ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 23, 2013

UMEMPA SABABU YA KUWA NA WEWE?

KARIBUNI kwenye uwanja wetu tujadiliane kuhusu mapenzi. Marafiki zangu, katika uhusiano umakini wa hali ya juu huhitajika ili uweze kuwa bora kila siku na kuufanya uhusiano wako kuwa wenye nguvu na usiotetereka! Katika hili hutegemea zaidi jinsi unavyoendesha uhusiano wako.

Ukitaka mpenzi wako akuchoke au umchoke, wewe ndiye mwamuzi, lakini pia ukitaka mpenzi asikuchoke au usimchoke wewe ndiye mwenye uamuzi kwa kuwa una uwezo wa kuyafanya yote hayo. Hebu nikuulize, umempa sababu mwenzako ya kuwa na wewe?

Je, unafanya nini kumfanya mwenzako asifikirie kabisa kuwa na mwingine zaidi yako? Kama nilivyotangulia kusema mara kadhaa huko nyuma kuwa, mapenzi ni sanaa marafiki zangu. Kuna wakati ubunifu unahitajika ili kumfanya mwenzako ajisikie fahari na faraja kuwa na wewe.


Wengi hawaelewi kuhusu hili, anaingia kwenye ndoa na mke wake au mumewe lakini baada ya muda anajikuta mapenzi yakipungua siku hadi siku mpaka anafikia hatua ya kuwa na mtu mwingine nje ya ndoa. Siyo sawa!
Inawezekana ukaendelea kuwa bora kwa mpenzi wako, inawezekana mpenzi wako akaendelea kuwa bora kwako ikiwa utahitaji kufanya hayo kwa dhati. Hakika kama ukitaka unaweza kuendelea kuwa wa kisasa katika uhusiano wako.
Yapo mambo ambayo ukiyafanya kwa ufanisi mkubwa, basi wewe utaendelea kuwa bora kwake naye atakuwa bora kwako. Hakuna kuchokana tena. Bila shaka sasa, hapo utakuwa mwenzi wako sababu hasa za kuwa na wewe. Hebu twende tukaone...

RUDI MWANZO KABISA
Siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa, jinsi unavyoanza ndivyo utakavyomaliza! Waswahili hawakuishia hapo, wakaongeza kuwa: “Unavuna kile ulichopanda!” Naamini katika semi hizo kuna mambo umejifunza.
Kama ulianza vibaya uhusiano wako tegemea kumaliza vibaya, lakini kama ulianza vizuri basi tarajia maisha mazuri ya kimapenzi yasiyo na maumivu katika moyo wako.

Kama unatarajia kuingia katika uhusiano na mpenzi mpya hakikisha hujionyeshi tofauti na hali yako halisi ilivyo. Jifunze kujikubali, hata kama unafanya kazi ambayo unadhani ni ya hadhi ya chini, mbainishe mpenzi wako hali halisi ilivyo. Kama anakupenda, kazi yako haiwezi kupunguza mapenzi baina yenu.

Kudanganya ni utumwa, usikubali kuingia katika utumwa au kifungo cha aina hiyo. Rafiki yangu mmoja alimdanganya mpenzi wake anafanya kazi katika shirika fulani kama kiongozi mkubwa, jamaa hakuishia hapo, akadai mshahara wake ni mkubwa na mambo mengine mengi.

Mpenzi wake kwa kuwa alijua boyfriend wake ana kazi na mshahara mzuri, alikuwa akimsumbua mara kwa mara amfanyie shopping! Kilichotokea hapo ni kwamba jamaa alikuwa akimkwepa kila kukicha. Unajua kwanini? Hana pesa.
Kama asingeongopa usumbufu wote alioupata usingetokea. Marafiki zangu, jifunzeni kujikubali mlivyo, msitake kujionyesha kwa watu mpo katika hadhi fulani kumbe hali halisi haipo hivyo, huo ni ulimbukeni ambao unatakiwa kuushinda.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, All About Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

Kwani kama jamaa angekuwa mkweli kwa mwanamke wake, angesumbuliwa kiasi kile? Inawezekana yule mwanamke alikuwa na mapenzi ya kweli kwa jamaa, lakini kichwani alikuwa akijua kuwa mpenzi wake mambo safi....sasa alikuwa na kosa gani kutaka shopping? Fikiria zaidi.

KUBALI MAISHA YAKO
Itakuwa kichekesho kama utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe hujipendi! Huwezi ukasema unamthamini mpenzi wako wakati thamani yako mwenyewe huitambui.
Naamini tunakwenda sawa, kama unashindwa hata kuoga na kubadilisha nguo safi nani atakayekupenda? Huwezi kuwa wa kisasa kama huzingatii usafi, jithamini.
Mwingine anaweza kukuta anajichukia bila mwenyewe kujua. Unaweza ukamkuta mtu anajitoa kasoro mwenyewe. Siyo sawa. Jipe nafasi ya kwanza. Jiamini.

Acha kujitoa makosa. Jipe moyo, wewe ni mzuri kuliko mwingine. Kikubwa zaidi ni kwamba, wewe utakuwa mzuri zaidi kwa yule ambaye anakupenda tu. Ndiyo ukweli ulivyo marafiki zangu.
Kujikubali ni silaha kubwa sana katika kuupa nguvu uhusiano wako na si uhusiano pekee, bali hata maisha kwa jumla.
Mada bado haijaisha, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, All About Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

No comments: