ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 15, 2014

UNAKAZANA KUMUITA MUMEO ‘BABY’, VIPI HILI LA KUMUOGESHA?


Ni wiki nyingine tulivu tunakutana tena kupitia safu hii namba moja kwa kuandika makala zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi. Ni matumaini yangu kuwa umzima na unaendelea vyema na mihangaiko yako ya kila siku ikiwa ni katika kujihakikishia maisha ya furaha na amani.

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nitazungumzia mambo ambayo baadhi ya watu walio kwenye uhusiano huona kuyafanya wakiwa na wapenzi wao ni ushamba bila kujua faida zinazoweza kupatikana.
Nazungumzia ubunifu wa baadhi ya wanawake kutoishia kuwapelekea waume zao maji bafuni bali wakati mwingine nao kuingia na kuonesha mahaba yao kwa kuwaogesha.

Katika mapenzi, yapo mambo ambayo unaweza ukayadharau ukidhani hayana umuhimu lakini nikuambie tu kwamba, mapenzi yanadumishwa kwa vitu vidogovidogo sana. Kwa mfano, wapo ambao tangu wameingia kwenye uhusiano hawajawahi kuwanunulia zawadi wapenzi wao.

Hawaoni umuhimu wa kufanya hivyo na wakati mwingine wanakwenda mbele zaidi kwa kusema, hayo ni mambo ya kizungu. Sikatai kwamba masuala ya kadi na zawadi ni ya kizungu zaidi lakini kuna ubaya gani kuiga kwa nia nzuri? Walioiga katika haya waliona faida zake, ndiyo wale ambao wanadumu kwenye uhusiano wao.

Wewe hutaki uhusiano wako unga’re? Kumnunulia mpenzi wako zawadi au kumpa kadi yenye maneno mazuri kunakupunguzia nini kama mpenzi wako atajisikia mwenye kuthanimiwa kwa kufanyiwa hayo?
Ukiacha hayo ambayo si lengo langu kuyazungumzia, nirudi kwenye hili la wapenzi kuogeshana.

Hili si geni kwenye jamii yetu. Tunaoishi nyumba za kupanga tunawaona wanandoa wakiingia bafuni na kuchukua muda mrefu huko wakifanya yale ambayo wanaamini ni sehemu ya kuboresha penzi lao, sioni tatizo katika hilo.

Nasema sioni tatizo na siyo ushamba hata kidogo kwa sababu, lengo hasa la hayo kufanyika ni kuboresha mapenzi na yanafanyika kwa usiri. Kinachonishangaza sasa, kuna baadhi ya watu wanaona wapenzi kuogeshana ni kukosa kazi ya kufanya.

Kwanza ifahamike kwamba, wawili waliopendana wanapofikia hatua ya kuoana wanakuwa mwili mmoja. Wanashirikiana katika mambo mengi na hakuna siri yoyote kati yao.
Ndiyo maana hata kwenye suala la kuoga pamoja, si jambo la kushangaa. Wanaojua mahaba wamekuwa wakifanya hivyo na imekuwa ni chachandu ya penzi lao.

Pengine unaweza kujiuliza faida za kufanya hivyo. Iko hivi, kwa taratibu za kindoa, mke anatakiwa mumewe anaporudi kutoka kwenye mihangaiko yake amuandalie maji. Ampelekee bafuni na kumuwekea kila kinachohitajika ikiwemo sabuni, taulo na vitu vingine.

Lakini ifahamike kwamba, kimahaba mke na mume kuna wakati wanakuwa kama watoto. Ndiyo maana unaweza kukuta mke anamuogesha mumewe, anamsugua, akimaliza anamfuta kisha anamchukua na kumpeleka chumbani. Wapo wanaofanya hivyo lakini najua wewe unaweza kuona ni jambo la ajabu sana.

Ninachotaka kusema katika hili ni kwamba, wanandoa kuogeshana si kwamba hawawezi kuoga wenyewe. Hilo linafanyika katika kuonesha mahaba. Kama mke anaweza kumuita mumewe baby, inashindikana vipi mke kumuogesha baby wake?

Kama mume anamuita mkewe baby, kuna tatizo gani mume kumlisha mkewe? Sidhani kama kuna tatizo. Yote haya yanafanyika ikiwa ni katika jitihada za kunogesha mahusiano yetu na si ushamba kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

Mimi nadhani tuna kila sababu ya kuwa wabunifu wa mambo ambayo yatatufanya tuonekane wa pekee kwa wenza wetu. Hilo la kuogeshana ni moja tu kati ya mengi ambayo tunatakiwa kuwafanyia wapenzi wetu kuonesha tunavyowapenda.

Tukumbuke kwamba, tunapolala na mapenzi yetu yanalala na yakilala, hakutakuwa na furaha. Tuyaamshe na kuyachangamsha kwa kufanyiana vitu adimu. Na nikuambie tu kwamba, utundu na ubunifu wako ndiyo silaha pekee ya kulidumisha penzi lako.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

The mdudu,ww ni mwehu kila kukicha ww ni ngono tu kwenda mbele hebu muogope mungu kwanza hivi ni nani hasa unaemfundisha hayo mambo ya ngono? Hakuna mtt mdogo hapa kila mtu anaweza kulilima shamba lake awezavyo