ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 14, 2014

Chenge amnyima Maghembe usingizi

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge,Andrew Chenge.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Andrew Chenge, amethibitisha kuzuiwa kwa bajeti ya Wizara ya Maji na kusema kuwa kamati yake haitakubali kupitisha bajeti ya wizara yoyote ambayo utekelezaji wa miradi ya maendeleo utakuwa wa kusuasua.

Alisema kamati hiyo inaishikilia bajeti ya Wizara ya Maji kutokana na fedha za miradi ya maendeleo kutopelekwa kwa asilimia 50 na hivyo kukwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi.

Akizungumza na NIPASHE jana, Chenge alisema bajeti hiyo ilipelekwa mbele ya kamati yake na kubaini kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 unaotarajiwa kumalizika Juni 30, mwaka huu, fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi hazikufika na hivyo miradi imekwama.

Alisema katika kamati yake hawatapitisha bajeti ya wizara nyingine ambayo imeshindwa kufikisha utekelezaji wa miradi kwa asilimia 50.

“Ahadi ni deni, katika bajeti ya mwaka jana waliahidi, lakini hawakutimiza, mimi nasimamia ahadi yao, tumewarudisha Wizara ya Maji watuletee majibu ya kuridhisha, iwapo hayatakuja tutatoa taarifa kwa Bunge ili waamue,” alibainisha Chenge.

Alisema kati ya Sh. bilioni 184 ambazo serikali iliahidi kuongeza kwenye bajeti ya maji ni Sh. bilioni 86 tu zilipelekwa huku zaidi ya Sh. bilioni 98 hazikupelekwa na kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini.

Chenge alisema iwapo kamati yake itapelekewa bajeti hiyo bila mabadiliko yoyote, kamati itatoa taarifa bungeni na kwamba katika kila bajeti wanachoangalia ni miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, alipoulizwa juu ya bajeti za Wizara ya Nishati na Madini na Ujenzi, alisema bado hazijafika mbele ya kamati yake na kusema iwapo zitafika bila kiasi cha zaidi ya asilimia 50 ya fedha kutekeleza miradi ya maendeleo, watachukua hatua.

Jumapili iliyopita, ofisa mmoja alisema kuwa hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu kati ya Sh. bilioni 312.1 fedha za ndani za miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge kwa wizara ya Maji, ni Sh. bilioni 86 tu zilikuwa zimetolewa na serikali, sawa na asilimia 27 ya fedha zote.

Kwa maana hiyo, wakati mwaka wa fedha wa 2013/14 umebakisha mwezi mmoja na ushei kumalizika ifikapo Juni 30, mwaka huu, asilimia 73 ya fedha zote za ndani za maendeleo sawa na Sh. 236.1 haijulikani zitapatapatikana kwa miujiza gani, hali ambayo imewakera mno wabunge kwa kuwa maji salama hayatapatikana kwa wananchi.

“Kama miezi 11 Hazina haikutoa fedha hizo, unafikiri mwezi mmoja zitatoka wapi Sh. zaidi ya bilioni 200? Hii ni balaa ndugu yangu,” alisema ofisa huyo kwa sharti la kutokutajwa jina.

Wiki iliyopita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, bila kutaja alisema zipo bajeti za Wizara mbalimbali zinashikiliwa na kamati ya bajeti.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika, Jumapili iliyopita alisema anakusudia kuandika barua kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kumtaka asiwasilisha bajeti yake kutokana na serikali kawadanganya wabunge.

Alisema fedha hizo kiasi cha Sh. bilioni 184 zilielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya programu ya maji vijijini na mijini kwa vijiji kumi kila wilaya na mpango mahususi wa kushughulikia tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema katika randama za Bajeti ya Wizara ya Maji ambazo zilitakiwa kuwasilisha bungeni Jumatatu ya wiki hii kwa mujibu wa ratiba ilionyesha kuwa miradi haijatekelezwa, zabuni imetangazwa, bado haujakamilika huku fedha za miradi ya maendeleo zikikwama kufika wizarani.

Aidha, kabla ya Mbunge huyo kuwasilisha barua kwa Waziri wa Maji, na kutaka bajeti hiyo iondolewe na kurudishwa kwenye kamati ya bajeti, kamati ya Bajeti ilishachukua hatua za kuishikilia bajeti hiyo.

Kutokana na kamati ya Chenge kuingilia kati, bajeti ya waziri Maghembe haijulikani lini itawasilishwa.

MAWAZIRI WENGINE KILIO
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, jana alisema kuwa zaidi ya Sh. trilioni 1.2 zilizoidhinishwa na Bunge, kati yake Sh. bilioni 245.6 zikiwa ni kwa ajili ya maendeleo, hadi kufikia Machi mwaka 2014, Wizara ilipokea zaidi ya Sh. bilioni 768.5 tu sawa na asilimia 69.7.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 719.1 zilikuwa za matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 49.4 sawa na asilimia 20.1 za shughuli za maendeleo.

Naye Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipowasilisha bajeti yake Jumamosi iliyopita, alisema kati ya Sh. bilioni 81 zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hadi kufika Machi 31, 2014, ni Sh. bilioni 26.9 tu sawa na asilimia 66.03 zilizotolewa.

Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ilitengewa Sh. bilioni11.6, hadi sasa imepewa Sh. bilioni 4.0 tu.

WAZIRI WA FEDHA
Wakati mawaziri wakilia ukata kukwamisha miradi ya maendeleo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, aliwaeleza wabunge Aprili 30, mwaka huu kuwa makusanyo ya mapato ya serikali yamefikia Sh. trilioni 11 sawa asilimia 93 ya makadirio ya mapato ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.

“Katika kipindi hicho mapato yote ya serikali yalikuwa Sh. trilioni 11 sawa na asilimia 93 ya makadirio ya mwaka 2013/14,” alisema na kuongeza kuwa kuna upungufu wa asilimia saba tu kwenye bajeti hiyo na kwamba endapo mwenendo huo utaendelea bila kudhibitiwa, kuna uwezekano wa kumaliza mwaka wa fedha 2013/14 na nakisi ya bajeti.

NIPASHE iliomba ufafanuzi wa maelezo hayo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, aliyetafsiri kuwa kuna ukosefu wa fedha unaoweza kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli za kawaida za uendeshaji wa serikali ambazo ni pamoja na kutoa huduma na kulipa mishahara.

Hata hivyo, alisema hatua zinachukuliwa ili kuzuia hali hiyo isitokee.

Jana NIPASHE lilipomuuliza Waziri Mkuya kuhusiana na wizara kadhaa kusuasua katika utekelezaji wa bajeti zao katika miradi ya maendeleo, alisema atalizungumzia hilo baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha Juni 30, mwaka huu.

“Mwaka wa fedha 2013/2014 bado haujamalizika, hivyo kama kuna baadhi ya wizara hazijakamilisha miradi yake ambayo ilitengewa bajeti, tutaangalia baada ya mwaka kuisha,” alisema Waziri Mkuya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: