Dar es Salaam. Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete hatakubali kuidhinisha kama akipelekewa ombi la kuongeza kiinua mgongo cha wabunge kutoka Sh43 milioni hadi Sh160 milioni.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana kuwa Rais Kikwete hajapokea maombi hayo huku akipinga maelezo kuwa Serikali ilishayakubali.
Gazeti dada la The Citizen wiki iliyopita, lilimkariri Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akisema Serikali ilikuwa imepitisha kupandishwa kwa kiwango cha kiinua mgongo kutoka Sh43 milioni hadi Sh160 milioni baada ya kumaliza kipindi cha miaka mitano.
Waziri huyo alikaririwa akisema kuwa kiwango hicho kilipitishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na tayari wabunge walishaanza kuchukua fedha hiyo licha ya ukweli kuwa Bunge hili halijamaliza muda wake.
Hata hivyo, Rweyemamu alisema nao wamelisoma suala hilo kwenye magazeti na kwamba halijafika Ofisi ya Rais... “Suala hili halijafika Ofisi ya Rais hata kama litaletwa, `I really doubt if the President will endorse such matter’ (Nina shaka kama Rais ataidhinisha suala hili).”
Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi tayari imekanusha vikali taarifa za kupandishwa kiwango hicho cha malipo kwa wabunge.
Kashililah akanusha
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alikanusha kuwapo kwa mapendekezo ya wabunge kulipwa kiasi hicho cha fedha.
“Malipo ya wabunge yanalipwa kwa mujibu wa sheria kwa Kiingereza inaitwa Political Service Retirement Benefits Act (Sheria ya Malipo ya Utumishi kwa Viongozi wa Kisiasa) ni sheria namba 3 ya 1999, kwa hiyo hakuna malipo yoyote yanayoweza kufanyika nje ya sheria hiyo,” alisema Dk Kashililah na kuongeza:
“Sheria inaelekeza kila kitu, kwa kuzingatia uhalisi wa mishahara ya wabunge kwa sasa, malipo yao ya mwisho hayawezi kufikia kiasi cha Sh160 milioni, hata kama mishahara itaongezwa haitaweza kufikia kiwango ambacho kitamwezesha mbunge kulipwa kiasi hicho cha fedha.”
Katibu huyo wa Bunge alisema malipo ya kiinua mgongo kwa wabunge yanakokotolewa kutokana na kiwango chake cha mshahara tu na siyo malipo ya posho za kuendesha shughuli za kibunge.
Licha ya Dk Kashililah kukataa kutaja kiwango cha mshahara wa mbunge kwa mwezi, gazeti hili limebaini kuwa malipo hayo kwa sasa ni Sh3.4 milioni.
Mbali ya mshahara, wabunge pia hulipwa fedha nyingine kiasi cha Sh8.2 milioni kwa ajili posho ya jimbo, gharama za ofisi, mafuta, malipo ya wasaidizi wao na dereva.
Matakwa ya sheria
Sehemu ya tano ya Sheria ya Malipo ya Utumishi kwa Viongozi wa Kisiasa katika Kifugu cha 21 inasema mbunge atalipwa kiinua mgongo ambacho ni asilimia 40 ya mshahara ya kila mwezi katika kipindi chote cha utumishi wake.
Kadhalika, Kifungu 18 (3) Mbunge atalipwa malipo ya nyongeza yanayoitwa posho ya ukomo wa Bunge (winding up allowance) ambayo ni asilimia 20 ya jumla ya mishahara yake ya miezi 24 iliyopita.
Kwa tafsiri ya sheria hiyo na kwa kigezo cha mshahara wa Sh3.4 milioni, wabunge wa sasa watalipwa kiasi cha Sh97.92 milioni watakapomaliza uongozi wao mwishoni mwa mwaka ujao.
Malipo hayo ni Sh81 milioni ambayo ni asilimia 40 ya jumla ya mishahara ya miezi 60 ya utumishi wa wabunge hao na Sh16.32 ambazo asilimia 20 ya mishahara ya miezi 24 kwa ajili ya malipo ya posho ya ukomo wa ubunge.
Malipo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia zaidi ya 100 ya kiinua mgongo cha Sh43 milioni walicholipwa wabunge waliostaafu 2010.
Kabla ya kupandishwa kwa kiwango hicho kuwa Sh43 milioni mwaka 2010, kwa miaka kadhaa kiwango cha kiinua mgongo kwa wabunge kilikuwa Sh20 milioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment