ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 29, 2013

HUKUMU YA WALIOTAKA KUMUUA NYERERE 1983

Walioshitakiwa kwa uhaini mwaka 1983 walikuwa wengi.
Ilielezwa mbele ya jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Nassor Mzavas kwamba washitakiwa walikuwa 19.
Miongoni mwao alikuwepo Thomas Lugangira au ‘Uncle Tom’ au ‘Uncle Check bob.’

Wenzake walikuwa ni Hatibu Gandi au ‘Hatty Mac Ghee’, Kapteni Mohammed Tamim, Kapteni Mbogoro, Kapteni Christopher Kadege, Luteni Badru Rwechungura Kajaja na Kapteni Mapunda.

Wengine walikuwa ni Banyikwa na mkewe, Christopher Ngaiza, Zacharia Hans Pope , Kapteni Rodrick Rosham Robert na wengine kibao ambao jumla yao walikuwa 19.

Wakati kesi inaendelea Lugangira na Hatty Mc Ghee walipanga njama na kufanikiwa kutoroka kutoka katika Gereza la Keko, Dar.
Ilidaiwa kuwa walitorokea nchini Kenya. Baada ya kufika Kenya, Lugangira akatorokea Uingereza. Hatty Mc Ghee alikamatwa na kurudishwa Tanzania kwa kubadilishana na mtu mmoja aliyekuwa akitakiwa Kenya aliyetajwa kwa jina la Private Hezekiah Ochuka ilidaiwa kuwa alifanya ‘madudu’ huko Kenya.

Mc Ghee aliporejeshwa nchini aliunganishwa na wenzake na kesi ikapamba moto.
Toleo lililopita nilieleza jinsi Komandoo Tamim alivyouawa wakati wa kurupushani za kumkamata pale Kinondoni Mkwajuni.

Lakini hata mahakamani wakati wa kutoa ushahidi juu ya komandoo huyo mwana usalama mmoja aliyekuwa akiitwa Mr X alisema walijaribu kumkamata lakini akawatoroka kwa kuruka ukuta wa nyumba aliyokuwa akiishi.

Akasema wakati wakimkimbiza Komandoo Tamim alidandia gari moja pick up iliyokuwa imebeba masanduku ya bia na kuanza kuwarushia wana usalama waliokuwa wakimkimbiza, hivyo akapigwa risasi na kufa.

Kesi hiyo ya uhaini ilikuwa inasisimua sana haswa maswali ya wakili wa utetezi aliyekuwa akiitwa Murtaza Lakha. Mawakili wengine wa utetezi ninaowakumbuka kwa jina moja moja ni Mucadam, Jadeja na Tarimo.
Upande wa serikali ulikuwa unaongozwa na Wakili William Sekule, pia alikuwepo Johnson Mwanyika.

Wakili Sekule alileta mashahidi kadhaa ambao walisumbuliwa sana na mawakili wa utetezi haswa Murtaza Lakha.
Jaji Mnzavas alitoa hukumu Desemba 28, 1985 ambapo washitakiwa wengine aliwafunga kifungo cha maisha na wengine walifungwa miaka kadhaa lakini Banyikwa na Ngaiza waliachiwa huru. GPL

No comments: