ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 3, 2014

MAPENZI BILA NDOTO NI WIZI MTUPU -4

MADA hii ina maana kubwa sana. Nashukuru wengi wanaelewa ndiyo maana napokea simu na SMS nyingi. Hii inatoa muongozo wa mapenzi yenye raha na maelewano.

Inakuongoza kuwa na mpenzi wako anayekidhi vigezo vyako, siyo unakuwa naye kwa sababu ndiye umempata.

Turejee pale nilipouliza wiki iliyopita, kama ni mwanaume jiulize, mwanamke wako unampenda akiwa kijana kabisa, mrembo, tena msichana mbichi, je akishakuwa ndani ukimzoea itakuwaje? Akishazaa utaendelea kuwa na mapenzi juu yake?

Mapenzi yenye sura ya maisha hayabadiliki baada ya kuoana na kuishi pamoja ndani ya nyumba, kwa kisingizio cha kuzoeana. Mapenzi sahihi hayapungui baada ya kuzaa. Badala yake hukua na kuchanua kwa maana hatua hizo ni kutimia kwa ndoto.

Ukiona mwenzi wako amepunguza mapenzi kwa sababu mpo karibukaribu muda mwingi, huyo ana walakini. Jitambue kwamba hukuwa wa ndoto zake. Ndiyo maana nasisitiza utilie shaka kila kitu chake mpaka utakapojiridhisha.

WA NDOTO ZAKO LAZIMA MUENDANE
Ukifika hapa hebu weka kituo kidogo, vuta pumzi kisha waza ukiwa umefumba macho “wewe na mwenzi wako mnapiga hatua ipi katika maisha yenu? Maelewano yapoje? Heshima je? Na mnafanana kwa kiwango gani?”

Sina maana ya kufanana kwa sura, namaanisha kushabihiana kwa mambo yenu ya kila siku. Kama mara zote fikra zenu zinakuwa tofauti hapo kunakuwa na walakini mkubwa. Wapenzi wanaounganishwa na ndoto ni lazima waendane.

Haiwezekani wapenzi wakawa na imani mbili tofauti. Mmoja awe anapendelea na kumshawishi mwenzake kurudi nyumbani mapema lakini mwenzake yeye usiku anageuka popo, anakesha viwanja na anaowaita marafiki.

Hii ni kwa jinsia zote. Si mwanaume wala mwanamke anayeruhusiwa kuzurura usiku wa manane na kumwacha mwenzi wake akikumbatiana na mto. Hili ni kosa kubwa sana ambalo watu wengi wanalifanya. Sababu yake ni kukosekana kwa ndoto.

Mwanaume kukesha viwanja, kuzurura usiku bila sababu za msingi na kumwacha mkewe peke yake nyumbani, kwa tafsiri zetu ni unyanyasaji. Ikiwa mwanamke ndiye kiguu na njia, kwa tamaduni zetu huyo ni kicheche, kiruka njia.

Kama wewe ndiye mtembezi, maana yake ili uhusiano wenu uendelee inabidi uvumiliwe sana. Unapojikuta upo kwenye mazingira hayo, inakuhitaji upate elimu ya kujitambua ili uweze kuyashinda ‘mapepo’ yaliyokutawala.

Vilevile ni hasara kubwa kwako kushindwa kukamilisha ndoto hasa pale wewe unapokuwa tatizo. Inakushinda nini kujisahihisha? Unaposhindwa kubadilika, maana yake unamtesa mwenzio na unayafanya mapenzi kuwa magumu.

Kwako ambaye mwenzi wako humuelewi lakini unaendelea kumvumilia, jiulize, uvumilivu wako mpaka lini? Utakonda, utapoteza hamu ya kula, utaugua vidonda vya tumbo na msongo wa mawazo utakusababisha maradhi ya shinikizo la damu lakini hatabadilika.

Katika hili, asili ya binadamu wasiojitambua hujawa na kiburi pale wanapovumiliwa. Yaani, badala ya kuuona uvumilivu wa mwenzi wake kama tunu yenye thamani kubwa, yeye hujichukulia kama mtu maalum, hivyo kuzidisha mauzauza na vitimbi.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

Asante, muhariri!! Hicho kipengele cha mwisho umekiweka wazi kabisa. Kwani waswahili husema( mwenye kupendwa akijua haachi kujizuzua.lkn zeze likimkatia anabaki kulia na kujutia ha ha Kuwa na ndoto upendoni muhimu.KUTOKA KWA MTOTO,KCK,NYC..