ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 20, 2013

MAMBO MADOGO YENYE THAMANI KUBWA KWENYE MAPENZI!-2

KUJUA na kutambua thamani ya mapenzi kutakufanya ufurahie katika sayari hiyo. Baadhi ya watu hawapati muda wa kufikiri japo kidogo tu kuhusu kuboresha ndoa au uhusiano wao.

Hapa katika All About Love ndiyo mahali sahihi ambapo utapata kujifunza na kutambua mambo muhimu kuhusu maisha ya mapenzi.

Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza mambo machache ambayo yanaweza kuonekana madogo lakini yenye thamani kubwa sana katika mapenzi. Leo tunakwenda kumalizia sehemu ya mwisho nikiwa na imani kuwa yatakuwa nguzo kwako na kupalilia uhusiano wako.

Ni vyema kuweka wazi kuwa, mada hii hasa inawahusu wanaume ambao mara nyingi wameonekana kuwa kama wako bize zaidi na maisha na kuwasahau wenzi wao. Ndugu zangu, wanawake zetu wanatuhitaji sana.
Wanapenda kuona tukiwapa nafasi ya kwanza kwa kila kitu katika maisha yao. Inawezekana kuna ugumu kutokana na changamoto mbalimbali lakini mambo haya ninayoainisha hapa ni madogo lakini yana nguvu kubwa sana. Hebu twende tukaone.

UJUMBE WA MAHABA
Kumtumia mpenzi wako au mkeo ujumbe wa mahaba ni sehemu ya kumwongezea ‘uchizi’ katika penzi lenu. Wengi hawapendi na pengine hawawezi kutunga. Siku hizi mambo ni rahisi sana, magazeti mengi yanaandika Love Messages.
Achana na magazeti hata baadhi ya kampuni za simu hufanya hivyo. Kopi kisha pesti mtumie. Utaona atakavyozidi kukupaisha kithamani katika maisha yake.

MITANDAO YA KIJAMII
Siku hizi kuna mitandao mingi ya kijamii. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu huitumia vibaya na kuanzisha uhusiano usiofaa huko. Wanawake wengi huwa hawana amani na wanaume zao hata kama kwenye maelezo yao ya utambulisho wameandika wameoa au wana wachumba.
Kuweka picha yake mara chache au maneno ya kuonyesha unavyompenda, huziba hisia zake mbaya na kujiona yuko na mwanaume huru na makini. Jaribu utaona ukweli wa ninachokisema.

KUWA HURU NAYE
Wanaume wengi hawapendi mahaba, lakini asikudanganye mtu, kuongozana na mwenzi wako, huongeza msisimko na kumfanya azidi kuwa huru na mwenye kujiamini. Usimwogope, mshike mkono, tembeeni huku mnazungumza.
Kichwani hujiona mwanamke kamili, aliye na mwanaume asiye na ‘vimeo’ mitaani. Haya ni machache kati ya mengi ambayo kwa hakika hustawisha penzi.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; Let’s Talk About Love, True Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: