ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 30, 2013

Waliomwagiwa tindikali wafunguka

Wakati Rais Jakaya Kikwete akiahidi kumaliza balaa la watu kumwagiwa tindikali nchini kote, hali ni tete visiwani Zanzibar na baadhi ya wananchi bado wamejawa hofu.

Mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete alimwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon kuwa chimbuko la tatizo hilo lina sura nyingi lakini hakuna shaka kuwa katika kipindi kifupi kijacho serikali yake italimaliza tatizo hilo.

Aliongeza kuwa hivi karibuni, Jeshi la Polisi lilifanya operesheni kubwa katika mitaa ya Zanzibar na kukamata watu 10 kwa tuhuma za kushiriki mipango ya kuandaa na kutekeleza vitendo hivyo.

Rais Kikwete alitoa msimamo huo wakati akizungumza na Ban Ki Moon ofisini kwake jijini New York, Marekani baada ya kuwa ameulizwa jambo hilo.

“Ni kweli tumekuwa na vitendo hivyo, zaidi visiwani Zanzibar kuliko Bara ambako hata hivyo nako vimekuwapo vitendo hivyo. Ni jambo la kulaaniwa sana na karibuni Jeshi la Polisi lilifanya operesheni maalum na msako mkubwa Tanzania Visiwani ambako watu 10 wametiwa mbaroni na watafikishwa katika vyombo vya sheria.”

Rais Kikwete alisisitiza: “Wakati lilipoanza tatizo hilo, tulidhani kuwa alikuwa ni Sheikh Soroga aliyekuwa anatafutwa peke yake na watu ambao walikuwa hawakubaliani kisiasa na msimamo wake, lakini mara wakaanza kushambuliwa watu wengine wakiwamo wasichana wawili wa Uingereza ambao walikuwa wanafanya kazi za kujitolea tu. Tatizo hili ni lazima likome.”

Uchunguzi wa NIPASHE visiwani Zanzibar umeonyesha kuwa hofu bado imetawala kwa wananchi wengi kuhusiana na matukio ya watu wasio na hatia kumwagiwa tindikali.

Mmoja wa waathirika, Sheikh Fadhil Soraga alikataa kuzungumzia suala hilo huku baadhi ya watu wake wa karibu wakisema kuwa amechukua hatua hiyo kutekeleza rai ya familia yake ambayo bado imejawa hofu kwa vile hadi sasa hakuna mtuhumiwa yeyote wa tukio hilo aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Sheha wa Tomondo, Mohamed Kidevu, ambaye pia alijeruhiwavibaya baada ya kumwagiwa kimiminika hicho, naye vilevile alisema kuwa hofu bado haijamtoka kwa vile watuhumiwa bado hawajakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

Katibu wa Kanisa la Anglikana visiwani Zanzibar, Nuru Justine Sallanya, alisema kuwa yeye na viongozi wenzake wa dini wanasikitishwa na matukio ya tindikali na kushangazwa na hatua ya kutofikishwa mahakamani kwa watuhumiwa.

Mwingine aliyezungumzia hofu ya matukio ya watu kumwagiwa tindikali Zanzibr ni Padri Cosmas Shayo wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph, Shangani mjini Zanzibar.

Alisema kinachowatia hofu ni kuona kuwa hakuna mtuhumiwa yeyote wa matukio ya tindikali aliyefikishwa mahakamani visiwani humo.

Hivi karibuni, Padri Ancelmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Cheju alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana na sasa anaendelea kuuguzwa nchini India.
Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Ali Msuko, aliwahi pia kumwagiwa tindikali wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 1995 na anasema kuwa hofu imewajaa wananchi wengi kwa sababu watuhumiwa hawajawahi kufikishwa mahakamani.

Ufuatao ni muendelezo wa simulizi kuhusiana na uchunguzi uliofanywa na NIPASHE visiwani Zanzibar juu ya matukio mbalimbali ya watu kumwagiwa tindikali. Simulizi hii ilianza Ijumaa na kuishia mahala ambako Msuka alikuwa akieleza namna ilivyokuwa wakati yeye alipokumbwa na balaa hilo kisiwani Pemba.

“Ilikuwa usiku, muda kama wa saa 2:00 hivi. Nikawa napita maeneo ya Mtemani Maghorofani ambako ndiko nilikokuwa nikiishi. Ghafla nikamwagiwa tindikali na mtu nisiyemfahamu. Niliumia sana maeneo ya shingoni, kifuani na kuelekea chini,” anasema Msuko.

“Nikalazwa katika Hospitali ya Wete, baadaye nikahamishiwa Mnazi Mmoja na mwishowe nikapelekwa India ambako nilifanyiwa operesheni mbili, ikiwamo ya kuhamisha ngozi kutoka mapajani kwenda kifuani… nilitibiwa kwa wiki sita,” anasema.

“Cha kusikitisha ni kwamba mtu aliyetuhumiwa kunifanyia unyama huo aliachiwa mwaka 2004… hadi leo nimekuwa mtu tofauti, nina mwonekano tofauti na mke wangu alilazimika kuwa mvumilivu sana katika kipindi chote cha kuugua.

“Leo hii nimekuwa nikiumia sana kila ninaposikia watu wengine wakimwagiwa tindikali na hakuna anayefikishwa mahakamani.

Mimi naamini kuwa nyuma ya matatizo haya yote ni siasa. Polisi wanapaswa kuongeza kasi yao katika upelelezi wa kila tukio na kuwafikisha mahakamani.

Wasipokamatwa, matukio haya yatazidi kutokea kwa visingizio mbalimbali. Ni kwa sababu wahalifu watajiona kuwa wana nguvu na hakuna wa kuwababaisha,” anasema.

Akieleza zaidi, Msuko anasema kuwa kwa mtazamo wake, tofauti za kisiasa zinaweza kuwa miongoni mwa vyanzo vya mashambulizi ya tindikali yanayoendelea sasa visiwani Zanzibar.

Msuko anaongeza kuwa zoezi la uandikishaji wa wakazi wa Zanzibar katika kila shehia, ambao mwishowe ndiyo huwapata watu wenye sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuwa chanzo cha baadhi ya matukio ya watu kumwagiwa tindikali.

Anasema sheria ziko wazi, zikimtaka kila Mzanzibari awe amekaa kwenye eneo lake kwa walau miaka mitatu ili apate sifa za kuandikishwa.

Hata hivyo, kuna watu hutaka waandikishwe katika maeneo wasiyokaa kwa kipindi hicho na mwishowe kuibuka mgogoro pindi sheha akiwakatalia.

“Ni vyema wananchi wote wakahimizwa kulinda amani na kuwafichua bila woga watu hawa wanaodhuru wenzao kwa tindikali.”

PADRI COSMAS SHAYO
Miongoni mwa waathirika wakubwa wa matukio ya mashambulizi ya kinyama visiwani Zanzibar ni Kanisa la Katoliki.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwishoni mwa mwaka jana Padri wao Ambrose Mkenda alijeruhiwa kwa risasi na hadi sasa anaishi na kovu kubwa mwilini.

Wamempoteza pia Padri Evaristus Mushi, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwanzoni mwa mwaka huu.

Na Septemba 14 mwaka huu, siku chache tu zilizopita, Padri Ancelmo Mwang’amba amekumbana na tukio jingine baya la kumwagiwa tindikali. Ni mfululizo wa matukio ya kuhuzunisha dhidi ya viongozi wa kanisa hilo ndiyo ulionilazimu kwenda pale kwenye makao makuu yao, Parokia ya Mtakatifu Joseph, eneo la Shangani.

Ile kufika tu, nikakutana na bango kubwa lililowekwa juu ukutani, bila shaka ni kwa nia ya kutoa nafasi kwa kila muumini wao anayefika mahala hapo kusoma ujumbe uliopo na kuufanyia kazi.

“Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.” Ndivyo ujumbe huo ulivyosomeka, ukikariri maandiko matakatifu ya Biblia, Mathayo 5:44.

Ujumbe huu uliobebwa kuadhimisha miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Kanisa Katoliki visiwani Zanzibar ulinishangaza.

Ni kwa sababu ulielekea kupoza nafsi za waumini wa kanisa hilo katika kipindi hiki kigumu zaidi kwao. Nikajiambia kuwa nitakapopata nafasi ya kuzungumza na askofu wa jimbo hilo, Mhashamu Augustino Shao, lazima nimuulize sababu za kupeana ujumbe ule.

Hatimaye nikajitoma ndani ya ofisi za uongozi wa kanisa hili. Baada ya kueleza dhamira yangu ya kuonana na Askofu Shao, nikapata maelezo kuwa kamwe isingewezekana kwa siku hiyo kwani ratiba yake ilibanwa na shughuli nyingi.

Badala yake, nikapewa nafasi ya kuonana na mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. Alikuwa ni Padri Cosmas Shayo.

Hakika, nilijiona kuwa ni mwenye bahati. Huyu pia alinipokea vizuri sana. Hata hivyo, baada tu ya kuketi kwenye kiti alichonikaribisha na kusalimiana naye kwa bashasha, Padri Shayo aliniambia kwa utani yaliyo moyoni mwake: “Ndugu yangu, kama usingekuja na huyo bwana ambaye ni rafiki yangu sana (mwenyeji wangu aliyeniongoza kufika mahala hapo), ni lazima ningekutimua au mimi mwenyewe ningetimka… hali ya kuaminiana imepungua, tumejawa hofu dhidi ya tusiowafahamu.”

Baada ya kuniambia hayo nikapata pa kuanzia. Padri Shayo akanieleza bila kificho kuwa wao (viongozi wa Kanisa Katoliki Zanzibar) wamejawa na hofu kubwa. Hawajui baada ya wenzao kudhuriwa ni nani atakayefuata. Na kinachowatia hofu zaidi ni kutotiwa hatiani kwa wahalifu wanaoendeleza mashambulizi ya kinyama dhidi yao.

“Nyoyo zetu zimejawa hofu…hatujui chanzo cha kuibuka kwa mambo haya, hatujui ni nani hasa wako nyuma ya matukio haya hata mkono wa dola usiwafikie, na hatuelewi hao wanaofanya unyama huu wana dhamira gani,” anasema Padri Shayo.

“Binafsi naona kuwa kizazi kipya ndicho kinatuvuruga… sielewi tatizo ni nini. Kama ni masuala ya Muungano (wa Tanganyika na Zanzibar), yanahusiana nini na mashambulizi haya (dhidi yetu).

Kama ni dini, mbona tumekuwa kwa miaka yote tukiishi kwa amani na upendo baina yetu (Wakristo) na Waislamu.

“Kanisa hili liko hapa (Zanzibar) kwa miaka mingi sana... hata enzi za utawala wa Sultan hakujawahi kuwa na mambo haya. Katika dunia ya leo, hamuwezi kuishi mkiwa Wakristo peke yenu.

Na wala hamuwezi kuishi mkiwa Waislamu peke yenu. Serikali ni lazima itumie vyombo vyake kukomesha mambo haya,” anasema Padri Shayo aliyetua Zanzibar tangu mwaka 1976.

“Vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Sisi tumekuwa na kazi ya kuwasihi waumini wetu wawe na moyo wa subira na kusamehe. Ujumbe wetu siku zote umekuwa huo (kama ule uliobandikwa ukutani).

Hata hivyo, mfululizo wa matukio haya unatupa wakati mgumu wa kuwasihi baadhi yao ambao wanaelekea kuchoshwa na rai ya kuwataka wasamehe mara sabini.

Mkenda kapigwa risasi, Mushi kauawa, leo hii Mwang’amba kamwagiwa tindikali… tunafanya kazi kubwa sana ya kuwatuliza.

“Ila jambo moja tu linalotushangaza ni kwamba kwa nguvu zake Mungu, sasa waumini wetu wanaongezeka… hata wale waliokuwa hawafiki kanisani mara kwa mara sasa wamekuwa karibu zaidi kufika kwa wingi sana.

“Imani yetu kwa serikali ni kuona kuwa matukio haya yanakomeshwa, wahusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua zinazostahili. Hatutarajii kusikia kuwa hakuna ushahidi.”

KATIBU ANGLIKANA
Safari yangu ilinifikisha kwa Katibu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar. Huyu anaitwa Nuru Justine Sallanya. Ofisi za kanisa hili ziko pale Kiungani, pembezoni tu mwa Bahari ya Hindi.

Siku hii nilikuwa na bahati ya pekee. Nilimkuta katibu huyu akijiandaa kutoka, tena tayari akiwa nje ya ofisi yake. Hata hivyo, baada ya kujitambulisha na kueleza kusudio la kuzungumza naye, alisitisha kila kitu. Akaongozana nami hadi ofisini kwake na kunikaribisha kiti.

Sikutaka kumchelewesha zaidi. Nikataka anipe maoni yake kuhusiana na tukio la hivi karibuni la kumwagiwa tindikali kwa Padri Mwang’amba. Nikataka anieleze pia kile anachoamini kuwa ndiyo chanzo hasa cha kuibuka kwa mashambulizi dhidi ya viongozi wenzao wa dini na nini kifanyike.

“Tuko kwenye kipindi cha mshangao. Hatujui nini motives (sababu) za yote haya,” anasema.

“Huko nyuma tulikuwa tukiishi vizuri sana. Hakuna tishio lolote la mambo haya. Amani ilitawala. Lakini sasa ni tofauti sana… hatujui ni nani sasa atakayeshambuliwa, wapi atashambuliwa na ni kwa wakati gani.

“Inaogopesha sana. Inawezekana haya mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na pengine kidini ni sababu za kutokea kwa yote haya,” anasema Nuru.

Akiongeza, Nuru anasema: “Linalovunja moyo zaidi ni kutoona yeyote akifikishwa mahakamani… hii maana yake ni kwamba wahalifu wanazidi kujengewa imani kwamba wao ni jasiri. Na hili si jambo zuri. Ni hatari sana.

“Mimi naona kuwa sasa hii serikali ya Umoja wa Kitaifa haina tena legitimacy (imepoteza uhalali). Ni kwa sababu mambo haya yanayotokea yanabomoa misingi ya kuundwa kwake.

“Ikumbukwe kuwa wakati wa kuundwa kwake, sote tuliamini kuwa hali ya amani itazidi kushamiri. Lakini sasa inakuwa kinyume chake. Wengine tunaanza kuona kuwa ni afadhali ilivyokuwa mwanzo kabla ya kuwapo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ni vyema serikali ikahakikisha kuwa inatekeleza wajibu wake wa kulinda raia… wahalifu wakamatwe na kuchukuliwa hatua.”

ITAENDELEA KESHO

CHANZO: NIPASHE

No comments: