Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu msimamo wao wa kutorudi bungeni kujadili Rasimu ya Katiba Mpya. Wengine ni wenyeviti wenza wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) na James Mbatia. Picha na Michael Matemanga
Dar es Salaam. Joto la Katiba Mpya linazidi kupanda nchini, huku baadhi ya wasomi na makundi mbalimbali ya watu wakizidi kutilia shaka utapatikanaji wa Katiba hiyo.
Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya (KSL), Profesa Patrick Lumumba na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu wameonya kwamba kwa hali ilivyo hivi sasa hakuna Katiba Mpya inayoweza kupatikana.
Wakizungumza katika mdahalo uliohusu mivutano ya makundi katika mchakato wa Katiba Mpya jana jijini Dar es Salaam, walisema kuwa CCM haikuwa na nia njema tangu mwanzo, huku Rais Jakaya Kikwete akitajwa kushindwa kusimamia ipasavyo.
Profesa Lumumba alisema Katiba ya Tanzania imejaa viraka na kwamba inahitajika Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa ya Watanzania na karne ya 21, itakayokwenda sambamba na changamoto za Afrika Mashariki.
Alisema nchi za Afrika Mashariki zilipata katiba zao kwa njia ya machafuko, hivyo Tanzania lazima itafute njia sahihi inayokubalika kwa wananchi wote bila ya kuwepo kwa kundi moja linalotaka kuhodhi mchakato wa Katiba Mpya.
“Tanzania ina nafasi ya pekee na kihistoria kujipatia Katiba Mpya bila vita na itakuwa ni jambo la kusikitisha ikiwa kwa mtazamo finyu ya kivyama utanyimwa na wanasiasa ambao fikra zao si za kukidhi matakwa ya katiba,” alisema Profesa Lumumba.
Alieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa alifanya makosa katika kusimamia mchakato wa Katiba Mpya, hivyo Watanzania wanapaswa wamsamehe ili mambo yaende sawa.
“Nimesikiliza hotuba za Rais (Jakaya Kikwete) alikubali kwamba alikosea, tukumbuke Rais wa nchi hawezi akaja akapiga magoti, cheo chake cha rais hakikubali hivyo, akisema alitoa maoni kama mwananchi kile ambacho anasema ni kwamba nisameheni,” alisema huku akishangiliwa na wajumbe ukumbini. Aliongeza kuwa iwapo Watanzania watataka Rais afanye jambo la ziada kuliko hilo alilofanya watashusha hadhi ya kiongozi huyo wa nchi.
Alisema Watanzania walipotunga sheria ya kufanya marekebisho ya katiba walifanya dhambi mbili za asili. Alizitaja dhambi hizo kuwa ni kuruhusu kuyataja baadhi ya mambo kwenye katiba kuwa ni matakatifu na kuvunja tume ya mabadiliko ya katiba.
“Mkiwa mnazungumzia mambo ya katiba hakuna mambo matakatifu yote lazima yazungumziwe. Tanzania siyo nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutafuta katiba ni nchi ya mwisho,” alisema huku akishangiliwa na wajumbe wa kongamano hilo.
Akiizungumzia dhambi ya pili alisema: “Lakini jambo ambalo halieleweki na wengi ni kwa nini Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba (Joseph) iliyokuwa na uzoefu ikavunjwa ? Katika mataifa yote unaihifadhi tume mpaka mwisho.”
Alisema tume hiyo ilitekeleza kazi yake kwa kiwango kikubwa na kwamba hakuna nchi Afrika iliyowahi kukusanya maoni kutoka kwa kila mwananchi.
Akizungumzia namna wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba linaloanza kikao chake cha pili Jumanne mjini Dodoma wanavyotakiwa kufanya kazi zao, alisema siku zote mjumbe ni mtu anayepeleka taarifa mahali fulani kama ilivyo na siyo kuibadilisha.
“Hilo ndilo jambo linalotambulika na mataifa yote na nyinyi Watanzania ndiyo mtakuwa wa kwanza kufikiri tofauti…Tume ya Warioba imefanya mambo yenye ubora yaliyopita viwango vya kimataifa,” alisema huku akishangiliwa kwa makofi na miluzi.
Alisema Ukawa wamefanya vizuri kujiondoa bungeni kwa kuwa walikuwa na sababu zinazoeleweka, lakini kwa kuwa sasa ujumbe wao umefika CCM wanaweza kurudi bungeni.
“Kama umejiondoa pindi ujumbe wako unapoeleweka unarudi bungeni ili upambanishe hoja,” alisema.
Profesa Lumumba alisema wanachama wa TLS wanatakiwa kuchukua hatua ya kufungua kesi mahakamani kuhoji uhalali je, katika kujadili Mamlaka ya Bunge hilo yanaishia wapi.
Jenerali Ulimwengu
Mchambuzi mkongwe wa masuala la kisiasa nchini, Jenerali Ulimwengu alitaja sababu zilizosababisha kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya ikiwa ni pamoja na CCM kutokuwa na nia ya dhati ya kupata katiba hiyo.
Alisema vyama vya upinzani vilidhani vingeweza kutumia mchakato wa Katiba Mpya kuingia Ikulu huku CCM nao wakidhani iwapo katiba ingepatikana wangepoteza madaraka yao.
“Watawala walisema hatuhitaji mabadiliko, hasa mtawala mkuu kuliko wote akasema tutakuwa na katiba mpya. Kwa hiyo tulikuwa mahali ambapo watumishi hawataki tajiri anasema atafanya,” alisema Ulimwengu.
Rais Mstaafu wa TLS, Francis Stolla alisema kufungua kesi ni lazima kuwapo na mlalamikaji lakini wataona ni jinsi gani wataweza kufungua kesi mahakamani ili mahakama itoe ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge hilo.
Naye Mwakilishi wa Chadema, Tundu Lissu alisema mjadala kama huu umechelewa ulitakiwa kufanyika miaka mitatu nyuma ambapo tungejiuliza wapi tunataka kwenda na tunataka kitu gani.
Ukawa watoa msimamo
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeendelea na msimamo wao wa kutorejea bungeni Agosti 5 mwaka huu na nguvu zao wanazielekeza katika vyama vyao kwenda kujipanga ili kuhakikisha harakati za kupigania Katiba Mpya zinafanyika nje ya Bunge.
Pia, Ukawa wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kuwa kigeugeu na awe na msimamo katika jambo hili lenye masilahi mapana kwa kila mwananchi.
Kauli ya Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi inatolewa ikiwa ni siku moja kupita baada ya kuvunjika kwa kikao cha usuluhishi kilichokuwa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi.
Kikao hicho kilichofanyika Hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, kilianza saa 4 asubuhi na kumalizika saa 1.30 usiku kwa Ukawa na CCM kuondoka bila kuafikiana hasa uhalali wa mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba ni yapi.
Jaji Mutungi akizungumza juzi na gazeti hili alisema hatima ya Watanzania kupata Katiba Mpya itategemea busara za viongozi wa vyama vya siasa.
“Ninavyoona mimi, hapa hatima ya Watanzania ya kupata Katiba Mpya itategemeana na busara za viongozi wetu wa vyama vya siasa pekee na si kitu kingine,” alisema Jaji Mutungi.
Wakizungumza jana na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, viongozi wa Ukawa walisema hawatarejea katika Bunge Maalumu la Katiba na wataendelea kuyaheshimu maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
“Ukawa hatuko tayari kuendelea na mazungumzo na CCM wala kurudi katika mkutano wa Bunge Maalumu kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti maoni ya wananchi na kutumia vibaya fedha za umma na kubariki uchakachuaji wa msingi wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume,” alisema Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema.
Aliongeza: “Kila chama kinakwenda kujadili na wanachama wake kupitia Kamati kuu zake kisha tutakutana ili kuona ni hatua gani zingine tuzifuate katika kuipigania Katiba Mpya.”
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi amewapotosha Watanzania na kuendelea kuuvuruga mchakato huo kama alivyofanya wakati akilizindua Bunge Aprili mwaka huu.
“Rais Kikwete alipewa fursa na Tume ya Katiba kutoa maoni yake, lakini alikataa sasa kule bungeni alitoa maoni ya nini wakati alitengewa muda na akaukataa? Na juzi katika hotuba yake ameendelea kusisitiza kuwa alitoa maoni kama mwananchi, anauharibu mchakato huu,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “Rais Kikwete anafanya mchezo kama ingekuwa ngoma ya kikwere angefanya hivyo lakini kwa jambo hili la kitaifa anatakiwa kuwa makini sana.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema katiba mpya itapatikana kwa utashi wa kisiasa na si maridhiano. Naye Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema marekebisho yaliyofanywa na Bunge Maalumu la Katiba Aprili 25 mwaka huu baada ya wajumbe wa Ukawa kutoka yalikuwa ni batili.
“Mabadiliko hayo yaliingiza kanuni mpya ya 32 (6) inayoliruhusu Bunge Maalumu kupendekeza sura mpya kwenye rasimu sasa hii hata tukirudi CCM watataka kuibadili rasimu nzima na kuitupilia mbali Rasimu ya Tume ya Katiba,” alisema Lissu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment