Dodoma.Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alipigilia msumari sakata la wabunge kuchukua posho bila kuzifanyia kazi stahiki kwa kuwaamuru wazirudishe.
Spika alitoa kauli hiyo jana asubuhi wakati akitoa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde akitaka ufafanuzi wa hatua ya Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Erasto Zambi kutumia Bunge kujitetea kuhusu tuhuma za kuchukua posho za safari bila kusafiri.
Alisema Zambi ni mbunge ,pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya na Kamishna wa Bunge anayefahamu taratibu za safari zinazoeleza kuwa kuchukua fedha bila kwenda safari ni makosa.
Silinde wakati akiomba mwongozo huo alimtuhumu Zambi kuwa alichukua kiasi cha Sh13 milioni za posho ya safari ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na nyingine kwa ajili ya safari ya shughuli za michezo lakini hakusafiri.
“Mtu anapozungumza kwa kutumia Bunge lako kujitetea kwa kukiuka taratibu, inaruhusiwa?” alihoji Silinde, ambaye pia ni Waziri kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.
Kabla ya Silinde kusimama na kuomba mwongozo, Zambi alikuwa amepewa fursa na Spika ya kuchangia taarifa za Kamati za Bunge za Nishati na Madini na Miundombinu zilizowasilishwa juzi.
“Jana (juzi) kulitokea maneno maneno fulani hapa bungeni. Alisimama ndugu Silinde akasema Zambi kala hela hakusafiri,” alisema lakini kabla hajamalizia kuzungumza Spika alimkatiza... “Naomba hilo uliache unapoteza muda na haliwasaidii wananchi, changia mambo mengine muhimu,” alisema Spika Makinda huku wabunge wengi ndani ya Ukumbi wa Bunge wakipiga makofi.
Hata hivyo, Zambi aliendelea kusisitiza kuwa taswira inayokwenda kwa wananchi ni mbaya na wameanza kumpigia simu kuwa ameiba fedha na kusema hilo ni jambo baya analostahili kulisemea.
Alisema utaratibu uko wazi kama hujasafiri unarudisha fedha na kusema... “Ningekuwa kiongozi wa ajabu sana kama ningekwenda Dubai na Uingereza na kutokwenda ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutoka chama kinachotawala.”
Baada ya kueleza hayo, Spika alisimama na kusema: “Waheshimiwa wabunge nimesema kama mlichukua pesa bila safari, mnarudisha si basi…. Wote kabisa ninawajua na ninalifanyia kazi. Wote waliochukua pesa warudishe ndiyo utaratibu wa Serikali na ndivyo inavyotakiwa. Wote watarudisha.”
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao aliwataka wabunge kutumia kikao cha kupeana taarifa cha wabunge wote kuzungumza kama kuna tatizo lolote badala ya kuumbuana ndani ya Bunge.
Moto wa posho hizo ulikolea juzi pale Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba alipoomba mwongozo wa Spika akitaka kujua hatua ya mbunge aliyechukua fedha na kwenda safari binafsi. Nchemba alisoma ujumbe wa simu uliokuwa ukionyesha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe alikatisha safari ya Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Joyce Mukya.
Nchemba alisema ingawa hayo ni mambo binafsi, lakini alitaka kufahamu Ofisi ya Spika inasemaje kwa mbunge aliyetumwa kuwakilisha Taifa halafu mtu binafsi kwa kutumia nafasi yake akamrudisha.
Kauli hiyo ilimfanya Silinde kusimama na kusema suala hilo linataka kuchukuliwa kama propaganda za kisiasa wakati wapo pia wabunge wa CCM waliochukua fedha bila kusafiri na kumtaja Zambi.
Wadau wawaponda wabunge
Watu wa kada mbalimbali wamewashutumu wabunge na kuwatuhumu kuwa wanashindwa kuisimamia Serikali kwa kuendekeza mambo ya posho.
Chama cha Walimu (CWT), wanasiasa, wasomi na wanaharakati hao walisema jana kwamba wabunge hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kujiwajibisha wenyewe au kuwajibishwa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema: “Wabunge wanapotengewa fedha kwa ajili ya kufanya shughuli fulani na kisha kuzitumia kwa shughuli nyingine maana yake ni kulipeleka taifa katika umaskini.”
“Kama wanafanya hivyo, msisitizo mkubwa unatakiwa kuwekwa wakati wakifanya marejesho ya fedha walizotumia. Wanaohakiki matumizi ya fedha hizo wanatakiwa kuwa wakali na kama itabainika kuna fedha zimetumika ndivyo sivyo hatua kali zichukuliwe,” alisema Ngowi.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema: “Tatizo lipo kwa wananchi maana hawajui fedha wanazopewa wabunge kama posho ni kodi yao. Kitendo cha wabunge kutafuna fedha za posho katika shughuli zao binafsi maana yake ni kwamba hawawezi kuisimamia Serikali katika suala zima la matumizi ya fedha.”
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda alisema: “Bila kujali ni mbunge kutoka chama gani, kama akibainika kuwa alitumia fedha za posho kwa ajili ya mambo yake binafsi, hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake kwani matumizi mabaya ya fedha ni sawa na wizi mwingine.” Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema ili kuhakikisha kuwa fedha za walipakodi zinatumika ipasavyo, inatakiwa kuundwa asasi ambayo itakuwa ikipanga na kusimamia mishahara na posho za viongozi na wabunge.
“Kenya wameweza kulinda matumizi ya fedha baada ya kubadili katiba yao na kuweka kipengele kinachoeleza kuwa mishahara na posho za wabunge na viongozi wa Serikali zitasimamiwa na asasi. Tunatakiwa kujua posho na mishahara ya wabunge ni kiasi gani. Katika hali ya kawaida kabisa mbunge akitafuna posho ni vigumu kuweza kuisimamia Serikali.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema tatizo lililopo ni Bunge kushindwa kusimamia ipasavyo kanuni zake za nidhamu.
“Kama Bunge lingekuwa linawachukulia hatua wabunge kulingana na kanuni zake, sidhani kama hali hii ingetokea, wabunge wanaofanya vitendo vya aina hii ni sawa na mafisadi wengine,” alisema Dk Bana.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema: “Wanatakiwa kuwajibishwa au wajiwajibishe wenyewe kama itabainika wamefanya vitendo hivi. Wabunge wanatakiwa kuwa waadilifu, sasa wanapoanza kukiuka misingi ya uadilifu ni janga kubwa.”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment