ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 26, 2014

FAT ah! TFF yateua Taifa Stars

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limerudi enzi zake lilipokuwa linaitwa Chama cha Soka (FAT) kwa kuteua kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ bila kumshirikisha Kocha Mkuu, Kim Poulsen.
Mfumo huo wa uteuzi ambao haupo katika nchi nyingine duniani unafananishwa na ule uliokuwa ukifanywa na FAT kwa miaka yote kabla ya kuvunjiliwa mbali miaka kumi iliyopita.
Mara ya mwisho, FAT iliteua kikosi cha Stars mwaka 2004, hata hivyo ulipoingia madarakani uongozi wa Leodegar Tenga uliacha jukumu la uteuzi wa wachezaji kwa kocha Marcio Maximo aliyekuwa ameajiriwa na Serikali.
Enzi hizo, kikosi cha Taifa Stars kilikuwa kinateuliwa na Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa FAT na wakati mwingine uteuzi huo ulikuwa ukipitishwa na kamati ya utendaji ya chama hicho cha soka.
TFF imefanya maajabu hayo ya zamani ya FAT baada ya jana kutangaza kikosi cha Stars ambacho kitacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia Machi 5 mjini Windhoek kabla ya kuingia kambini Machi Mosi ikiwa na kocha mpya anayetarajiwa kutangazwa leo au kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura alishikwa na  kigugumizi kuhusiana na jukumu la uteuzi wa timu hiyo bila  kumshirikisha kocha.
Alipoulizwa nani amechagua wachezaji hao na watakaa kambini wakiwa na kocha gani, Wambura alisisitiza kuwa wachezaji hao  wamechaguliwa na TFF.
“Timu hii imeteuliwa na TFF na siyo kocha, hiyo ndiyo taarifa rasmi, kusema nani ataifundisha, naomba muwe na subira, itajulikana ndani ya saa 48 (siku mbili),” alisema Wambura.
Kwa upande wake, Kim ambaye bado ana mkataba wa kuinoa Stars hadi Mei mwakani alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema hajui lolote na anayefaa kuulizwa ni TFF kupitia  Rais wake, Jamal Malinzi.
“Mimi sijui chochote kuhusiana suala hilo, naomba nisiwe mzungumzaji, muda ukifika nitasema, lakini kwa sasa muulize Rais wa TFF (Malinzi) atakuelezea kila kitu na kwa nini wamefanya hivyo,” alisema Kim kwa kifupi.
Katika kikosi hicho, TFF imewaacha  kipa mzoefu nchini, Juma Kaseja ambaye mwaka jana pia aliachwa na Kim katika kikosi cha timu ya  Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars iliyoshiriki michuano ya Chalenji nchini Kenya kwa kigezo kuwa hakuwa akishiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pia, wachezaji mahiri kama, John Bocco, Salum Abubakari na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ nao hawamo kikosini. 
Baada ya kuingia kambini Machi Mosi, kikosi hicho kitachujwa na kubakia wachezaji 20 watakaokwenda Namibia Machi 3.
“Wachezaji wanatakiwa kuripoti kambini saa moja kamili jioni na wale ambao watakuwa na mechi za ligi zinazochezwa Machi 2 watatakiwa kujiunga na wenzao saa chache baada ya mechi zao,” alisema Wambura.
MWANANCHI

No comments: