Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi Nchini, Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema nao wametakiwa kujiuzulu kutokana na uozo uliobainika katika ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyosababisha Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katibu wa madiwani wa jiji hilo, Julian Bujugo alisema wakuu hao wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa wao ndio wanaotoa amri kwa askari wao na siyo mawaziri.
“Nao wanatakiwa kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kama hatua ya kuonyesha uwajibikaji wao, askari wao wamefanya maovu makubwa,” alisema. Alisema kama wakuu hao wa watakaidi agizo la madiwani watalipeleka suala hilo kwa Rais Kikwete.
“Watendaji wa Serikali ndio chanzo cha uonevu, hata mawaziri ‘mizigo’, nao wanatakiwa kujiuzulu. Alimtolea mfano Waziri wa Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Bujugo alisema ameshindwa kuwasimamia wakulima na kusababisha mvutano na vurugu katika Sekta ya Kilimo.
Chiza alitajwa kama waziri ‘mzigo’ na Kamati Kuu ya CCM iliyokutana wiki mbili zilizopita chini ya uenyekiti wa rais Kikwete.
Bujugo ambaye ni diwani wa Kata ya Magomeni alisema mbali na wakuu hao wa ulinzi na usalama, pia wakuu wote wa wilaya waliohusika kusimamia operesheni hiyo nao wanapaswa kuwajibika kwa kuwa walijua na waliona wazi vitendo vichafu walivyofanyiwa wananchi lakini walikaa kimya.
Ripoti ya tume ya kuchunguza Operesheni Tokomeza Ujangili ilisomwa bungeni mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembelii na kuwango’a mawaziri hao.
Waliong’olewa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa njia panda kutokana na wabunge kuendesha mpango wa chini chini wa kupiga kura ya kutokuwa na Imani naye kwa maelezo kuwa ameshindwa kuwasimamia mawaziri wake.
Chanzo Mwananchi
2 comments:
Mimi sidhani kama kuna haja ya sisi voters kutaka vyombo vya ulinzi na usalama navyo viwajibishwe. Jukumu la kuviajibisha vyombo vya ulinzi na usalama ni la watunga sera na wasimamizi wa sera za serikali. Kama hao watunga sera na wasimamizi wa sera za serikali hawakuuona huo uozo, basi ni wazembe na hawatufai. Na kuwajibishwa kwao ni halali.
Kama tukizidi kwenda chini tukifuata chain of command, tutafika pahala tutataka hata wale police inspectors, army lieutenants and junior police/army officers wengine waliokuwa wakisimamia field operations nao wawajibike. That's none of our business. As voters, we deal only with those we trusted to govern.
Nakubaliana na mdau wa hapo juu. Kuwatimua viongozi wa Ulinzi na Usalama kutaleta misukosuko ambayo Taifa letu halipo tayari kuikabili. Tunao Wanajeshi wengi ambao tumewapeleka DRC na South Sudan ambao wanataka mwongozo mwema, hivyo siyo jambo la busara kumtimua mkuu wa Jeshi. Usalama wa Taifa dhidi ya majangili nao ni muhimu, hivyo kumtoa mkuu wa polisi siyo busara. Jamani, wanasiasa waache kupiga kelele kila saa, waache viongozi wa ulinzi na usalama pekee. Ni jambo la busara, for our country's PEACE and STABILITY.
Post a Comment