ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 23, 2013

[AUDIO] DAKIKA 90 ZA DUNIA: Miaka 50 tangu kuuawa kwa Rais John F Kennedy

 
Ijumaa wiki hii, Marekani imeadhimisha nusu karne tangu kuuawa kwa Rais wa 35 wa taifa hilo, John F Kennedy aliyeuawa Novemba 22, 1963 alipokuwa akisafiri kwenye gari la wazi jijini Dallas
Rais John F Kennedy akiwa katika gari la wazi muda mchache kabla hajauawa kwa risasi. Pembeni yake ni mkewe na mbele yake ni aliyekuwa Gavana wa Texas John Bowden Connally, Jr.ambaye pia alijeruhiwa katika shambulio hilo
Kwa wiki nzima, kumekuwa na shughuli mbalimbali kukumbuka tukio hili lililoshitua wengi nchini humo. Mambo mengi yametendeka. Vitabu vipya vimeandikwa na watu wamezungumzia kuuawa kwa Rais huyo pamoja na ufuasi alioacha kwenye uongozi mpaka sasa. Na kama ilivyotegemewa, Kengele ziligongwa, maua yaliwekwa kwenye kaburi, bendera zilipepea nusu mlingoti na nyimbo mbalimbali ziliimbwa
Rais Barak Obama, aliadhimisha kumbukumbu hizo Jumatano wiki hii kwa kuweka shada la maua kwenye kaburi la Rais Kennedy na pia kutoa tuzo za heshima kwa watu mbalimbali akiwemo Rais mstaafu Bill Clinton, mwanahabari maarufu Oprah Winfrey na wengine 14.
Rais Barack Obama (wa pili kulia) akiwa na mkewe Michelle, Rais mstaafu Bill Clinton (wa tatu kulia) na mkewe Hillary Clinton wakitoa heshima mbele ya kaburi la JFK jumatano wiki hii.

Hii ni sehemu ya ripoti ya Jamii Production kwenye kipindi cha DAKIKA 90 ZA DUNIA kinachorushwa na kituo cha Radio cha Capital FM cha Dar Es Salaam Tanzania kila Jumamosi kuanzia saa moja na nusu asubuhi (7:30 AM).
Bahati Alex (L) Capital Radio Jijini Dar es Salaam na Mubelwa Bandio (R) wa Jamii Production Washington DC
Hii ilikuwa ripoti ya Novemba 23, 2013

No comments: