Waziri wa Nchi, Ofisi Rais (Kazi Maaalum), Profesa Mark Mwandosya, amewahakikishia Watanzania kuwa kwa sasa afya yake imeimarika.
Profesa Mwandosya ameyasema hayo jana jijini Mbeya wakati akisalimia wananchi baada ya kumalizika kwa matembezi ya mshikamano ya kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete.
Mwandosya alishiriki matembezi hayo ya Kilometa tano pamoja na viongozi mbalimbali, wanachama CCM na wananchi kwa ujumla.
“Wale ambao mlikuwa mna wasiwasi kuhusu afya yangu, kwa sasa imeimarika, si mmeniona wenyewe naweza?” alihoji Mwanyosya huku umati wa watu ukilipuka kwa shangwe.
Mwandosya alishiriki matembezi hayo yaliyoanzia viwanja vya Soweto na kuishia katika bustani ya viwanja vya Sokoine na kudumu kwa saa moja.
Katika miaka ya hivi karibuni afya ya Mwandosya ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki ilidhoofika kutokana na kuugua na kupelekwa India kutibiwa.
Baada ya kumalizika kwa matembezi hayo, Rais Kikwete alisema: “Kwa kweli nimesikia furaha sana ambayo sijawahi kuipata katika matembezi niliyowahi kushiriki kutokana na wingi wenu na furaha yenye hamasa tele mliyonayo, naamini hamuwezi kurudi nyuma.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment