ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 9, 2014

MNAOCHUKIA HAINA MAANA, KUBALINI KUJIFUNZA KWA DIAMOND!

KWENU,
Wasanii wote wa Tanzania. Hongereni kwa kazi na namna mnavyojituma kupitia sanaa zenu. Ni jambo zuri tena la kujivunia maana mmetambua vipaji vilivyo ndani yenu na kuvitumia kujipatia riziki.

Kwa upande wangu, naendelea vizuri. Nawatakia heri wasanii wote Waislam walio kwenye funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ni mwezi ambao kwa hakika, tunahitaji kuwa na subira na utulivu wa hali ya juu.

Nimeona ni vyema leo nizungumze na wasanii wote kwa pamoja. Ndugu zangu, katika kila kinachofanywa na binadamu, kama akitaka kiwe na mafanikio ni lazima kuwe na juhudi, ubunifu, nia na malengo.

Unaweza kuwa na vyote au kimojawapo ambacho kwa hakika kitakusaidia kupata vingine kisha kupaa kwenye kilele cha mafanikio. Hapa nitoe mfano mmoja mzuri sana kwa Diamond. Huyu bwana mdogo hana muda mrefu sana kwenye game.


Ameibuka juzijuzi tu, lakini kutokana na juhudi, ubunifu, nia na malengo amefanikiwa na anazidi kupaa kimafanikio. Diamond tangu ameanza na kibao chake cha kwanza kabisa alijitahidi kuendelea kuongezeka na siyo kupungua.

Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya mpaka sasa anafanya vizuri kimataifa. Kwa bahati mbaya sasa, wapo baadhi ya wasanii (hasa wa muziki wa Bongo Fleva) wanamuonea kijicho! Nasisitiza baadhi.
Hawafurahishwi na mafanikio yake. Mbaya zaidi, sumu imesambaa sasa mpaka kwa baadhi ya mashabiki. Chuki tu! Kwa nini yeye? Kwa nini afanikiwe kimuziki? Kwa nini aorodheshwe kwenye kugombea tuzo? Kwa nini? Kwa nini?!

Diamond aliposhindwa kutwaa Tuzo za MAMA zilizofanyika hivi karibuni nchini Afrika Kusini, baadhi ya watu waliandika mambo ya ajabu sana kwenye mitandao ya kijamii.

Wengine walifikia hatua ya kusema kuwa, eti kama Diamond angeshinda watu wasingekunywa maji! Huo ulimbukeni tunaupata wapi ndugu zangu? Diamond ni nani? Jibu ni rahisi tu. Ni Mtanzania.
Anapokwenda kushiriki tuzo za kimataifa anasimama kama Mtanzania. Hiyo ndiyo sababu hata rais wetu, Dk. Jakaya Kikwete aliona umuhimu na akampongeza maana aliwakilisha taifa.

Kuwa kwenye kinyang’anyiro pekee ni ushindi tosha. Kuna wasanii wangapi Afrika? Kwa nini amechaguliwa yeye? Kwa nini si wengine? Kwa nini hukuchaguliwa wewe?

Kama una roho hiyo ya korosho, achana nayo. Ni ushamba. Piga kazi utafanikiwa. Kwanza Mungu hawezi kumsaidia mtu ambaye ana roho mbaya, asiyependa mafanikio ya mwenzake.
Safisha moyo wako, fanya kazi kwa bidii, ongeza ubunifu, angalia soko linahitaji nini, kisha achia kitu hewani – utavuma! Bila shaka ndivyo anavyofanya Diamond.

Juzi tu ametoka Marekani alipokuwa akishiriki kwenye Tuzo za BET. ni mafanikio hayo. Lakini kwa sababu ni tuzo za kimataifa, hatuwezi kusema ni mafanikio yake peke yake. Ni mafanikio ya wasanii wote wa Tanzania.

Mafanikio ya Watanzania wote. Ni mafanikio yetu. Kwa nini asipongezwe? Kwa nini tusijipongeze? Kwa nini tusijifunze kupitia kwake? Chondechonde wenye roho za kwa nini, hazina maana, pambaneni.
Ukiona rafiki yako amenunua gari zuri, usiumie – iwe changamoto kwako na ikupe hasira ya kusaka mafanikio. Hata ukichukia, hakuna kitakachobadilika, sanasana utakonda bure!
Yuleyule,
Mkweli daima,
...............................
Joseph Shaluwa GPL

1 comment:

Anonymous said...

Hapo Joe umenena kabisa. Tuwe na wivu wa maendeleo na sio wivu wa chuki. Chuki haitatusaidia kitu chochote. Zaidi itakukondesha na kukunyima usingizi. Tuwe na mentality ya "why not me." Japo kwa uzuri na sio kwa ubaya. Kama unakuwa na wivu na chuki kwa mwenzako kwa sababu ya maendeleo yake na kutokana na bidii zake, you are a looser. Na wewe fanya vyako kwa bidii zote na utafanikiwa, why not?