Golikipa Machachari wa Timu ya Simba,Ivo Mapunda akiruka juu kudaka mpira uliokuwa unaelekea langoni kwake.
Hamisi Tambwe aliendeleza kile anachofanya vizuri kwenye ligi kuu ya Bara msimu huu baada ya jana kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 wa Simba dhidi ya Yanga, lakini mchezaji mpya Awadh Juma alipachika bao lake la kwanza katika mechi za watani wa jadi nchini akicheza kwa mara ya kwanza.
Juma alifunga bao hilo katika dakika ya 64 baada ya kumpokonya mpira Juma Kaseja nje kidogo ya eneo la hatari wakati kipa huyo mpya wa Yanga na wa zamani wa Simba akijaribu kuurudisha ndani ya 18 kwa miguu ili aweze kuucheza kwa mikono.
Katika siku ya kufa nyani kwa Yanga, beki na nahodha Nadir Haroub alionyeshwa kadi nyekundu kutokana na kupata ya pili ya njano katika mchezo huo katika dakika ya 81.
Ikianza mchezo huo wa kirafiki na wachezaji 10 kati ya walioingia uwanjani tangu filimbi ya kwanza kuikabili Simba katika sare ya ajabu ya 3-3 Oktoba 20, na ikiimarishwa na Kaseja langoni, Yanga ilitarajiwa kufunika katika mchezo huo.
Lakini badala yake ni wapenzi wa Simba waliofurika katika uwanja huo jana waliokuwa na furaha kwa muda mwingi wa mchezo kutokana na timu yao inayofundishwa na Zdravko Logarusic kuonana vizuri kwa pasi fupi fupi ikifanya mashambulizi mengi ya hatari.
Goli la 'kuchafua kurasa za magazeti' la Yanga kwenye Uwanja wa Taifa lilifungwa na mchezaji wa zamani wa Simba Emmanuel Okwi aliyekuwa akiichezea timu yake mpya hiyo kwa mara ya kwanza tangu atue nchini Alhamisi.
Hata hivyo ni mashabiki wachache wa Yanga waliokuwa wamebaki uwanjani kulishuhudia bao hilo baada ya wengi wao kuwa walianza kuondoka uwanjani robo saa kabla ya mpira kumalizika.
Mbali na magoli hayo, ushindi wa Simba ungeweza kuwa mkubwa zaidi kama isingepoteza nafasi nyingi nzuri za kufunga, ikiwemo shuti la Ramadhani Singano lililogonga mwamba baada ya saa ya mchezo.
Tambwe alifunga bao lake la kwanza muda mfupi kabla ya robo saa ya mchezo, alipotuliza mpira wa krosi wa juu kutoka kwa Juma kwa mguu wa kulia, kabla ya kupiga shuti lililokwenda wavuni kupitia pembeni kabisa mwa goli la Kaseja upande wa kushoto.
Mrundi Tambwe ambaye katika magoli yake 10 ambayo yanamfanya kuwa mfungaji anayeongoza kwenye ligi kuu ya Bara manne ni ya penalti, aliipatia Simba bao la pili kwa tuta dakika moja kabla ya mapumziko.
Mwamuzi Ramadhani Ibada kutoka Zanzibar alitoa penalti hiyo baada ya beki namba tatu wa Yanga Joseph Luhende kumkwatua Singano ndani ya eneo la hatari, akiwa anamsogelea zaidi Kaseja langoni.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid, Joseph Owino, Donald Msogoti, Thomas Mkude, Haruna Chanongo, Henry Joseph (Ramadhani Chombo dk.35), Amisi Tambwe (Amri Kiemba dk.58), Said Hamisi (Ramadhani Singano dk.27), Awadh Juma (Zahoro Pazi dk.73).
YANGA: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Joseph Luhende, Nadir Haroub (Juma Abdul dk.53), Kelvin Yondani, Athumani Iddi (Simon Msuva dk.45), Haruna Niyonzima, Frank Damayo, Didier Kavumbagu (Emmanuel Okwi dk.45), Mrisho Ngasa (Jerry Tegete dk.70), Hamisi Kiiza (Hamisi Dilunga dk.45).
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment