Advertisements

Friday, September 12, 2014

KWA MADEREVA KAMA HAWA TUTAENDELEA KUOMBOLEZWA SAANA TU

                          Stori: Ojuku Abraham
HAKUNA lugha nyingine ya kusema zaidi ya kuainisha kuwa pepo wa ajali za barabarani zinazoua mamia ya watu ni uzembe wa kutisha unaofanywa na madereva katika uendeshaji magari bila utii wa sheria.
Basi la Mtei Express likiovateki wakati kuna magari mawili yanakuja kwa mbele.

Uchunguzi wa Gazeti la Ijumaa uliofanywa hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini umebaini kuwa, mbali na mwendo kasi unaotajwa mara kwa mara kuwa unachangia ajali, suala la kutozingatia sheria za usalama barabarani ni hatari zaidi.

Picha za magari ya abiria yaendayo mikoani zilizotumika ukurasa wa nyuma wa gazeti hili ni kielelezo tosha kuwa madereva wengi hawajui sheria za usalama barabarani au wanazivunja makusudi jambo ambalo husababisha kutokea kwa ajali nyingi za magari kugongana uso kwa uso.
Mabasi manne yakiovateki lori kwa wakati mmoja.

Katika ajali kubwa na mbaya iliyotokea wiki iliyopita mjini Musoma na kuua zaidi ya watu 40, ilitokana na mabasi mawili ya J4 na Mwanza Coach kugongana uso kwa uso katikati ya daraja; kukosa umakini kwa madereva ni chanzo.

Uamuzi wa kizembe kama huo na ule unaonekana katika picha zilizobeba habari hii ambapo madereva wa magari husika wanaonekana ‘kuovateki’ kinyume cha muongozo wa uendeshaji.Sheria zinamkataza dereva kulipita gari jingine kwenye mlima, mteremko mkali na mahali penye kona, lakini kwa mshangao madereva wengi wamekuwa hawazingatii hilo.
Basi likiovateki wakati mbele kuna kona.

“Ukisafiri hasa kwenye barabara kubwa kuna alama zinazokuongoza, lazima dereva uzifuate, lakini madereva wetu hawafanyi hivyo, inawezekana hawajui sheria au wanapuuza kwa sababu adhabu zetu ni nyepesi tofauti na nchi nyingine kama Rwanda,” alisema Mohammed Mpinga, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni.
Hata hivyo, mbali na uvunjifu huo wa sheria, uchunguzi wetu umebaini kwamba madereva wengi wamekuwa wakiendesha magari huku wakiwa wamelewa pombe na hivyo kuwafanya wakose umakini.

Mbali na ulevi baadhi ya madereva wa mabasi yaendayo mkoani wamekuwa wakiendesha kwa mashindano ya kuwahi kufika waendeko ili wasifiwe na abiria kuwa wamewawahisha jambo ambalo mwishowe kuwahi huko huwatokea puani na kuwasababishia ajali.Taarifa ya polisi inaonesha kwamba kwa mwaka jana pekee kulikuwa na ajali 23,842, kati ya hizo ni za mabasi 931, zilizoua watu 313.
Gazeti hili linampongeza Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe kwa hatua anazochukua kuyafungia makampuni ambayo mabasi yake hupata ajali za kizembe na kwamba tunatoa mwito kwa polisi wa usalama barabarani kusimamia sheria ipasavyo ili pepo wa ajali atoweke nchini.
Credit:GPL

No comments: