Monday, October 28, 2013

WATANZANIA UGHAIBUNI WAHAMAMISHWA KURUDI NYUMBANI KULETA CHACHU YA MAENDELEO.

Afisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT-Geoffrey Kirenga akielezea mengi
Afisa Ubalozi Caroline Chipeta akifungua mkutano
Mbunge Profesa Peter Msolla akisisitiza haya ya kuendeleza Sayansi na Teknolojia
Mdau Zuberi akiuliza swali
Mhandisi Mbogo Futakamba akiwasihi Watanzania warudi nyumbani kuchangia maendeleo
kwa picha zaidi na maelezo bofya soma zaidi
Mtanzania mkazi Uingereza akiuliza swali
Muda wa maswali na majibu
Watanzania waliokuwepo wakichangamkia maongezi
Waziri Mhandisi Christopher Chiza akiwahutubia Watanzania London
Yusuf Kashangwa- Mkurugenzi wa Kituo Cha Biashara Ubalozini akizungumza
pic by Urban Pulse.com

Watanzania wakazi Uingereza wamehakikishiwa kuwa taaluma na uzoefu wao ughaibuni vitasaidiwa na vyombo husika vya serikali wakirejea na zana, mbinu na uwekezaji wa kilimo.
Kauli hii ilitolewa na msafara mzima wa viongozi uliofuatana na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alipokutana na Watanzania Ubalozini, London , Jumatano tarehe 23 Octoba 2013 .
“Malengo makubwa,” alieleza Waziri, “ ni usalama wa chakula na kujitosheleza kupanda mazao msingi kama mahindi, sukari na mchele. Tunachotaka ni maendeleo ya kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha biashara. Nyinyi mnaweza kuwekeza katika uwezeshaji wa kilimo badala ya kununua kifaa kimoja kimoja.”
Akitoa mfano alisema Mtanzania aliyeshaishi ugenini anayetaka kuchangia atafanya bora zaidi kinyume cha kutafuta mbolea na kifaa kimoja, kimoja kuwa vifaa vikubwa ambavyo wakulima na jumuiya nzima vyaweza kukodisha.
Akifafanua zaidi Waziri Chiza aliyekuja Uingereza kwa mwaliko wa siku tano wa kiserikali alisema ni vyema Watanzania walioko ughaibuni kutafiti hali ikoje nyumbani. “Utafiti si kuingia mitandao ya Google na kujisomea tu. Njooni ubalozini maana hapa kuna habari za ukweli. Serikali inaweza isijibu ombi la mtakaji haraka kama watu binafsi; hivyo ni vyema kufika ubalozini kupata habari za undani zaidi.”
Waziri alisisitiza kilimo chetu bado ni cha kizamani –kinachotegemea jembe la mkono kwa asilimia 64, “nyinyi mlioshatembea tembea” mnaweza kuchangia na “sisi tuko tayari kuwasaidia kutimiza malengo.”
Akiendeleza mada hii, Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Profesa Peter Msolla alisema vyombo vyote vya kimaendeleo nchini vinahitaji sayansi na teknolojia. “Kila kitu- maji, kilimo, mifugo- vyahitaji sayansi.”
Profesa Msolla alisema nchi yetu inahitaji sana waalimu wa sayansi. “Twahitaji waalimu wa fizikia na hesabu. Waalimu walio wabunifu watakaowafanya wanafunzi wayapende masomo hayo.”
Akiueleza umati huu uliomsikiliza kwa makini, Profesa Msolla ambaye aliyekuwa zamani Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia alitoa mfano wa Chuo cha Mkwawa chenye wanafunzi 3,000. Akasema kati ya wanafunzi hao, 156 tu ndiyo wanachukua hesabu na sayansi. “Vijana wengi leo hawapendi hesabu wala sayansi,” alilalamika.
Naye, kiongozi mwingine msafarani, Geoffrey Kirenga, alisisitiza kuwa dosari zote za umaskini na uchumi zinatokana na uhaba wa watalaamu.
Bwana Kirenga ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu, kituo maalum cha uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini Tanzania (SAGCOT) alieleza hatua kuu ya maendeleo haya ni kutoa elimu kwa mabwana shamba. Alitaja mfano wa mkulima anayepanda mazao bila mpango. “Akifika sokoni kuuza anakuta pia wapo wenzake wengi waliyoyapanda. Matokeo yanatupwa. Mwaka unaofuata anaamua kutoyapanda- yakipungua sasa bei inapandishwa. Tatizo ni la upangaji na taaluma nchini. Tunahitaji sana watalaamu.”
Akizungumzia mfano wa zao la mchele ambalo hutoka zaidi bara Asia, Bwana Kirenga aliitaja Japani kaskazini inayozalisha tani 5 na nusu kwa mwaka. “ Kilombero inaweza kuzalisha zaidi ya Mjapani.”
Hoja ilikua nzito aliposema bara la Afrika linatazamia kulisha dunia inayoendelea kuongezeka idadi ya watu. “Iweje sisi tuendelee kuagiza vyakula kama mafuta ya kupikia na viazi mviringo toka Uholanzi ilhali twaweza kupanda vyote hivyo?”
Naye Mhandisi Mbogo Futakamba alikumbusha haja ya taaluma ya kiakili nyumbani kwa kusisitiza namna fikra na” chachu ya kimtazamo “ inavyotakiwa.
“Nyinyi mnafanya kazi na Wazungu. Ukiishi na mzungu unajifunza nidhamu ya kazi. Hapa maisha ni ya kukimbia. Si kama nyumbani unasema n’takwenda kwa mjomba kuvizia chakula. Hivyo basi mkitumia nguvu ile ile mliyonayo huku ughaibuni nyumbani- tukiwa kama 50 tunaweza kutoa mchango mkubwa.”

Imeandaliwa kwa ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Uingereza, Urban Pulse na Freddy Macha

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake