ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 22, 2014

Marekani inathibitisha kifo cha Ballali

Ballali alilazwa katika hospitali mbili tofauti kabla ya kufariki dunia.
Neville Meena, Mwananchi
Taarifa za Idara za Serikali ya Marekani zinathibitisha kwamba aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali alifariki dunia akiwa Washington DC, akiwa na umri wa miaka 66.
Gazeti hili lilianza kufanya uchunguzi kuhusu ukweli wa kifo cha Ballali miaka miwili iliyopita, kutoka na kuwapo kwa mkanganyiko na sintofahamu kuhusu kifo hicho, vilivyosababishwa na jinsi alivyoondoka nchini Agosti 2007, kuugua kwake, mazingira ya kifo na hata usiri uliotawala mazishi yake.
Mbali na Mwandishi wa Mwananchi kufika alikozikwa kwenye Makaburi ya Gate of Heaven, eneo la Silver Spring, Maryland nchini Marekani mwanzo ni mwa mwezi huu, taarifa rasmi za Serikali ya Marekani zinaonyesha kuwa Ballali alifariki dunia Mei 16, 2008.
Taarifa rasmi za idara zenye dhamana ya kutunza rekodi mbalimbali za watu wanaoishi Marekani zinaonyesha kwamba mara ya mwisho Ballali alikuwa akiishi Washington DC na alifariki akiwa na umri wa miaka 66.
Taarifa hizo zinapatika katika Idara za Serikali ya Marekani zinazotambuliwa kama United States Vital Records na United States Public Records Index, ambazo zinahusisha majina ya watu, ndoa, ndoa zilizovunjika, anwani za makazi yao ya sasa na walikowahi kuishi kabla, namba ya huduma (social security number) na taarifa nyingine muhimu.
Taarifa hizo zinaonyesha kuwa kabla ya kuishi Washington DC, Ballali aliwahi kuishi Potomac, Maryland katika anuani inayosomeka 11514 Seven Locks Rd, pia aliwahi kuishi Potomac, Maryland 20854 kwenye anuani 1801 45th St NW # 302 na pia Washington, Dc 20007 kwenye anuani za 13017 Parkland Dr na Rockville, Maryland 20853.
Rekodi hiyo namba 143502395 inawataja watu wanaoweza kuwa na ukaribu na Ballali kuwa ni A. R. Ballali, Elizabeth T. Ballali, Octavio T. Ballali, Rachel J. Ballali. Pia zipo taarifa zinazomtaja Anna Muganda kuwa mmoja wa watu wa karibu wa Ballali.
Ufuatiliaji uliofanywa Mwandishi wa Mwananchi zimethibitisha kwamba Elizabeth ni dada yake na Ballali wakati Octavio na Rachel ni watoto wa Gavana huyo aliowazaa na mke wa kwanza, Malva Ballali ambaye ni Raia wa Agentina.
Inaaminika kuwa Anna, Malva, Octivio na Rachel ndiyo wanaofahamu ukweli kuhusu kilichosababisha kifo cha Ballali, lakini kwa nyakati tofauti watu hao wa karibu na marehemu hawakuwa tayari kueleza kilichotokea.
Ndugu wa karibu wa Anna wanasema mwanamama huo ambaye alikuwa na Ballali mpaka pumzi yake ya mwisho, hayuko tayari kuzungumzia suala hilo na kwamba hapendi kabisa kukumbushwa uchungu wa kifo cha mumewe.
Juzi Mwandishi wa Mwananchi alijaribu kuwasiliana na Octavio na mama yake, Malva, lakini wote kwa pamoja walirejesha ujumbe kwamba hawana cha kuzungumza, kwani wao mbali na kwamba hawakuwahi kuishi Tanzania, wasingependa kurejea machungu yaliyowakuta.
Simu kwa familia
Wakati hayo yakidhihiri, baadhi ya wanafamilia Ballali wamesema walipigiwa simu mara kadhaa, wakiulizwa iwapo ndugu yao huyo bado yuko hai au amefariki dunia.
Wakizungumza na Mwanadishi wa Mwananchi nchini Marekani, baadhi ya ndugu wa Ballali walisema takriban miezi mitano kabla ya kukutwa na mauti, walipokea simu hizo kutoka Ubalozi wa Tanzania, Washington DC, ukihoji iwapo Gavana huyo alikuwa hai au amekufa.
Walisema taarifa hizo ziliwashtua na hawakufahamu sababu za kuulizwa huko kwani hata kama Ballali angekuwa amefariki dunia, wao ndiyo walipaswa kutoa taarifa za kifo chake na siyo taarifa hizo kutoka Tanzania.
“Mara ya kwanza tulipigiwa simu alfajiri kutoka kwa Ofisa wa Ubalozi, Joseph Sokoine akituuliza kwamba amepata taarifa kutoka nyumbani Tanzania kwamba Ballali amefariki dunia,” alisema mmoja wa ndugu hao, jina tunalihifadhi kwa sasa na kuongeza:
“Baada ya kupata simu hiyo, nilimtafuta mke wa marehemu (Mama Anna Muganda) wakati huo walikuwa bado wako Boston, lakini ndiyo walikuwa wameruhusiwa kutoka Hospitali ya Massachusetts, nilimuuliza kuhusu hali ya mgonjwa akasema hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri”.
Alisema baada ya kupata uthibitisho huo alimpigia Sokoine na kumjulisha kwamba taarifa hizo hazikuwa za kweli kwani mgonjwa alikuwa akiendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa na kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Ndugu huyo wa Ballali alisema baada ya wiki mbili, walipokea tena simu kutoka kwa Sokoine na zamu hii waliwaambia kwamba alikuwa amepokea simu kutoka Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, wakiuliza kuwapo kwa taarifa kuwa Ballali alikuwa amefariki dunia.
“Baada ya kupokea simu hiyo tulifuatilia tena Boston na tuliambiwa Ballali alikuwa mzima. Nilimuuliza Joseph (Sokoine), kama mgonjwa angekuwa amefariki wakati huo, taarifa zilipaswa kutoka upande gani? Maana kama mgonjwa tulikuwa naye sisi basi ndiyo tulipaswa kuwapa taarifa zote na siyo nyumbani Tanzania kutuarifu sisi,” alisema ndugu huyo.
Balozi Sokoine
Akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi jana, Balozi Sokoine ambaye hivi sasa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alikiri akiwa ubalozini mara kadhaa waliipigia simu familia ya Ballali kwa lengo la kufahamu maendeleo ya ugonjwa wake.
“Nakumbuka kuwapigia simu ndugu wa marehemu Ballali na siyo mara moja, lakini tulikuwa tunafuatilia maendeleo ya mgonjwa na tulikuwa tunampigia simu mke wake, Mama Muganda na ndugu wengine walioko Marekani,” alisema Balozi Sokoine.
Kuhusu iwapo waliwahi kuulizia taarifa za kifo cha Ballali, balozi huyo alisema: “Nakumbuka pia tuliwahi kuulizia suala hilo kutokana na rumors (uvumi) uliokuwa umeenea Tanzania kwamba Ballali amefariki, kwa hiyo tulipowaulizia wanafamilia walituambia kwamba alikuwa hai bado”.
Balozi Sokoine alisema miongoni mwa watu ambao aliwahi kuzungumza nao wakati huo ni kaka wa Anna, Emmanuel Muganda ambaye alisema aliwapa ushirikiano wa kila aina kuwawezesha kupata taarifa wakati Ballali alipokuwa mgojwa.
“Bwana Muganda (Emmanuel) nakumbuka wakati tukifuatilia taarifa hizo alitusaidia sana kufahamu hali ya mgonjwa na hata tulipomuuliza kuhusu rumors (uvumi) huo naye alisema walikuwa wakiulizwa na ndugu wa Tanzania kuhusu suala hilo,” alisisitiza Balozi Sokoine.
Kwa upande wake Muganda ambaye alipata kuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili y Sauti ya Amerika (VOA), alikiri kupokea simu kadhaa kutoka Ubalozi wa Marekani, lakini akasema hakuwa akikumbuka hasa ni kitu gani alichoulizwa kuhusu ugonjwa wa Ballali.
“Yes (ndiyo) walikuwa wakipiga simu mara nyingi na lilipojitokeza suala la uvumi wa kifo cha Ballali na wao kutuuliza, tulihoji kwamba kwanini pengine taarifa hizi zisitoke kwenye familia kwenda serikalini na badala yake wao ndio walikuwa wanauliza,” alisema Muganda ambaye bado anaishi Marekani mpaka sasa.
Kuugua kwake
Baadhi ya ndugu na familia wa Ballali wanasema wakati alipoondoka kwenda Marekani, Gavana huyo alikiwa mzima na kwamba alilazwa baada ya vipimo alivyofanyiwa katika Hospitali ya Massachusetts, Boston alikokwenda kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Mjini Washington DC, gazeti hili liliambiwa kuwa Ballali alikuwa amepanga kurejea Tanzania baada ya uchunguzi huo, lakini baada ya kufanyiwa vipimo hivyo daktari wake alimlaza kutokana na kubaini tatizo kwenye utumbo wake mpana.
Mmoja wa ndugu zake alidokeza kuwa tatizo aliloliona daktari kupitia vipimo vya kitaalamu, lilikuwa ni tofauti kabisa na tatizo halisi, hivyo alishauriana na mwenzake aliyekuwa Washington hivyo kumtibu matatizo yote mawili.
Alifanyiwa upasuaji mkubwa na baada ya kupata nafuu aliruhusiwa kurejea nyumbani na baadaye kurudi Washington DC, lakini Aprili 2008 aliumwa tena na kulazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown. Alikaa hospitalini hapo hadi mwanzoni mwa Mei mwaka huo, alipoambiwa na madaktari kwamba asingeweza kupona na kwamba mauti ingemkuta katika wiki mbili.
Ballali alirejeshwa nyumbani kwake, Washington DC ambako aliendelea kuugua na hatimaye kukutwa na mauti Mei 16, 2008, kisha kuzikwa katika makaburi ya Gate of Heaven yaliyopo Silver Spring, Maryland, Mei 23. Nyuma ya kifo chake aliacha maelekezo kwamba pindi atakapofariki dunia, mwili wake usiwekwe hadharani kwa maana ya kutizamwa na watu nje ya familia wala kusafirishwa kuja Tanzania kwa ajili ya maziko.
Gazeti hili liliwasiliana na hospitali zote mbili ambako Ballali aliwahi kulazwa, lakini lilijibiwa kwamba taarifa za mgonjwa huyo zinaweza kutolewa tu ikiwa familia ndiyo inayozihitaji.
Mwananchi

No comments: