ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 29, 2013

Kuboronga Operesheni tokomeza, serikali nzima ing’oke

Na Mboneko Munyaga, Dar es Salaam, December 29, 2013
Kilichofanyika katika “Operesheni Tokemeza” ni mambo ambayo watu hawawezi kufanyiwa hata kama nchi ikivamiwa na majeshi ya maadui. Jeshi letu la ulinzi lina historia ndefu ya kupigana vita mbali mbali, ikiwemo hii ya majuzi kuwatokemeza M23 mashariki mwa DR Congo, kwa nidhamu ya hali ya juu. Sasa huu ukatili na watu kuuawa kinyama walikofanyiwa Watanzania na baadhi ya askari kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu umetoka wapi?
Niseme mapema tu kabla ya kutoa hoja zangu kwamba kwa yale yaliyotokea katika Operesheni Tokomeza Ujangili, serikali nzima na siyo mawaziri wanne tu, ilipaswa kuwajibika. Pili operesheni haikufanikiwa katika malengo yake, yaani kutokomeza majangili na kuokoa tembo na wanyama wengine ambao ni urithi wa kipekee unaopatikana katika nchi yetu.
Serikali nzima ilipaswa kuwajibika kwa nini? Naamini uamuzi kama huo haukuzuka tu hivi hivi nchini mwetu. Lazima ni jambo lililotolewa uamuzi katika ngazi ya Baraza la Mawaziri. Kwa hiyo ni jambo la umauzi wa pamoja na ambalo lilikuwa na Baraka za mawaziri wote, akiwemo Waziri Mkuu. Sasa, katika hao wote, hakuna aliyetoa angalizo ni jinsi gani zoezi lifanyike na kamandi yake iwe wapi na kwa nani.

Matokeo yake, kilichofanyika, ni sawa na nchi kuvamiwa na majeshi ya adui serikali nzima ikiwa imelela usingizi. Haiwezekani “majeshi’ yaingie vijijini watu wateswe na kuuawa huku kamati za ulinzi na usalama za vijiji, wilaya na mikoa hazina habari. Ndio maana nasema, aliyelala usingizi mkubwa kabisa hapa ni Waziri Mkuu. Kimsingi, hata Rais anaguswa lakini Mwalimu Julius Nyerere alitufundisha kuwa na tahadhari sana tunapotaka kuitikisa taasisi ya urais.
Kwa mantiki na uzito wa wosia huo wa Baba wa Taifa, nami sintamgusa Rais lakini wananchi tutamtaka Rais katika hili, atufanyie kazi ya kueleweka. Haiwezekani tukawa taifa lisilopata mafunzo ya kudumu kutokana na uzoefu utokanao na makosa ya nyuma. Siyo jambo geni kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuboronga katika aina ya “operesheni tokomeza.”
Rais wa Awamu ya Pili, Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi na mawaziri wenzake wakati huo, walipata kujiuzulu katika miaka ya 1970 kutokana na watendaji kuua watu katika operesheni ya kusaka wauaji wa vikongwe katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga waliokuwa wakidhaniwa wachawi.  Operesheni hiyo hakuna aliyeijua sana na kwa kweli pengine mambo yangeweza kwenda kimya kimya tu na watu wasijue kilichotokea.
Lakini kwa kuwa Mwalimu alikuwa kiongozi mwadilifu, yeye mwenyewe ndiye aliyelijuza taifa kilichotokea. Kama sikosei na niko radhi kukosolewa, hakukuwa na tume ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mauaji hayo ya watuhumiwa wa mauaji ya vikongwe. Wala hapakuwa na kikao maalum cha Bunge kilichotengwa kwa siku nzima kujadili taarifa ya Tume Maalum ya Bunge. Si nia yangu kurejea kilichotokea huko nyuma lakini ninachosema ni kwamba hilo pekee yake lingetosha kuwa fundisho la kudumu kwa viongozi katika serikali yetu.
Kwa mantiki hiyo basi, tumwombe Rais kutufanyia jambo linaloeleweka, siyo kuendelea na hii ngoma ya kitoto isiyokesha. Binafsi, namwomba Rais avunje Baraza la Mawaziri lote. Baadhi ya mawaziri wanaweza kurejea katika baraza jipya lakini isiwemo sura ya “Mtoto wa Mkulima”, mawaziri mizigo na watatu katika hao wanne waliojiuzulu. Kweli ni gharama kubwa kutunza Waziri Mkuu mstaafu na hasa ikitiliwa maanani kwamba tunao mawaziri wakuu wastaafu lukuki. Lakini ieleweke hiyo ndiyo gharama ya demokrasia.
Nashindwa kuelewa mantiki ya Dk Mathayo David Mathayo naye kuhusishwa katika “menzi ga nyanza” ya kuboronga katika Opereseheni Tokomeza.  Kosa la Dk Mathayo inasemekana ni yeye akiwa Waziri mwenye dhamana ya kuangalia kitoweo, alishindwa kudhibiti wafugaji kutoingia katika Hifadhi za Wanyama Pori. Nimetembelea mbuga zetu mara nyingi na sijawahi kuona ardhini mpaka wa mbuga hizo unapoanzia na kuishia. Lakini pamoja na hayo, wafugaji wa “Dk Mathayo” ndio waliouawa na waziri amewajibishwa!
Yaani mtu aue watoto wako kwa sababu wamekwenda kwa jirani wakachezacheza uani halafu baba ndiye uadhibiwe kwa “kutolea watoto wako vizuri!.” Hainiingii akilini. Kama ni hivyo, mzazi wa mtoto anayegongwa na gari ndiye angeadhibiwa kwa kutomfundisha mwanae kutembea vizuri barabarani au waziri wa uchukuzi naye angewajibika kwa madereva kugongagonga watu hovyo barabarani!
Dhana kuu hapa siyo “kuwajibika kisiasa.” Kuwajibika kisiasa ni sawa na kufunika pazia. Dhana kuu hapa ni kuchukizwa na kilichotokea. Kama wote tumechukia, haitakuwa mzigo kwa baraza la mawaziri kujiswaga lenyewe mtoni. Kwa kufanya hivyo, naamini tutakuwa tumejenga taifa la viongozi wawajibakaji na watenda kazi wa kweli.
Machungu waliyopata watu walioumizwa na kupewa ulemavu wa kudumu na damu ya waliokufa katika operesheni hiyo ndiyo iwe gharama halisi ya somo la uwajibikaji na utawala bora katika nchi yetu. Kujiuluzulu mawaziri ni muhimu lakini haitoshi. Serikali nzima iende na maji.

1 comment:

Anonymous said...

Rais Kikwete na Wakuu wa mikoa wote..walitakiwa kung'oka..yeye Rais ndiye aliyekuwa mtu wakwanza kutangaza hii vita ya wenyewe kwa wenyewe akiwa mkoani KAGERA..hivyo kama yeye ndiye aliyewaagiza wakuu wa mikoa ambao wote niwatumishi wa CCM,basi walitakiwa wote waondoke.Sioni kwanini bado watanzania mna mawazo yakusema kwamba huwezi kumzungumzia Rais wanchi wakati unajua kabisa hapa kaboronga.....wakuu wa mikoa nilazima wachaguliwe na wananchi sambamba na uchaguzi wa Rais na wabunge.huyu aliyesema kwamba hawezi kumzungumzia Rais kikwete hafai hata kuwa Diwani wa kata ya changanyikeni....zungumza ukweli pake unapoona kuna uzembe fulani.Waziri mkuu huyo tunajua kuwa yupo tu kwasababu ya Rais,hivyo hawezi kung'oka mpaka yeye Rais kikwete aobdoke....pia next election jamani tujaribu kumchagua Rais asiyependa kupanda ndege kila wakati kama vile anakwenda chalinze....safari za nje ya nchi nighalama..Rais kikwete ndiye kiongozi pekee Africa na duniani kote anayekuja Marekani kama vile hapa ni kariakoo..Asante saana Vijimambo.