ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 16, 2013

TEC yataka Kamishna wa Polisi Z’bar afukuzwe kazi

Kamishana wa jeshi la Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa
Kamishana wa jeshi la Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa

Tukio la kumwagiwa tindikali Padri wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, Joseph Mwang’amba huko Zanzibar limechukua sura mpya baada ya Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) kumtaka Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa kufukuzwa kazi.

Makamu Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi aliliambia gazeti hili jana kuwa anapaswa kuondolewa kwa sababu ya kukithiri kwa matukio hayo visiwani.

Askofu Niwemugizi alisema kamanda huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa ameshindwa kukamata watu wanaofanya vitendo viovu dhidi ya viongozi wa dini.

Kwa upande wake Kamishna Mussa alisisitiza hawezi kujiuzulu na kwamba anayestahili kulaumiwa ni Mkurugugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa sababu kwa upande wake alishawakamata watuhumiwa wa matukio hayo.

“Kazi yangu mimi ni kupeleleza na kukamata watuhumiwa,ila kazi ya kushitaki watu ni ya DPP hivyo mimi siyo wa kulaumiwa’Alisema .

Hili ni tukio la nne la uhalifu dhidi ya viongozi wa dini huko Zanzibar baada ya kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wakati Padri Ambrose Mkenda alipigwa risasi na Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhili Soraga alimwagiwa tindikali.

Katika hatua nyingine, Askofu Niwemugizi alisema kuwa matukio hayo kwa sasa yamekuwa wazi kwamba ni mpango wa kuangamiza Ukristo na Wakristo kwa ujumla katika Visiwa vya Zanzibar.

“Uchochezi umefanywa wa kuhamasisha chuki dhidi ya Ukristo unasikitisha. Tulikaa kama Wakristo tukaiambia Serikali mambo ambayo inaweza kufanya kukomesha vitendo hivi, lakini hadi sasa hakuna lililotekelezwa,” alisema na kuongeza:

“Awali ilielezwa kwamba siyo sababu ya kidini, watu wa Kikundi cha Uamsho ndiyo walioanzisha moto huo na wanauendeleza, hali inatisha zaidi kwamba hata jamii ya Wazanzibar haionyeshi nia ya kushiriki kukomesha ukatili huu, kama huyu Padri Mwang’amba amemwagiwa kwenye kituo cha intaneti ni eneo ambao lina watu mbona mhusika hajakamatwa? alihoji.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Maadili kwa Jamii kwa Viongozi wa Dini ya Kikristo, Mchungaji William Mwamalanga alisema kuwa Kamishna huyo wa Polisi anatakiwa kufukuzwa kazi kwa kuwa anaichafua Zanzibar kwa kushindwa kudhibiti matukio hayo ya uhalifu kwa makusudi, pia amejaa udini.
Padri alitishiwa kifo miezi mitatu kabla

Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana, imebainika kuwa alitishiwa kuuawa miezi mitatu kabla ya kukutwa na tukio hilo.

Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.

Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Dk Shein alisema Polisi inatakiwa kuongeza nguvu za uchunguzi ili kukabiliana na matukio ya kikatili ya umwagaji wa tindikali, yanayoshamili visiwani humo hivi sasa.

“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee … ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Dk Shein.

Dk Sheni alisema, kitendo hicho ni cha kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo.

Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.

“Unajua kawaida ya watu wa Zanzibar hufanya mazoezi barabarani, sasa kipindi anapita eneo hilo katika kilima, kuna mtu alimwambia atamfanyia kitu kibaya ambacho hatujui ndiyo hiki au la,” alisema Padri Assenga na kuongeza:

Alisema Juni mwaka huu mara baada ya kupewa vitisho hivyo alikwenda kutoa taarifa kwa Sheha wa eneo hilo na kituo cha polisi.

“Mara baada ya kutolewa vitisho hivyo Juni mwaka huu, alichukua jukumu la kwenda kutoa taarifa kwa mkuu wa eneo hilo (Sheha) na kituo cha polisi.”

Akielezea tukio la kumwagiwa tindikali Padri Mwang’amba, alisema alimwagiwa saa 9:45 alasiri juzi wakati akizungumza na simu nje ya internet café iliyopo eneo la Mlandege.

Padri Assenga alisema kabla ya kumwagiwa tindikali, Padri huyo alikuwa ndani ya internet akitoa ‘photocopy’ za nyaraka. Alipokuwa akitoa ‘photocopy’ (nakala) alipigiwa simu na mtu ambaye anamfahamu hivyo ikabidi atoke nje kuongea naye, lakini alivyokuwa akiongea alimwona kijana akija na kikopo alichokishika mkononi na kummwagia na kukimbia kuelekea katika mitaa ya eneo hilo,” alisema Padri Aseenga.

Alisema mara baada ya hapo, alipelekwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, kwa matibabu baada ya kujeruhiwa usoni, kifuani na mikononi ambapo hivi sasa afya yake inaendelea vizuri.

Naye , Msemaji wa Jeshi la Polisi, Zanzibar Mohamed Muhina alisema, hana taarifa hizo za vitisho na kuahidi kulifanyia kazi.

“Tukio limetokea mchana kweupe na watu walikuwapo lakini wananchi wamekuwa hawatupi ushirikiano hivyo tunawaomba kutupa ushirikiano ili kukomesha vitendo hivi,” alisema Muhina.

Tukio lilivyokuwa
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo, Padri Mwang’amba alisema kwamba lilitokea nje ya duka linalotoa huduma za mawasiliano ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege Wilaya ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.

Padri Mwang’amba akimweleza Dk Shein kuwa hali yake ni nzuri na anaweza kuona vizuri, lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua katika sehemu za usoni na machoni mwake.

“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi,” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake kwa kutoathirika sana.

Uwanja wa Ndege
Katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Kiongozi huyo aliwasili saa 4.16 asubuhi na ndege ya Shirika la Costal akiongozana na Padri Assenge.

Kiongozi huyo aliyekuwa akitembea taratibu, huku akijitahidi kujifunika mwili wake na kanga kuzuia mwanga wa Jua kutokuathiri zaidi mwili wake ulioathiriwa na tindikali.

Chanzo; Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Mimi pia kwa upande wangu kwa sasa nafikiri hawa wakurugenzi wa mashitaka ya jinai nao, nafasi zao zingefutwa tu sababu wananchi wa kawaida hatuoni umuhuímu wa nafasi zao na hata kiutendaji kwa bara na hata visiwani. Sanasana wamekuwa wakilinda maslahi ya watu flani flani au tabaka flani.

Anonymous said...

Afukuzweeee kazi Mara moja! Uwajibikaji wake umekuwa hovyoooo na msaidizi wake afukuzwe pia! Kazi imewashinda kabisa!!!!!!!!! ZANZibar ugaidi umetawala. Hakuna Amani tena! Rais wa Zanzibar Naye uwajibikaji ni viiipi kwani? !