ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 13, 2014

Mkulo, Mwenyekiti watunishiana misuli

  Wavaana mbele ya mawaziri, wabunge
  Ni mbio za ubunge Kilosa mwaka 2015
Mustafa Mkulo

Joto la Uchaguzi katika Jimbo la Kilosa, limeanza kupanda kwa kasi kubwa, baada ya Mbunge wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Mkulo, kutunishiana misuli na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa, Amer Mubarak, mbele ya viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Morogoro.

Mbarak ambaye ni Diwani wa Kata ya Kimamba wilayani humo na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo licha ya kutotangaza hadharani nia ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini inadaiwa kuwa anakusudia kugombea jimbo hilo kwa tiketi ya CCM ambalo kwa sasa linaongozwa na Mkulo, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2012.

Mahasimu hao walitunishiana misuli hiyo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejementi ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, na viongozi wengine wakiwamo Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, pamoja na na wabunge, wakuu wa wilaya zote za mkoa na wenyeviti wa halmashauri.

Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho, Waziri Kombani ambaye pia ni Mbunge wa Ulanga Mashariki (CCM) alilazimika kutumia busara kuwatuliza Mkulo na Mubarak kuacha kutumia muda mwingi kutupiana maneno yasiyo kuwa na manufaa katika kikao hicho.

Kuibuka kwa malumbano hayo kulitokana na Waziri Kombani kutaka kupata maelezo kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhusiana na kutokamilika kwa barabara ya kiwango cha lami kutoka Dumila hadi Mikumi kupitia Kilosa ambayo ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete katika ilani ya uchaguzi ya CCM.

Waziri Kombani alisema kwa sasa barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami katika mji wa Rudewa ambayo sawa na kilometa 45 tu wakati inapaswa kumaliziwa hadi Mikumi ambayo ni zaidi ya kilometa 90.

Akijibu hoja hiyo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Doroth Mtenga, alisema walipokea fedha za ujenzi wa awamu ya kwanza kutoka mjini wa Dumila hadi Rudewa na kwamba kipande cha kumalizia kutoka Rudewa hadi Mikumi kimetengewa awamu ya pili huku upembuzi wa awali ukiwa umekamilika.

Baada ya maelezo hayo ndipo aliposimama Mkulo na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mradi huo kusuasua akisema ni kutokana na ukosefu wa fedha na kwamba zitakapopatikana utaendelea.

Kufuatia kauli ya Mkulo, Mubarak naye alisimama kuchangia hoja hiyo huku akimtaka Mkulo kuacha kuendeleza mjadala huo katika kikao hicho na kwamba alipaswa kulizungumzia suala hilo bungeni akiwa na Waziri wa Ujenzi na kwamba hapo siyo mahali pake.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Mbunge (Mkulo) anatupotezea muda tu hapa, suala hili ameshindwa kuliongelea bungeni akiwa na Waziri wa Ujenzi, anaongelea hapa, atuachie sisi wenyeviti wa halmashauri tuzungumzie suala hilo,” alisema Mbarak.
Maneno ya Mubarak yalionekana kumuudhi Mkulo na kulazimika kusimama tena na kutoa maneno makali dhidi ya Mwenyekiti huyo.

Mkulo alisema Mubarak hajui kanuni na wajumbe wanaopaswa kuhudhuria vikao vya bodi ya barabara na kumtaka kusoma hizo kanuni hususani zinazoainisha washiriki na sio kuropoka.

Mkulo alisema kwa sasa yeye ndiye Mbunge wa Jimbo la Kilosa mpaka 2015, hivyo ana haki ya kuizungumzia barabara hiyo kwa kuwa alishiriki kwa karibu kutafuta fedha zake akiwa Waziri wa Fedha huku akisisitiza kuwa kama kuna mwanaume anataka kugombea jimbo hilo asubiri mpaka wakati wa uchaguzi ili wapambane.

Alisema kuna mamluki (ambao hakuwataja) kuwa tayari wananyemelea jimbo hilo na wataka kukwamisha mradi huo wa barabara kwa lengo la kujinufaisha kisiasa, lakini alisema hawataweza kufanikiwa kwa kuwa barabara hiyo itamalizika kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake wa uongozi.

MWENYEKITI CCM AWATULIZA
Hata hivyo, malumbano hayo yalizimwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogerezi, ambaye aliwataka Mkulo na Mubarak kumaliza matatizo yao huko huko wilayani kwao na siyo kulumbana katika kikao hicho.

Kalogerezi alisema ni vema viongozi wa kila wilaya akiwemo Mbunge na Mwenyekiti kumaliza mambo yao katika mikutano ya vikao vya kamati ya ushauri vya wilaya zao.
NIPASHE lilipomuuliza Mubarak kama ana nia ya kugombea ubunge wa Kilosa mwakani, alisema kuwa Mkulo anaogopa kivuli chake.

Alisema ukifika wakati mwafaka atazungumzia suala la kugombea kwa sababu ni haki yake kikatiba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: