ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 29, 2013

KUNA NYAKATI MTAGOMBANA, MTANUNIANA, HIVYO HAIONDOI UKWELI KUWA MNAPENDANA - 8

WIKI iliyopita katika makala haya nilikutaka uwe na matarajio chanya, kwamba vyovyote itakavyotokea, inakupasa utambue kuwa yeye ni mpenzi sahihi kwako na anaweza kubadilika kuwa bora zaidi ya hapo.

Ni kweli mmegombana na ni wazi hamuivi leo kwa sababu kuna masuala yanawagombanisha lakini wewe jenga matarajio chanya juu yake halafu pita njia sahihi wakati wa kuishi naye. Anakuudhi, pengine anakufanya mpaka ukose usingizi, swali la kujiuliza ni moja tu; je, mnapendana?

Maudhi na migogoro, haviondoi ukweli kwamba mnapendana. Kichwani weka imani kwamba baada ya migogoro na maudhi kuna maisha mazuri yaliyojaa maelewano ambayo yatatamalaki. Huu ni muongozo ambao ukiushika kikamilifu, utakupa dira sahihi ya maisha yako.

Mtu aliye na matarajio chanya kwa mwenzi wake, hawezi kuyumbishwa na vitu vidogovidogo. Hatakimbilia kutamka maneno mabaya dhidi ya mpenzi wake kwa sababu ndani yake kutakuwa na imani kwamba wanapendana na huko mbeleni mambo yatakaa sawa, isipokuwa sasa kuna mambo tu ya mpito yamejitokeza.

Migogoro ni Shetani, ukiruhusu itawale maana yake uhusiano wenu hauna baraka za Mungu. Hapa namaanisha kwamba kama ni ndoa basi haimpendezi Maulana. Tafakari sasa ni kwa nini ndoa yako haipo kwenye jicho limpendezalo Mungu? Chukua hatua.

Kufukuzana ni tafsiri ya Shetani kushinda, pingana na utawala wa ibilisi katika uhusiano wako kwa kuweka matarajio chanya kwa mwenzi wako. Kila siku mkigombana, tafuta suluhu naye halafu amini kwamba kwa mwendo wa taratibu atakaa sawa na kukidhi vigezo unavyotaka.

AMINI KWAMBA ULIYENAYE NDIYE ANAKUFAA
Ukigombana na mwenzi wako kisha ukamnanga kisawasawa kuwa hakufai unapotoka. Aidha, limepita gogoro la kiwango fulani ndiyo unaamua kuwaza na kujipa majibu ya uongo kuwa mpenzi wako uliyenaye hakufai. Ni makosa makubwa ambayo hutakiwi kuyafanya.

Yupo ambaye tabia yake ni kumlinganisha mwenzi wake na watu wengine kisha anatomtoa kasoro. Katika pointi hiyo, mwenye makosa ni wewe na hiyo ni kuonesha jinsi ambavyo ulivyo hujiamini. Amini kwamba uliye naye ndiye mpenzi bora chini ya jua.

Ikiwa kila siku kila mmoja atatembea akiringa kuwa na mwenzi aliyenaye, haitatokea kuachana. Kwanza sababu ya kumwagana itakuwa nini? Wengi huona kutengana ni suluhisho kwa vile ndani yao hujawa na kiburi kwamba wapo wazuri zaidi mbele ya safari ya maisha yao.

Mheshimu mwenzi wako na uishi naye kama vile ndiyo umefika ukingoni na huhitaji zaidi tena. Hiyo ikiwa kanuni yako, utaona jinsi ambavyo utaishi kwa kumheshimu mpenzi wako. Mkigombana, utamuomba msamaha haraka maana ndiye pekee unamhitaji.

Vilevile kama atakuomba msamaha, utamsamehe haraka kwa maana hutaweza kuhimili hali ya kukosa maelewano naye kwa sababu yeye ndiye kila kitu kwako. Hivyo basi, acha fikra mbaya, heshimu chaguo lako, amini kwamba yeye ndiye mpenzi bora na wengine ni fotokopi.

HITIMISHO
Maisha hayako tambarare peke yake, mabonde na milima lazima ukutane navyo. Mapenzi siyo kila siku yatakufanya uwe na tabasamu, zipo nyakati ambazo utalazimika kuwaza au pengine kuumia kabisa.

Siku zote katika maisha yako, pambana kupata furaha. Ikitokea wewe na mwandani wako picha haziendi kutokana na tofauti za hapa na pale, wajibu wako ni kuirekebisha hiyo hali kwa haraka ili tabasamu lenu lirejee.

Ni vizuri kuzingatia kwamba upo uhusiano uliovunjika si kwa sababu wahusika walikuwa hawapendani, bali wenyewe waliamua kulea migogoro na chuki zisizo na maana. Tambua na uweke akili; Inauma sana kuachana na mtu unayempenda.

Wapo watu ambao wameachana mpaka imepita miaka lakini kila siku wanakumbukana. Wanauliziana hadi maisha yao ya kimapenzi yanavyoendelea. Wanashindwa kuutambua ukweli kwamba kinachowasukuma kufanya hivyo ni mapenzi ya dhati yaliyomo myooni mwao.

Hapa naomba nifafanue kitu; Unaweza kuwa na mapenzi ya dhati na mtu hata asiwe mwenzi wako. Ndani ya nafsi yako utakuwa unajihisi una kitu kuhusu yeye. Utapenda kujua habari zake, shangaa kwamba ukimuona yupo na mpenzi wake unaweza kuumia.

Inaweza kutokea wewe na yeye, wote mnapendana tena kwa penzi la dhati lakini hamjapata kuwa pamoja. Wapo ambao wamezeeka wakiwa marafiki walioshibana, wenye kusaidiana katika shida na raha. Hao walijiwekea tu ukuta uliowazuia kukamilisha penzi lililopo ndani yao.



Hivyo basi, hata hao waliochana lakini bado wanakumbukana, watakuwa wanalazimishwa na nyoyo zao kutambua uwepo wa wapenzi wao waliopita. Kujua wanaendeleaje kiafya, kimapenzi na kimaisha kwa jumla. Wengine hulazimisha kubaki marafiki.

GPL

No comments: