ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 6, 2014

Yanga yaishika pabaya Ahly

Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi kwenye uwanja wa Boko beach jijini Dar es Salaam jana. Picha na Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Uongozi wa Klabu ya Al Ahly ya Misri umekataa mchezo wa baina yao na wawakilishi wa Tanzania, Yanga kupigwa katika mji wa El Gouna na badala yake umependekeza ufanyike katika jiji la Alexandria.
Yanga na Ahly zitashuka uwanjani Jumapili hii kuumana katika pambano la marudiano la raundi ya kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika litakalochezwa huko Misri. Tayari Yanga imeenda Misri.
Katika pambano la kwanza lililofanyika Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ilichomoza na ushindi wa bao 1-0.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Al Alhy, Hadi Khashaba aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa klabu yake imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kwamba uwanja wa Gouna haukidhi mahitaji ya mechi hiyo.
Khashaba alisema badala yake klabu yake imependekeza mchezo huo ufanyike katika mojawapo ya viwanja vitatu ambavyo ni Alexandria, Burj Al Arab na Stade Borg vinavyopatikana katika jiji la Alexandria.
“Tumewasilisha barua Shirikisho la Soka Misri (EFA) tunasubiri taarifa ili tuweze kuandaa malazi ya wageni wetu ambao watafika hapa Alhamisi (leo),”alisema Khashaba.
Wakati Khashaba akitangaza msimamo wa klabu yake, juzi beki wa timu hiyo Said Ahmed Shedid akizungumza na mtandao wa klau hiyo alisema mchezo dhidi ya Yanga utakuwa mgumu kwao kama utachezwa El Gouna.
Aliitaja sababu kuwa ni hali ya hewa ya mji huo kufanana na ile ya Dar es Salaam ambako mchezo wa kwanza baina ya timu hizo mbili ulifanyika.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu aliliambia gazeti hili kuwa mpaka jana jioni klabu yake ilikuwa haijapokea taarifa rasmi ya wapi na uwanja gani mchezo huo utafanyika.
“Kimsingi mpaka sasa (jana jioni) sijapata taarifa yoyote kutoka kwa wenzetu wa Al Ahly kuhusiana na uwanja utakaotumika kwa ajili ya mechi kati yetu na wao na mechi itachezwa mji gani,”alisema Njovu.
Hata hivyo kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati ratiba ilipokuwa mechi za marudiano zinafanyika baada ya wiki mbili inaonyesha wenyeji walitakiwa kutoa taarifa ya uwanja kwa wageni siku 10 kabla, lakini baada ya mabadiliko yaliyofanyika kwa mechi kuchezwa baada ya wiki moja hakuna kanuni inayoonyesha wageni wapewe taarifa ya uwanja utakaotumika siku ngapi kabla ya mechi.
Mwananchi

No comments: