Dar es Salaam. Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mbagala, Dar es Salaam, Paulo Mwandemre (30) amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu kifuani na ‘vibaka’.
Tukio hilo lilitokea jana saa 7.00 mchana wakati Mwandemre alipokuwa akitoa darasani kutimiza majukumu yake.
Mkuu wa Shule hiyo, Macelina Kimario alisema vijana hao walikuwa wakizungumza na wanafunzi ndipo Mwandemre alikwenda kuwauliza wanafunya nini.
“Alipowauliza wanafanya nini ndipo kulitokea kutokuelewana na aliwakamata wote wawili na alipokuwa akiwapeleka ofisini ndipo mmoja aliyekuwa na kisu akakitoa na kumchoma kifuani,” alisema Kimario.
Aliongeza: “Mara baada ya kumchoma mmoja alikamatwa na mwingine alikimbia huyu aliyekamatwa tulimweka ndani na wanafunzi walikuwa wakimtaka ili wamwadhibu lakini tuliwazuia hadi polisi walipofika na kumchukua. Mwalimu alipelekwa katika Hospitali ya Zakiem na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa matibabu.
Mwandishi wa habari hizi alimkuta Mwandemre akiwa amelazwa wodi namba saba na hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.
“Sitaki kuzungumza na waandishi..... mimi sitaki wala kupigwa picha......niacheni,” alisema Mwandemre akiwa wodini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema vijana hao wawili walikuwa eneo la shule na walipomuona Mwandemre akipita na mfuko mdogo walimvamia na kuuchukua.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment