ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 28, 2014

JUMUIYA YA KIMATAIFA YASHAURIWA KUTOTAMBUA KUJITENGA WA CRIMEA

 .Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa  Ukraine, Bw. Andrii Deshchytsia akiwasilisha mbele ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Azimio ambalo pamoja na  mambo mengine limeitaka Jumuiya ya Kimataifa na  Mashirika ya Kimataifa, kutoitambua kura ya maoni iliyopigwa March 16 ya kujitenga  kwa Crimea  kutoka Ukraine na hatimaye kujiunga na Urusi, Ukraine inasema  kura hiyo  ya maoni si halali na ni njama za kumega mipaka halali ya nchi yake. Azimio hilo  lilipitishwa siku ya Alhamis kwa kura 100 za ndiyo, 11 za hapana na 58 hazikuegemea upande wowote.
Muwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Vitaly I. Churkin akitoa maelezo  kuhusiana na Azimio hilo lilowasilishwa na Ukraine na kuungwa mkono na nchi nyingi za Magharibi na zile za Ulaya, kwamba,  kujitenga kwa Crimea kulikuwa halali na  Urusi haikuwa na namna nyingine bali kuitambua  kura hiyo na kusisitiza kwamba kihistoria Crimea ni sehemu ya Urusi.

Na Mwandishi Maalum

Wakati  hali ya sintofahamu  ikiendelea kuwa tete  kufuatia    Crimea  kuamua kupiga kura ya maoni na hivyo  kujitenga kutoka Ukraine na kasha  kujiunga na Urusi.Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jana  alhamisi, limepiga kura  kupitisha  na kuunga mkono azimio ambalo pamoja na mambo mengine, linaitaka  Jumuiya ya Kimataifa kuto tambua kwa namna yoyote iile   kura  hiyo na kujitenga kwa Crimea kutoka  Ukraine.
Kabla ya tukio la upigaji kura kufanyika,  baadhi ya   wajumbe wanaoziwakilisha nchi zao, walitoa maelezo ya   kwa nini nchi zao zilikuwa  zimeamua kupiga kura  ya ama kuunga mkono azimio , kutoliunga mkono  au kutoegemea  upande wowote.
Baada ya  maelezo hayo,  matokeo ya kura yalikuwa ifuatavyo, Nchi 100 zilipiga kura ya ndiyo,  nchi 11 zikipiga kura ya   kulikataa azimio wakati nchi 58 zenyewe ziliamua kupiga kura ya kutoegemea  upande wowote.
Azimio hilo  liliwasilishwa  mbele ya wajumbe wa Baraza   Kuu la  Umoja wa Mataifa, na    Bw. Andrii Deschcytsia, Kaimu Waziri wa Mambo ya  Nje wa Ukraine   ambaye  katika  uwasilishaji wake alijenga  hoja zilizowataka wajumbe kuliunga mkono azimio hilo.

Naye  Muwakilishi wa  Kudumu wa Urusi  katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Vitaly I. Churkin yeye pamoja na kutetea  uamuzi wa serikali yake wa  siyo tu kutambua kura hiyo  ya maoni lakini pia kujitenga kwa  Crimea, alitoa hoja ya kutaka upigaji wa kura hiyo uwe  ni wa kura zilizohesabiwa ( recorded vote).
 Balozi Churkin alisititiza kwamba,  kura ya maoni iliyopigwa na wananchi wa  Crimea na hatimaye kuamua kujitenga na  kisha kujiunga na  Urusi  ilikuwa ni   ni kura halali na kwamba Urusi  haikuwa na  namna nyingine zaidi ya kuitambua kura hiyo.
Aidha  kupitia azimio hilo ambalo limepitishwa baada ya  Baraza Kuu la Usalama kushindwa kupitisha  azimio kama hilo mnamo March 15 siku  moja kabla ya kura  ya maoni kufanyika baada  ya Urusi kulipinga,  linayataka   pia Mashirika ya  Kimataifa  kuto tambua kujitenga kwa Crimea  na jiji la Sevastopol kwa  mujibu wa kura ya maoni ya   March 16.
Ingawa Baraza Kuu  la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio hilo,  azimio linakosa  nguvu kama ambavyo lingepitishwa na Baraza Kuu la Usalama.
Wengi wa wazungumzaji waliounga mkono azimio hilo,  au hata wale ambao hawakuegemea upande wowote,wamesisitiza haja na umuhimu wa kuheshimu  Katiba  ya Umoja wa Mataifa pamoja na  Misingi   ya sheria za kimataifa, ambazo pamoja na mambo mengine  zinasisitiza  kuheshimiwa kwa mipaka ya nchi na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyigine, pamoja na kuimarisha  umoja na  mshikamano
Baadhi ya wazungumzaji, wameleezea wasiwasi wao kuhusu kupitishwa wa azimio hilo ambalo  limeungwa mkono   karibu na nchi zote za Magharibi na zile za Ulaya  kuwa  kwa kufanya hivyo  ni sawa na kuchochea zaidi mgogoro huo.

No comments: