.Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangala
Mwanafunzi huyo jina limehifadhiwa, ambaye ni mkazi wa mjini Shinyanga inadaiwa awali alikuwa anaishi na Askofu huyo nyumbani kwake.
Muda wa masomo ulipokaribia aliondoka na Askofu pamoja na watoto wake wawili kuelekea shuleni jijini Mwanza.
Walipofika Mwanza, alipangishiwa chumba katika nyumba ya kulala wageni na kisha kubakwa na Askofu huyo.
Akielezea tukio hilo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo alisema binti yake alibakwa Januari 17, mwaka huu, katika hoteli moja iliyopo jijini Mwanza wakati Askofu huyo akimsaidia kumpeleka shule wilayani Magu.
Alisema walipofika Mwanza, aliwapeleka kwanza watoto wake shule na kisha binti yake kumpangishia nyumba ya kulala wageni akidaiwa kesho ndiyo angeenda shule.
‘’Hapo awali mwanangu alikuwa anasumbuliwa na mapepo na ndipo nilipompeleka kwa Askofu huyo kuombewa na akapona. Baada ya hapo Askofu aliniomba mwanangu awe anakaa naye kwake pindi anapokuwa likizo kwa ajili ya kujisomea na wenzake, ambao ni watoto wake wawili wa kiume,” alisema mama mzazi wa mwanafunzi huyo.
Aliongeza: “Likizo ilipokwisha nilimfuata mwanangu aende shule. Nikampa kila kitu pamoja na nauli. Lakini Askofu alikataa akasema, mama binti yako nitaenda naye sababu na watoto wangu nawapeleka shule huko huko Mwanza. Nikamkubalia. Wakaenda naye kesho yake. Nikapigiwa simu na kaka yangu, ambaye yupo Magu kuwa mwanao anadai amebakwa na Askofu.”
Hata hivyo, mama huyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa kaka yake, ndipo alipochukua jukumu la kumrudisha nyumbani mjini Shinyanga kwa ajili ya kwenda kuchukua hati maalumu ya matibabu ya polisi (PF3) pamoja na vipimo hospital ili amfungulie kesi ya ubakaji Askofu huyo.
Naye Askofu alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo, alikanusha kuwa hakumbaka na kukikiri kuwa mtoto huyo alikuwa anaishi naye.
Alisema waliondoka pamoja kwenda Mwanza akiwa na watoto wake wawili na kwamba, alipofika Igoma, Mwanza, alimpandisha mtoto huyo kwenye gari zinazokwenda wilayani Magu, majira ya saa 12 jioni.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Fredliki Mlekwa, alisema vipimo havikuonyesha kuwa binti huyo amebakwa kutokana na kuwa zimeshapita saa 24, hivyo hana majibu juu ya kubakwa kwa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangala, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa bado anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Aidha, inadaiwa kuwa binti aliyebakwa na Askofu huyo kwa sasa yupo shuleni kimasomo wilayani Magu, huku kesi hiyo ikiendeshwa na mama yake mzazi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment