Ndugu zangu watanzania. Kwa niaba ya Familia yetu ya Buzohera napenda kutanguliza shukurani za dhati kwenu ninyi ndugu zangu kwa moyo, mali na hali mlizotuonyesha kwenye kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wetu ,mtoto wetu, dada yetu,rafiki yetu, Zainabu Haroun Buzohera.
Familia yetu imekuwa na kipindi kigumu sana kwa Msiba huu wa mtoto wa kwanza wa familia ya Bi.Rehema na Mzee Haroun Buzohera. Familia yetu ilipata habari za msiba huu kwa mshituko mkubwa sana lakini kwa ushirikiano wenu tunafarijika .
Dada, Mtoto, rafiki wetu Zainab ameacha Mume ( Dullah) na Wadogo zake watatu , Ngalu , Gwiyama na Halima Buzohera. Pia ameacha Mama yake mzazi Bi. Rehema na Baba yake mzazi Mzee Haroun Buzohera. Marehemu alikuwa ni kipenzi katika familia yetu na alikuwa ni mtoto ambaye mwenye upendo na heshima kwa wazazi wake ndugu jamaa na marafiki. Zainabu alikuwa mwenye furaha siku zote na mwenye ushirikiano na watu na mpenda watu . Kwenye Familia yetu alikuwa ni mfano wa kuigwa na wadogo zake haswa kwenye kupendana na kukamilisha malengo yao kimaisha, upendo na ushirikiano kwa jamii ya watanzania na wengine wengi, hakika pengo aliloacha halitoweza kuzibika.
Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru watanzania wote mnaoishi Marekani kutoka State mbali mbali zikiwemo DMV, NY, NJ, NC, DE, MA,TX na nk, Moyo mliotuonyesha katika kipindi hiki kigumu ni wa pekee. Michango yenu ya Hali na mali imetutia sisi moyo mkubwa na kutupa faraja sana sisi wana familia. Ushirikiano wenu mliouonyesha kwenye kukamilisha usafirishaji wa Mwili ni mfano wa wazi na unaonesha jinsi ndugu yetu alivyoishi na ninyi kiupendo. Na inadhihirisha ni jinsi gani mlivyo kuwa na upendo na mpendwa wetu. Mwenyezi Mungu awazidishie nyote na familia zenu. Na tunawaomba muendeleze upendo wenu kama watanzania.
Pia Familia inapenda kuushukuru Uongozi wa Jumiya ya Watanzania wa DMV kwa kusimamia na kushughulikia msiba na kusimamia kamati ya mazishi. Pia tunapenda kuishukuru kamati nzima ya mazishi iliyo ongozwa na Kaka Iddi Sandaly. Na vilevile tunapenda kuushukuru ubalozi wa Tanzania nchini Marekani kwa ushirikiano wao na kusaidia kwenye kusafirisha Mwili wa Marehemu.
Familia inapenda pia kuwashukuru watanzania wote wanaoishi Tanzania na walio nchi mbali mbali kwa michango yao ya hali na mali mlioionyesha. Kwa kweli tunawashukuru sana.
Tunawaomba tumkumbuke kwa Dua na Mwenyezi Mungu awazidishie.
Asanteni Sana.
Familia Ya Buzohera.
No comments:
Post a Comment