Utajua mbinu bora za kumpata mwenza sahihi lakini pia jinsi ya kuishi naye kwa raha mustarehe na kamwe asifikirie kukusaliti wala kukuacha. Mpenzi msomaji wangu, leo nataka kuzungumza na wanaume walio kwenye ndoa lakini pia si vibaya na wale wanaotarajia kuingia kwenye maisha hayo wakasoma.
Nimelazimika kuandika juu ya mada hii kutokana na namna ambavyo kasi ya wanaume kusalitiwa imekuwa kubwa huku wengine wakiombwa talaka na wake zao waliotokea kuwapenda.
Huwa nakaa na kujiuliza, inakuwaje mkeo ambaye aliapa kutokusaliti leo aamue kutoka kwenye ndoa na kwenda kumvulia nguo mwanaume mwingine?
Inakuwaje mwanamke anamuahidi mumewe kuishi naye kwa shida na raha lakini siku ya siku anaomba talaka tena macho yakiwa makavu?
Kwa hili unaweza kubaki njia panda lakini nilichokibaini ni kwamba, wanawake wengine wanakuwa na tamaa zao na wanaposhawishiwa, husahau viapo walivyotoa huko nyuma.
Mbali na hili nimegundua kuwa, baadhi ya wanaume wanasalitiwa na kuombwa talaka kwa sababu ya kushindwa kuchukua nafasi zao kama wanaume, na hili ndilo nitakalolizungumzia leo.
Baadhi ya wanaume wanakimbilia kuopoa wake wazuri lakini wakishaingia kwenye ndoa, wanajisahau na kubweteka.
Ifahamike kwamba, mwanaume anayemjali mpenzi wake ndiye anayetimiza wajibu wake, lakini wengi hujikuta wakitoswa na wapenzi wao kutokana na ufahamu mdogo ama dharau ya mambo madogomadogo.
Ni vyema ukatambua kuwa uhusiano hauna mambo ‘simpo’. Kila kitu kina umuhimu mkubwa kulingana na nafasi yake sambamba na utekelezaji wako.
Mwanamke anahitaji mahaba yaliyoshiba na hakika ukijua ‘kumhendo’ kama mke kwa kiwango kitakachomridhisha, hatawaza kukuacha wala kukutafutia mume mweziyo. Unawezaje kulifanikisha hilo?
Mpende, mheshimu, mjali
Najua unaweza kusema unampenda mkeo na ukawa unawaambia wenzako hivyo lakini je, unaonesha hivyo kwa vitendo? Je, ni kweli umempa nafasi kubwa kwenye moyo wako na kwamba yeye ndiye kila kitu kwako?
Tufahamu kwamba, mwanaume kupitia mapenzi yake ana uwezo mkubwa wa kumshika vilivyo mkewe na kumfanya asibabaishwe na wanaume wakware.
Ndiyo maana nasema kama mpenzi wako anakuacha na kwenda kwa mwingine au anakusubiri unakwenda kazini kisha anachepuka, ujue kuwa umeshindwa kuchukua nafasi yako kama mume.
Wanawake wanawapenda wanaume ambao huonesha upendo kwa vitendo, huonesha kujali, jasiri wasioogopa changamoto za kimaisha hivyo anza leo kutimiza wajibu wako, naamini utamfanya mwenza wako akuone ni wa pekee unayestahili kupendwa na kuheshimiwa.
Muoneshe kuwa umetulia
Hapa namaanisha kwamba, unatakiwa kumuonesha mkeo kuwa umetulia na si mtu wa kuchenguliwa akili na hivi visichana vya kizazi cha dot.com ambavyo haviangalii mume wa mtu wala nini. Wao wanachotafuta ni pesa hivyo watakutega kwa vivazi na hata kujilengesha kwako kwa kukupigia simu au kukutumia sms za kimapenzi.
Ili kumfanya mkeo awe na imani na wewe unatakiwa kuwapotezea. Kuwa makini nao na usiwaruhusu wakuzoee. Ukifanya hivyo na mkeo akajua si mtu wa kubabaishwa na micharuko, naye atatulia kwani atajua yuko na mtu makini.
Kumbuka ukiwa ni mtu wa kuendekeza ukaribu na hawa mabinti wasio na heshima, mkeo naye atajiweka karibu na masharobaro ambao wengi wao hawana heshima na wanaweza kumfanyia vitendo visivyo vya kistaarabu na hatimaye kuifanya ndoa yenu kuwa kama shimo la taka.
Mpe haki yake
Labda kama unaumwa au una matatizo yanayofahamika lakini ukweli ni kwamba, kama humpi mkeo haki yake ya ndoa kama inavyostahili, atavumilia sana lakini mwisho atakusaliti kama siyo kuomba talaka yake.
Katika hili naomba niseme kwamba, raha ya ndoa pamoja na mambo mengine ni pale mnapokutana faragha, ukimchengachenga mkeo wakati mwenzio anakuhitaji, unajitengenezea mazingira ya kuwapa mwanya wanaume wengine wakudokolee ‘chakula’ chako.
Mgeuze kuwa mchumba
Kumbuka yale uliyokuwa ukimfanyia mkeo enzi zile mkiwa wachumba mfanyie sasa. Mnunulie zawadi, mtoe ‘out’ siku mojamoja na mambo mengine ambayo unajua yatamfanya aamini bado unampenda licha ya kwamba mmekuwa pamoja kwa muda mrefu, hata kusaliti kamwe.
GPL
No comments:
Post a Comment