ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 29, 2014

KWA NINI UNAUMIA JUU YA MTU ANAYE FURAHI?

MTU mmoja mwenye akili aliwahi kusema mapenzi ndiyo kila kitu katika dunia, kwamba mtu anayepata faraja zote kimapenzi ndiye anayeishi vizuri zaidi kuliko hata mamilionea tunaowaona.

Na baadhi ya watu wanafikiri kuishi vizuri kimapenzi maana yake ni kuwa na uhusiano mzuri na mwenza au mke/mume wako nyumbani au yeyote katika uhusiano. Kuishi vizuri kimapenzi, ni pamoja na kuamua kuacha kupenda pia!

Nimewahi kukutana mara nyingi na akina dada (wanaume hawaonekani kusumbuliwa sana na kitendo cha kuachana na wenza wao wa zamani) ambao wamekuwa wakilia juu ya kutendwa na wenza wao wa zamani na kwamba kutokana na hali hiyo, wanajikuta wanajuta na eti, hawataki tena kutendwa!
Ni kweli, kuishi kinyumba na mwenzako ni jambo lenye kuleta furaha katika maisha, lakini wakati tunapolitambua hili, ni vema pia kufahamu kwamba kitu hiki ambacho tunakiona kinatuletea furaha, ndicho cha hatari zaidi pengine kuliko hatari unazoweza kuzifikiria.

Mapenzi yakimuingia mtu, yanaweza kusababisha hata akapata msongo wa mawazo, akajikuta akipoteza uwezo wake wa kufikiri na hata kutenda mambo kwa ajili ya maisha yake. Wapo watu ambao mapenzi yamewafanya waishi kwa kulia na kumlalamikia Mungu kila siku, wakiamini ameamua kuwaumiza pasipo sababu ya msingi.

Hata hivyo, baadhi yetu pengine tunashindwa kutofautisha maana ya mapenzi na uhusiano wa kingono. Wengi hutafsiri uhusiano wa kingono kama mapenzi au kinyume chake. Na wengine hata hudhani kwamba kuishi pamoja kama mke na mume, huenda ndiyo mapenzi baina ya wawili hao.

Kuishi kinyumba kwa mwanamke na mwanamme ni hatua moja kubwa sana katika kujenga mapenzi, ingawa uzoefu unaonyesha kuwa wapo watu wanaojikuta wakijiingiza katika maisha ya kinyumba siyo kwa sababu ya mapenzi, bali kwa kusukumwa na hali halisi ya maisha wakati huo.

Niwe mkweli kwako na wewe uwe mkweli ndani ya nafsi yako, si kila uliyepata kushiriki naye uhusiano ulimpenda kutoka moyoni, yawezekana kabisa ulijikuta hivyo kwa sababu mbalimbali, ili uweze kupata kazi, ili utibiwe, ili urahisishe maisha kimapato au sababu nyingine kadha wa kadha.

Ni kwa sababu hizi, ndiyo maana ninawashauri kuwa makini sana na namna unavyowekeza nguvu yako ya kupenda kwa mtu ambaye huna uhakika na jinsi gani yeye anavyokupenda.

Pia tunatofautiana katika tafsiri ya neno kupenda. Ili uwe salama, ni vyema kumchunguza mwenza wako na kujua jinsi anavyotafsiri kupenda kwake, kwa sababu wengine huamini kuwajibika katika majukumu yake kama mwanaume ndiyo kila kitu, kama anaacha hela ya kula nyumbani hahitaji tena mambo ya kulala katika mkeka na kulishana viazi!

Wapo baadhi ya wanawake wanaoshinda wakijiumiza mioyo yao kwa kuamini kuwa huko waliko wenza wao wanawasaliti. Hali hii huwafanya waishi katika maisha ya kujiumiza bila sababu za msingi. Hisia zao za kusalitiwa huzipa uhai kiasi kwamba hujiona kama watu waliopoteza amani ndani ya mioyo yao.

Niwaambie kitu kimoja. Nani kakuambia ameshikilia amani ya moyo wako? Amani ya moyo wako iko mikononi mwako, kama utakaa na kujitesa juu ya mtu ambaye ana furaha, ni kutojitendea haki wewe mwenyewe.

Nimewahi kuandika mara kadhaa, ni sawa kuwa na wivu kwa mwenza wako, lakini daima kumbuka wivu huo usije kugeuka kuwa shubiri. Unashinda ndani ukiwaza juu ya maisha ya mwenza wako huko aliko kiasi kwamba akija unamchunguza hadi unageuka kuwa kero.

Hebu badilika kuanzia leo, jifanye kama vile uko peke yako. Kama ‘utampotezea’ na kumuondoa kabisa katika fikra zako, mateso yako ya leo yatageuka kuwa historia na huwezi kuamini, mnaweza kujikuta mnaishi vizuri kuliko vile ulivyokuwa unajilizaliza.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

dah yani hii mada kama umeniongelea mimi maana nimekuwa nikiwaza kusalitiwa na kujikuta nalia na kuumia karibu wiki ya tatu hii. wakati mwingine nawaza kuwa single but najipa moyo niwe mvumilivu as mambo nayoyahisi wakati mwingine hayana uhakika ni wivu ndo umenizidi. from today onwards ntaanza kujipenda na kuujali moyo wangu nisije pata ugonjwa wa moyo na presha kisa msongo wa mawazo na maumivu ya moyo. asante kwa mada nzuri.