ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 28, 2014

MWANAMKE,MWANAUME, NANI ANAONGOZA KUTOA SIRI ZA UHUSIANO?


NIJumanne tena, safu hii ya maisha na mapenzi ipo kukuelimisha na kukupa maujuzi ili ikibidi siku moja msomaji wangu ubadilike.

Wiki iliyopita tulimalizia mada yetu ya; Unaachana naye unachukua kila kitu ulichomnunulia. Wiki hii tuna mada nyingine ndiyo hiyo hapo juu; mwanamke na mwanaume katika uhusiano nani anaongoza kwa kutoa siri nje? Au kufanya umbeya.
Nilibahatika kuzungumza na jinsia zote kuhusu mada yetu wakati naiandaa, hoja ilikuwa nusu kwa nusu, yaani ilionekana kama wote tu na si suala la jinsia.

WASEMAVYO WANAWAKE
Nilibaini kuwa baadhi ya watu walizungumza na mimi kwa utetezi huku wakiwa na ukweli mwingine moyoni, lakini pia nilijifunza kitu cha ziada kwamba, kumbe baadhi ya wanawake wenyewe wana majibu ya wazi.

Mama Piliani, mkazi wa Sinza-Palestina jijini Dar, yeye alisema kwa kawaida, mwanamke anamudu kutoa siri za ndani wakati wote, akiwa na furaha na akiwa na hasira lakini mwanaume mara nyingi hufanya hivyo pale anapokuwa na hasira ya jambo fulani.

“Mwanamke akiwa na hasira anamwambia shoga yake; ‘mimi huyu mwanaume wangu nadhani amenishinda sasa. Nikitaka tendo la ndoa anakuwa mvivu, hawezi, sijui nitoke nje, eti unanishauri vipi?’
“Akiwa na furaha atamwambia shoga yake; ‘yaani mwanaume wangu nampenda sana, kitandani yuko vizuri, ukikutana naye leo, unaweza kukaa hata wiki maana anakuwa amekata kiu yote.’

WANAUME WAO
Utafiti nilioufanya nilibaini kuwa, wanaume wengi hutoa sira za uhusiano pale tu wanapohitaji ushauri wa masuala magumu yanayowatokea. Lakini pia wapo baadhi ya wanaume nao wanapenda sana ‘ubuyu’ hivyo huanika siri zao za uhusiano bila kutaka ushauri.

ETI NI TIBA
“Mimi siwezi kumficha rafiki yangu kipenzi kuhusu magumu yanayonitokea ndani ya uhusiano. Unajua kusema pia ni tiba tosha. Kama wewe huna tabia ya kuficha mambo magumu unaweza kuja kufa kwa presha,” alisema Tamimu, mkazi wa Tandale Kwatumbo, Dar.
Kauli ya Tamimu iliungwa mkono na mkewe aliyekuwa naye kwenye Kituo cha Daladala cha Kwaremi, Dar wakisubiri usafiri.

Mke huyo alisema: “Unajua hata mtoto, akitendewa ubaya asipolia anapata tabu sana, lakini akilia anakuwa sawa. Ndiyo umbeya pia, kama una magumu katika uhusiano halafu huwaambii wenzako utapata tabu, watu watakushangaa kukuona unakonda tu, lakini ukisema unapata nafuu.”
Kuhusu kutoa sifa ya mambo mema, mke huyo alisema: “Huo sasa ni uendawazimu. Unamwambia shoga yako kuhusu mumeo anavyokutosheleza kitandani si ndiyo mwanzo wa kuibiwa!”

KITABIA
Kwa mujibu wa wataalam wa mambo ya tabia za binadamu, mwanamke kwa siku anazungumza maneno 20,000 na kumzidi mwanaume kwa maneno 13,000. Ina maana mwanaume anazungumza maneno 7,000 tu kwa siku!

Wataalam hao wanatanabaisha kwamba, tabia hiyo ndiyo inayomfanya mwanamke kuongoza katika kutoa siri za uhusiano kuliko mwanaume kwa vile wanaongea sana.

Wataalam hao wanakwenda mbele zaidi kwa kusema, umbeya au kutoa siri za uhusiano kwa mwanamke ni jambo la asili ndiyo maana watoto wa kike huanza kutangulia kuongea kuliko wa kiume ambaye yeye huwa mwepesi kwenye kuanza kutembea.

Baadhi ya wanawake wanalijua hilo ndiyo maana unaweza kumsikia mwanamke akisema: “We mwanaume mzima unakuwa mbeya kama mwanamke bwana.”Kuthibitisha hilo, vuta kumbukumbu kama kuna siku ulikuta ugomvi kati ya mwanamke na mwanaume, nani alishindwa kwa sababu ya kusema sana, lazima mwanaume alishindwa!

MADHARA
Si vibaya kwa mtu kuanika mabaya anayokumbana nayo kwenye uhusiano lakini ni vyema kufaya hivyo kwa nia ya kusaka suluhu na si kumsema mwenzako kwa lengo la kumwanika, madhara yake marafiki unaowaambia nao watawaambia wengine na wengine, na mwenzio atakuwa mtu wa kudharauliwa kwa sababu udhaifu wake utajulikana.

Ni vyema kama mwenzako katika uhusiano ana udhaifu, umsitiri kwani wewe ndiyo mwenzake. Kama udhaifu wake ni wenye kukera na kutokuvumilika nenda kwa viongozi wa dini au wazazi ili suala liwe ni shauri lenye kutatuliwa kwa hekima.
GPL

2 comments:

Anonymous said...

Wanaume wa kitanzania mwisho wanaongea hata kama hawa jaulizwa. Na wavulia kofia. Hapa DMV

Anonymous said...

story za kijiweni hizi sasa utafiti huu umefanywa na nani na umepimwa kiwango gani.namuuga mkono hapo juu mdau mwanamama . si dmv peke yake ni kote ulimwenguni siku hizi wanaume wa kitanzania wanaonge kama upatuu bila hata kuulizwa tena siku hizi afadhali hata mademu kuliko mijemba hii.
mwanamme aliyelelewa vizuri kwao na kuiva na demu aliye lelewa vizuri kwao na kuiva kwa malezi hawezi akawa na taabia hizi za ajabu ajabu kutoa siri za ndani nje ya nyumba.

wanaotoa siri za ndani nje ya nyumba wasio ivaa kimalezi.Tabia njema huanzia kwenu ulikolelewa .

chagueni wanaume wenye tabia njema na wake wenye tabia njema uzuri baadaye.

huna tabia njema unaachiwa miyooo tuu.