ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 11, 2014

KAMPUNI YA MWANANCHI YAZINDUA MTAMBO WA KUCHAPISHA MAGAZETI YAKE JIJINI MWANZA.


Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd. (MCL), jana ilizindua mpango kabambe wa kuchapisha magazeti yake jijini Mwanza na kuyasambaza asubuhi katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.

Akizindua uchapishaji wa magazeti ya kampuni hiyo ambayo ni Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti usiku wa kuamkia leo, Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula alisema hatua hiyo itawaepusha wasomaji wa maeneo hayo kusoma “habari viporo” walizokuwa wakipata kwa muda mrefu.


Mabula alisema upatikanaji habari kwa wakati kwa njia ya magazeti katika Kanda ya Ziwa umekuwa ni moja ya changamoto kubwa kwa miaka mingi.

“Ni moja ya vikwazo katika kasi ya kuleta maendeleo ya umma na mtu mmojammoja. Ndiyo maana nina hakika mmepata na mtaendelea kupata mapokezi ya kishindo kutoka kwa wakazi wote wa Kanda ya Ziwa,” alisema Mabula.

Aliainisha maeneo makuu manne ambayo MCL itakuwa imesaidia kuboresha kuwa ni ubichi wa habari kwa sababu Mwanza wamekuwa wakipata magazeti kuanzia saa nne asubuhi, huku mikoa ya jirani ikiyapata jioni au siku inayofuata.

“Tena hata hiyo saa nne ninayosema, magazeti yaliyokuwa yanafika muda huo sanasana ni Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, huku magazeti mengine yakifika wakati jua limesogea sana,” alisema.

Kuhusu ajira, Mabula alisema Wananyanza, yaani wakazi wa Kanda ya Ziwa, watakuwa na sauti maalumu kwenye magazeti ya MCL na kwamba haoni sababu ya kuzifanya taasisi mbalimbali kuepuka kutangaza biashara zao kwenye magazeti hayo.

Akimkaribisha Mabula, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MCL, Zuhura Muro alisema ni mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa Taifa, kwa watu wa Kanda ya Ziwa kupata na kusoma gazeti lililochapishwa siku hiyo kwa wakati na habari zikiwa motomoto.

Muro alisema Kampuni ya MCL inaamini haki ya kupata habari ni ya msingi kwa binadamu wote, bila ubaguzi wa aina yoyote.

“Tunaamini katika misingi ya kutoa habari za ukweli, zilizotafitiwa kwa kina, zisizoshinikizwa na kundi lolote na zisizokuwa na upendeleo wa aina yoyote,” alisema Muro.

Alisema utafiti walioufanya unaonyesha kuwa asilimia 0.1 ya watu wa Kanda ya Ziwa ndiyo wanaosoma magazeti, idadi ambayo ni ndogo na inaminya watu kujua fursa walizonazo kujiletea maendeleo.

“Hali hii inasikitisha sana. Kwa Kweli ni jambo ambalo halieleweki kuona kanda yenye utajiri mkubwa na idadi kubwa ya watu inakuwa haipati huduma za habari kama inavyostahiki,” alisema na kuongeza

No comments: