ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 4, 2014

WAJUE WATU 10 WENYE NGUVU TANZANIA

KWA muda wa miezi miwili , magazeti ya Global Publishers Ltd yaliendesha zoezi la kuwashirikisha wasomaji wake juu ya mtu gani mwenye nguvu zaidi ya ushawishi katika jamii ya Watanzania.
Rais Jakaya Kikwete.
Jumla ya Watanzania 438,726 walipiga kura kupendekeza majina mbalimbali. Watu 10 waling’ara zaidi kwa kugawana jumla ya kura asilimia 97.4, huku wengine ambao hawakuweza kuchomoza wakiambulia mgawo wa asilimia 2.6.
Katika hao 10 waliong’ara zaidi, mtiririko kulingana na wingi wa kura unagawanywa kama ifuatavyo.
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anashika nafasi ya kwanza. Kwa nafasi yake kama mkuu wa nchi, Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Chama Tawala CCM, ndiye aliyeongoza kwa kupata kura nyingi kwamba ana ushawishi mkubwa katika makundi yote. Watu 118,456 ambao ni sawa na asilimia 27 walimchagua.
Edward Ngoyai Lowassa
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa anashika nafasi ya pili kwa nguvu ya ushawishi katika Tanzania. Ingawa hayumo kwenye Baraza la Mawaziri, ameonesha anakubalika sana kijamii kwa kuchaguliwa na watu 83,358 ambao ni sawa na asilimia 19.

Zitto Zuberi Kabwe
Mbunge huyu wa Kigoma Kaskazini Chadema ndiye alifungua milango kwa vijana wengi kujiingiza katika siasa mwaka 2005. Umahiri wake katika kujenga hoja zinazotikisa nchi, zilimpatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya chama chake. Anachukuliwa kama kijana aliyewapa wenzake uwezo wa kujiamini. Pamoja na misukosuko ya kisiasa inayomkabili lakibi bado ameng’ara kwa kuchaguliwa na watu 65,809, sawa na aslimia 15.
Reginald Abraham Mengi
NI mfanyabiashara mkubwa mzawa, maarufu pengine kuliko wote Tanzania. Ndiye mtu anayemiliki vyombo vingi vya habari, vikiwemo televisheni, redio na magazeti. Ni mmoja wa matajiri wachache wenye utamaduni wa kuwasaidia wasiojiweza. Kutokana na mchango wake kijamii, naye ameng’ara. Watu 43,873 ambao ni sawa na asilimia 10 walimchagua.
Kadinali Polycarp Pengo
MUADHAMA Polycarp Kardinali Pengo ni kiongozi wa madhehebu ya Kikatoliki anayeheshimika katika jamii ya Kitanzania. Ni mtu makini na anayehubiri amani na upendo muda wote. Taswira yake kwenye jamii imemuwezesha kuchaguliwa na watu 35,098 (asilimia 8).
Dk. Willibroad Peter Slaa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Alijipatia umaarufu mkubwa wakati alipokuwa mbunge wa kuchaguliwa Jimbo la Karatu. Uwezo wake wa kujenga hoja na kuitetea, msimamo mkali dhidi ya rasilimali za taifa kulimfanya kupendwa na wengi.
Jambo hili lilimfanya kuwa mpinzani mkubwa wa CCM wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, ingawa baadaye alishindwa na Rais Kikwete. Mvuto wake kwa wananchi, ulichangia pia kuongezeka kwa idadi ya wabunge wa chama chake, kutoka 11 mwaka 2005 hadi 48. Watu 26,324 (6%) wamempigia kura.
Said Salim Bakhressa
MFANYABIASHARA maarufu nchini na mmoja wa watu wanaotajwa kuwa na fedha nyingi zaidi Tanzania. Anamiliki viwanda vya kutengeneza unga, juisi, matunda, biskuti, soda na koni. Pia ndiye msambazaji mkubwa wa unga kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Bakhressa ambaye ni Mzanzibari, pia anamiliki timu ya mpira wa miguu ya Azam FC ambayo ni ya kwanza nchini kuwa na uwanja wake wa kisasa. Ndiye mmiliki wa kituo cha televisheni cha Azam TV, vilevile ana vyombo vya usafiri wa majini. Watu 21,936 (5%) wamemchagua.
John Pombe Magufuri
MMOJA wa mawaziri wenye historia nzuri ya uchapa kazi kiasi cha kusifiwa sana na wananchi. Tokea alipoibuliwa kwa mara ya kwanza na kuwa waziri wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu, kasi yake imezidi kung’aa na kumfanya kuwa kipenzi cha wananchi. Katika orodha hii amechaguliwa na watu 17,549 (4%).
Dk. Harrison George Mwakyembe
Makali yake yalidhihirika zaidi alipoongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kuhusu uwepo wa ufisadi katika kampuni ya kufua umeme ya Richmond mwaka 2007-2008, kazi ambayo ilimalizika kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa kuachia ngazi pamoja na Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, waliokuwa mawaziri wakati huo.
Kazi yake nzuri akiwa mbunge, baadaye kuwa naibu waziri wa Uchukuzi na hata baada ya kuwa waziri kamili, imemfanya achaguliwe na watu 8,775 (2%) kuwa mmoja wale 10 wenye ushawishi.



Issa Ponda     
Ni Katibu wa Jumuiya za Kiislam Tanzania. Amekuwa akiendesha harakati nyingi kudai haki za Waislam, hivyo kumfanya awe akilumbana na serikali mara kwa mara. Anachokifanya kinabeba maana kubwa kwa watu, ndiyo maana amechaguliwa kwa kura 6,142 (1.4%), hivyo kufunga orodha ya wale 10 wenye mvuto zaidi Tanzania kwa mwaka 2013-2014.

5 comments:

Anonymous said...

HATUMTAKI, HII NI JANJA YA KUMUUZA HAUZIKI KWA WATANZANIA WENYE UCHU NA NCHI YAO AMETULIZA SANA NA KUTURUDISHA NYUMA MIAKA KUMI TUKIMPA SI TUMEKWISHA!!!

Anonymous said...

hizo takwimu hazisomeki kama kweli unaipenda nchi yako

Anonymous said...

HIYO SURVEY NI UPUUZI MTUPU NA HAINA VALIDITY. HOW DID YOU DO THE SAMPLING? KAMA MLI-SAMPLE WATU WA KILIMANJARO NA ARUSHA REGIONS, THEN MOST LIKELY YOUR DATA IS CORRECT MAANA CHADEMA NDO WAMEJAA HUKO, AND THE CHAGA PEOPLE ARE MORE THAN HAPPY TO SEE MENGI(SURVEY SPONSOR?) AND SLAA ON THE FRONT PAGES!

Anonymous said...

Inasikitisha sana na inaonyesha jinsi gani sisi watanzania tulivyolala. Pamoja na ubadhilifu wote alioufanya Lowasa, tena mbele ya macho ya umma na hata kufikia kulazimika kujiuzuru kwa kashfa hizo. Leo bado tunasuburu kumuweka katika mstari wa mbele wa matukia yenye sura nzuri.
Sasa ni kuwa hatuna watu, tumechoka au ujinga uliokomaa mpaka tunang'ang'ania mijitu ya namna hii.
Mtamlaumu nani kesho akiiunza nchi yote kwa ajili ya tamaa. Hivi hamuogopi kuona mtu anang'ang;ania uraisi kama hivi, mnajua anachokitaka? Tusije kumtafuta mchawi kumbe sisi wenyewe.

Anonymous said...

Uduanzi mtupu!watanzania wengi ni bongo lala kama kweli izo ni kula zao!!