Katika historia fupi, Mzee Small alipata elimu ya msingi
katika Shule ya Mingumbi huko Kilwa mkoani Pwani. Mbali na kuwa mkongwe,
Mzee Small kila ulipobahatika kuzungumza naye alikuwa na kawaida ya
kutamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania Bara kuchekesha
runingani.
Mzee Small alianza sanaa hiyo yapata miaka 31 iliyopita na
alipata kufundishwa na mwigizaji Said Seif ‘Unono’ (ambaye pia kwa sasa
ni marehemu).
Mbali na kushiriki sanaa katika vikundi mbalimbali, Mzee
Small wakati wa uhai wake ametumika katika vikundi vya mashirika kama
vile Reli, NASACO na mengine mengi, ambayo kwa sasa hayajihusishi tena
na shughuli hizo.
Mzee Small alianza kujulikana sana katika fani ya uchekeshaji
hasa pale alipoibuka na mchezo uliojulikana kama 50, 50, 100, na ule wa
Mjini Shule uliomwelezea mwanamke wa kijijini aliyeolewa mjini.
Mbali na kutamba na michezo hiyo, Mzee Small alikuwa ni
mcheshi na mwenye kupenda utani wakati wote, aliibuka na kichekesho
kisemacho Nani Mwenye Haki, ambacho baadaye alikiboresha zaidi.
Baadaye aliibuka na kitu kingine kikali kilichokwenda kwa
jina la Nani Kama Shule, huku akiwa amewashirikisha wakali wengine kama
King Majuto, Kingwendu na wachekeshaji wengine wanaotamba kwa sasa
Bongo.
Mzee Small alikuwa ndiye mmiliki wa kundi la sanaa
linalojulikana kama Afro-Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kutoa ajira kwa vijana wa mitaani.
Pamoja na kuwa na uzoefu wa kisanaa, lakini mkongwe huyo
hakuwahi kuwa na mpango wa kujiunga na kundi lingine, ila alichokuwa
akifanya ni kurekodi na wasanii wengine alipokuwa akiitwa kwa
makubaliano maalum.
Pia mkali huyo wa vichekesho enzi za uzima wake na uhai wake
alikuwa akijishikiza katika duka moja Kariakoo la Home Shopping Centre
kimatangazo.
Kutokana na vichekesho, Mzee Small huwa anatania kuwa sanaa
ilimpa mke wa ndoa katika televisheni ambaye ni Bi Chau huku akianisha
kuwa mkewe, Bi Fatuma huwa hana tatizo lolote na Bi Chau kwani anajua
kinachoendelea kuwa ni kazi tu.
MATESO YA KIAFYA
Wakati akiendelea na harakati za kisanaa, mwaka juzi Mzee
Small aliripotiwa kupatwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alipokuwa
kwenye shughuli za kisanaa Kanda Ziwa.
Ugonjwa huo ulimpa mateso makubwa huku akiwa hana msaada
wowote. Wakati akiteseka na kiharusi alipata tatizo linguine kwenye
ubongo huku akitakiwa kila mwezi kwenda kliniki kwa ajili ya ‘check- up.
Hakika kila nafsi itaonja mauti na leo Mzee Small ambaye
mbali na kuiburudisha alikuwa akitoa mafunzo kwa jamii yetu kupitia kazi
zake, leo ameonja mauti na Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ampunzishe
Mkali huyo wa vichekesho mahali pema.
-Father Kidevu Blog
2 comments:
Wasanii wa Tz jiandaeni na maisha ya uzeeni kwani kila msanii akifikwa na maradhi uzeeni anasubiri michango ya watu, yeye mwenyewe anakua hana akiba yeyeyote. Bila kuchangiwa hali inakuwa mbaya sana. mfano: Mzee Kipara, Gurumo, Jose Maina, Gebo Peter, Bi Kidude, aliyewai kuwa kocha wa makipa wa Yanga n.k.
Jueni kuwa mchango wenu kwa jamii ni bure hauthaminiwi wakati wa shida, jiandaeni kwa kuweka akiba sio matanuzi tu na kujiona watu muhimu sana machoni mwa wengine
INNA LILLAHI WIANA ILLAHIM RAJIUN sote ndo njia tutakayopita hii polesni sawa wafiwa wote ndugu na jamaa na marafiki wa mzee small
tutaku miss sana sana kabisa mzee wetu kwa vichekesho vyako.
Post a Comment