 2013, kurejea nyumbani
ambako atawasili Jumatatu mchana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29
Septemba, 2013
No comments:
Post a Comment