ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 20, 2014

Mume na mke wazua balaa Bunge la Katiba

Zanzibar/Dar. Chama cha National League for Democracy (NLD) Zanzibar kimemtaka, Rais Jakaya Kikwete kufuta uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupitia chama hicho kwa madai kuwa walioteuliwa katika chama hicho ni mtu na mkewe na kufanya uteuzi huo kukosa sura ya Muungano.
Tamko hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa NLD - Zanzibar, Khamis Haji Mussa katika taarifa aliyoisambaza kwa vyombo vya habari mjini hapa juzi, kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Dk Emmanuel Makaidi amewasilisha majina mawili, la kwake na la mkewe, Modesta Ponera kwa ajili ya uteuzi.
Alisema NLD - Zanzibar kilianza kufuatilia taratibu za uwasilishaji wa barua tangu Desemba 27, mwaka jana kwa kumwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ baada ya kupokea maelekezo ya Ikulu ya Tanzania kwamba majina ya Zanzibar yatafanyiwa kazi visiwani na ya Bara yangepelekwa Ikulu Dar es Salaam.
Alisema kwa mujibu wa utaratibu huo, vyama vyote vyenye usajili wa kudumu vilitakiwa kila kimoja kutoa mtu mmoja kutoka Tanzania Bara na mwingine Zanzibar ili kuwa na sura ya kitaifa, lakini Dk Makaidi alikiuka utaratibu huo.
Makaidi ajitetea
Akizungumzia tuhuma hizo, Dk Makaidi alikiri kuwa Ponela ni mke wake, lakini akasema ni mwanachama wa NLD, hivyo ana haki ya kuteuliwa.
Alisema alipeleka majina manne Ikulu na kwamba upande wa Zanzibar ulitakiwa kufanya hivyo kupitia Ikulu ya Zanzibar... “Walifanya uzembe, hawakupeleka majina ya wanachama wa NLD, matokeo yake nikapeleka majina manne, tukapata uwakilishi.”
 Alisema mkewe ni mwanachama wa NLD hivyo ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi yoyote kulingana na sifa zake... “Wanalalamika nini hata chama tawala cha CCM, Rais Jakaya Kikwete ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na Mkewe Salma pia ni mjumbe wa Nec.”
Alisema Ponela kuwa mkewe hakumfanyi akose haki zake za msingi na kwamba sifa zake na elimu ndivyo vilivyomfanya Rais amteue.
Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Florens Turuka alipoulizwa alisema Ikulu haina taarifa za suala hilo lakini wanaamini vyama vya siasa vilikaa na kupendekeza majina manne na kuyawasilisha Ikulu, ndipo Rais alipoteua wajumbe mawili kati yake.
Mzimu wa posho walitesa Bunge la Katiba
Siku mbili baada ya kuanza kwa Bunge hilo, baadhi ya wajumbe wametaka waongewe posho kwa maelezo kuwa kiasi wanachopewa sasa cha Sh300,000 kwa siku hakiwatoshi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha Dodoma.
Wajumbe hao walitoa kauli hiyo jana katika kikao cha kuwasilisha na kujadili rasimu ya kanuni za Bunge hilo ambacho kilianza saa nne asubuhi.Kwa kiasi kikubwa, kikao hicho ambacho awali waandishi wa habari walizuiwa kuingia, kilitawaliwa na hoja ya kuongezwa kwa posho za wajumbe na kuungwa mkono na wajumbe wengi bila kufuata utaratibu maalumu uliokuwa ukisisitizwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho.
“Wajumbe wengi walikuwa wakisimama na kutaka kuzungumza bila kufuata utaratibu maalumu. Jambo hilo liligeuza ukumbi wa Bunge kuwa kama soko,” kilisema chanzo chetu. Baadhi ya wajumbe waliopata nafasi ya kuzungumzia nyongeza ya posho hizo ni Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi na Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa.
Katika ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari, baada ya kikao hicho kuahirishwa kwa muda, Ndassa alisema: “Bunge ndiyo linalotengeneza Katiba ya nchi. Nasikitika kuwa kiwango cha fedha ambacho tunalipwa ni kidogo na hakitoshi kwa sababu kuishi katika Mji wa Dodoma ni gharama kubwa.”
Ndassa alisema kati ya Sh300,000 wanazolipwa wajumbe hao, posho ya kikao ni Sh220, 000 na 80,000 ya kujikimu na kwamba kiasi hicho hakitoshi.
“Mfano ni siku ya Jumamosi na Jumapili. Katika siku hizo mbili wajumbe wote hawalipwi Sh220,000 za posho za kikao na wakati huohuo wanatakiwa kuwalipa madereva wao, kununua mafuta ya gari, chakula na malazi,” alisema.
Aidha, alisema kitendo cha wajumbe kutakiwa kulipwa Sh220, 000 baada ya kusaini katika kitabu cha mahudhurio mara mbili kwa siku ni sawa na udhalilishaji.
“Nilimweleza mheshimiwa mwenyekiti kwamba wajumbe tupo 600 na kulingana na hali halisi wote hatuwezi kuhudhuria kikao kila siku, zipo siku ambazo baadhi yetu wanakuwa na shughuli nyingine na wapo watakaougua, sasa na hao wasilipwe Sh220,000 kweli?” alihoji.
Alisema Serikali inatakiwa kulitazama suala hilo kwa kina kwa maelezo kuwa linaweza kuibua mvutano unaoweza kusababisha wajumbe hao kushindwa kuijadili Rasimu ya Katiba kama inavyotarajiwa na wengi.
“Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walikuwa wakilipwa Sh500,00 kwa siku, lakini wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanalipwa Sh220,000 tena mpaka wahudhurie kikao. Hii siyo sawa kabisa,” alisema.
Alisema madereva wa Tume hiyo ya Katiba walikuwa wakilipwa Sh220,000 kwa siku... “Posho yangu ni sawa na aliyokuwa akilipwa dereva wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sielewi kabisa maana hata viwango vyetu vya posho ni tofauti na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar, wao wameongezewa posho.”
Alisema jambo hilo litaibua ubaguzi kwa sababu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kuongezewa posho lakini wajumbe 201 walioteuliwa na Rais hawana mahali pa kulalamika ili kuongezewa posho.
Pamoja na Ndassa kutotaka kuweka wazi, kumekuwa na madai kuwa wajumbe kutoka Zanzibar wameongezewa Sh120,000 na Baraza la Wawakilishi, hivyo kuwafanya kupata Sh420,000 kwa siku.
Hata hivyo, Katibu wa Baraza hilo, Yahya Khamis Hamad alikana madai hayo akisema hakuna fedha za ziada walizolipwa.
Alisema malipo waliyosaini wakiwa Dodoma yaliyotokana na kuhudhuria vikao vya Kamati za Baraza, lakini si nyongeza ya posho.
Akizungumzia suala hilo Nchambi alisema: “Sisi tumeshazoea maisha ya Dodoma na tunaishi hivyohivyo tu licha ya kuwa fedha ni ndogo. Ila hawa wenzetu ambao ni wageni hali zao ni mbaya.
“Wajumbe wapo hapa kwa ajili ya kutengeneza moyo wa nchi yao na wakati tunakuja hapa Dodoma tulielezwa wazi kuwa tusiende kuishi katika nyumba za wageni za vichochoroni. Sasa kwa mantiki hiyo hiki kiwango cha fedha tunacholipwa kitatosha kweli?
“Hapa bungeni wapo maprofesa walioacha kazi zao zinazowaingizia fedha nyingi na kuja kuandika Katiba. Kitendo cha kuwalipa fedha kidogo kinaweza kuwakatisha tamaa.”
Kificho alihitimisha mjadala huo kwa kusema suala hilo la posho litawasilishwa serikalini kuona namna ya kulifanyia kazi.
Baada ya wabunge kutoka kwenye mjadala huo, Mjumbe, Kabwe Zitto alisema anasikitika kwamba tangu siku ya kwanza, suala la posho linashika kasi... “Kiukweli inavunja moyo sana… Ni dhahiri wajumbe lazima walipwe lakini malipo ya posho ndiyo kipaumbele kweli?”
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Raymond Kaminyoge Fidelis Butahe na Freddy Azzah wa Mwananchi

No comments: