Inahitaji hekima za hali ya juu kusahau maudhi ya nje haraka, kwani wengi wamekuwa shubiri kwa wapenzi wao. Anaingia ndani, mwenzake anampokea kwa bashasha lakini badala ya kumpokea, anamsukuma! Kitu kidogo anafoka: “Usinitibue, kichwa changu hakipo sawa leo.”
Nimeeleza kuwa inahitaji mtu mwenye hekima ya kiwango cha juu kuweza kuepuka hasira za pembeni anapokuwa na mwenzi wake. Ni moyo wa kishujaa kweli, kwani wengi moto wa nje huuwasha ndani mpaka nyumba inashindwa kukalika.
Inawezekana kiwango cha uvumilivu ni kidogo, kwa hiyo ni ngumu kutenganisha maudhi kwa haraka, hivyo hapa chini kuna njia sita ambazo zinaweza kukusaidia kukabiliana na hali hiyo pale yanapokufika.
MUELEZE HUJISIKII VIZURI
Ikibidi sema unaumwa. Mpenzi bora atapunguza maswali au baadhi ya vitu na kukuacha upumzike. Hiyo itakusaidia kuingiza hewa kichwani ambayo itakuongezea nafasi na mwisho wa siku kichwa kitakuwa chepesi.
Maneno ya hapa na pale ukiwa na msongo wa vitu kichwani, utaona kama ni vuvuzela zinapuliza masikioni. Unapomuomba mwenzio akupe nafasi ya kupumzika kwa sababu hujisikii vizuri, itakusaidia kupunguza uzito wa kichwa.
ANGALIZO; Unapaswa kuwahi kujieleza kabla mwenzako hajaanza yake, kwa maana akisema yeye halafu wewe ndiye ufuate, atajua umeamua kumkwepa.
LALA USINGIZI
Tafuta usingizi kisha utokomee kwenye njozi, ukiamka hutokuwa yule yule. Angalau kichwa kitakuwa kimepumua na uzito umepungua.
EPUKA MAJADILIANO
Kama nilivyosema mwanzo, unapokuwa na vitu vingi kichwani halafu uendelee kuongeza vingine utaona ni sawa na vuvuzela zinapuliza masikioni. Hivyo basi, itakuwa nafuu kwako endapo utakataa majadiliano ya aina yoyote.
Kuepuka majadiliano, siyo tu kwamba kutaleta unafuu kichwani, bali pia kutakuepusha na migogoro ambayo unaweza kuingia kwa sababu ya msongo.
MUELEZE KINACHOKUSUMBUA
Ni tiba kwako endapo utafungua kinywa na kumueleza mwenzio kile ambacho kinakusumbua. Atajua kinachokusibu, kwa hiyo atajua jinsi ya kukuzoea kuliko kufika na kukaa kimya au kumjibu mkato au kufoka bila mpango.
CHAGUA KINACHOKUFURAHISHA, FANYA
Unapenda kuangalia filamu au kingine chochote na unaamini ukikifanya kitakuondolea hasira, basi fanya ili kujiweka vizuri kisaikolojia mbele ya mwenzi wako. Kuna wale ambao hasira zao hutoweka baada ya kupanda kitandani, nalo si tatizo ilimradi kutibu hasira.
Angalizo ni kwamba kupanda kitandani kunahitaji uhuru wa hisia. Utazungumza vipi na mwenzi wako mpaka mkubaliane kupeana hiyo dawa? Muhimu ni kumueleza kinachokusibu, akikuhurumia, basi huo ndiyo uwe mwanzo wa kutii kiu.
UVUMILIVU
Yote ni muhimu, lakini uvumilivu ni kitu cha msingi. Jifunze kusikiliza vitu bila kutoa majibu. Acha baadhi ya mambo yawe fahari ya masikio. Inawezekana umesikia na jibu unalo lakini unatakiwa uitambue hali uliyonayo, kwa hiyo endelea kunyamaza.
Ukiweza hili basi umefaulu mtihani mgumu na haitatokea ugombane na mwenzio kisa umeudhiwa na kazini kwako au kwenye daladala.
GPL
No comments:
Post a Comment