Dar es Salaam. Vyama vya upinzani vimeandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya vyama vinne vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutiliana saini makubaliano saba ya ushirikiano, kubwa ikiwa kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia sasa.
Tukio hilo lilifanywa na viongozi wakuu wa NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD jana katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi wa dini na taasisi mbalimbali.
Akisoma makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alianza kwa kueleza historia ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilitengenezwa kwa muundo wa chama kimoja cha siasa (CCM)... “ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi.
Mwaka 2011 tulianza mchakato wa kuandika Katiba Mpya, ilipatikana Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi lakini maoni hayo yameondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.”
Alisema kitendo cha kuachwa kwa maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, kimesababisha athari katika matukio muhimu ya kidemokrasia.
Akitaja makubaliano hayo, saba aliyosema yana lengo la kuzaa Tanzania Mpya, Dk Slaa alisema, “Jambo la kwanza ni kuhusisha sera za vyama vyetu na kuchukua yale yote yanayofanana ili tumwe na kauli zinazolingana na kufanana kwa Watanzania.”
Alisema jambo la pili ni kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye ngazi zote za uchaguzi kuanzia Serikali za Mitaa, madiwani, wabunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Tatu, alisema utaratibu wa namna gani vyama vinavyounda Ukawa vitashirikiana katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015, utatolewa na vyama hivyo katika wakati muafaka na kusambazwa kwa viongozi wa vyama hivyo wa ngazi zote ili waweze kuutumia kama mwongozo na kufanyia kazi.
Nne, kushirikiana katika mchakato wa kuelimisha umma kuifahamu na kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa ambayo haijazingatia maoni ya wananchi badala yake imezingatia masilahi ya kikundi kimoja cha watu ambacho ni CCM.
Tano, kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za kitaifa na zenye masilahi kwa Watanzania.
Sita, kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya masilahi kama ilivyo sasa na kama inavyojidhihirisha katika Katiba Inayopendekezwa.
Saba, “kuhimiza na kusimamia ushirikiano wa pamoja baina yetu na asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania yenye nia ya dhati ya kulinda na kuenzi Muungano wetu bila kunyenyekea masilahi binafsi ya kikundi, kabila au itikadi.”
Dk Slaa alisema kwa uamuzi huo wa Ukawa ni wazi kuwa Watanzania watawaunga mkono huku akiwataka wajiandae kuwa na Tanzania Mpya.
Maalim Seif
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alisema msimamo wa Ukawa ni msimamo wa Watanganyika na Wazanzibari, huku akiwataka wananchi kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa na kuifananisha na takataka.
“Wamepiga kura kupitisha Katiba peke yao, wakaikubali peke yao, wakaitangaza peke yao. Eti wameikabidhi Katiba kwa Rais (Jakaya) Kikwete na Rais wa Zanzibar, sijui hawa viongozi wameikubali vipi hii Katiba, hakuna kitu pale,” alisema huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Maalim Seif alisema theluthi mbili kutoka Zanzibar haikupatikana na Bunge hilo lilitumia ujanja wa kuongeza idadi ya wajumbe wawili kutoka Zanzibar, ambao hawakutakiwa kupiga kura kupitia upande huo wa Muungano.
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Ukawa ina msingi wa uadilifu, uwazi na uwajibikaji na ndiyo kiboko ya kupambana na CCM. Kama mnataka rasilimali za nchi yenu kataeni Katiba Inayopendekezwa. Adui wa nchi hii ni mafisadi ndani ya CCM, lazima tuwe na mtandao wa mabadiliko nchi nzima. Vijana tufanye mazoezi ya viungo kwa ajili ya kupambana na mafisadi hawa.”
Aliwataka wananchi kuhakikisha kuwa wanajisajili katika daftari la Serikali za Mitaa ili kuwachagua viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa... “Naanza kuona mwanga wa kuiondoa CCM madarakani. Tujenge ushirikiano kwa ajili ya nchi yetu.”
Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Yaliyotokea leo siyo mapenzi ya Lipumba, Mbowe, Mbatia, Makaidi wala Nyambabe, bali ni mapenzi ya Mungu. Kama kuna mmoja wetu aliyepo hapa anayeshuhudia tukio hili huku amenuna … dhoruba limtokee.”
Huku akishangiliwa na umati wa wafuasi wa Ukawa, Mbowe alisema ni mategemeo yake kuwa viongozi wote waliotia saini makubaliano hayo, walizungumza kutoka rohoni kwamba wanaungana na wana nia moja.
Aliwataka viongozi wa chama chake katika ngazi zote, kuhakikisha wanakubaliana na mapendekezo yanayotolewa na Ukawa na kwamba yeyote anayeona hataweza aondoke mapema.
“Katika chama chetu hakuna masilahi ya maana kuliko nchi yetu. Ni marufuku kiongozi wa Chadema kupuuza muungano wa Ukawa na kama yupo mwenye masilahi binafsi aanze safari mara moja,” alisema Mbowe.
Aliwaagiza viongozi wa taasisi zote za Chadema, Bawacha, Bavicha na Baraza la Wazee, kuhakikisha wanafanya kampeni za kuipinga Katiba Inayopendekezwa nchi nzima kuanzia Novemba Mosi. Aidha, aliwaomba viongozi wa Ukawa kuhamasisha viongozi wao kuipinga Katiba Inayopendekezwa.
Mbatia
Mbatia alisema Taifa limeandika historia mpya na kuwaomba viongozi wenzake ndani ya Ukawa kuaminiana ili Watanzania nao wawaamini kwa kuwa wanataka kuweka mbele masilahi ya taifa.
Kuhusu Katiba, Mbatia alisema ni maarifa, mwongozo na inayounda dola hivyo asiwepo wa kuifanyia mchezo. Alitaka Katiba Inayopendekezwa ikataliwe na wananchi kwa kuwa haisadifu sifa hizo.
“Ukawa wana utulivu wa ndani wa kuwatumikia Watanzania wote… tuache kuangalia masilahi binafsi. Wakishinda Chadema… mimi nikubali, akishinda CUF lazima nikubali, hata wakishinda NLD nao nitakubali lakini na NCCR tukishinda nao waone tumeshinda kusiwepo na kinyongo kwa kuwa wote tunapigania mama Tanzania,” alisema.
Makaidi
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema umoja wa wananchi ndiyo utakaowapa nguvu viongozi wa Ukawa na kuongeza kuwa anaipenda Tanzania na anataka Zanzibar iwe na mamlaka kamili.
“Mungu siyo Athuman wala siyo wa John… Mungu alijua kupitia misukosuko hii ya Katiba, Ukawa tutaunganishwa. Bahati hii inaweza isitokee tena, wakati wa ukombozi ni sasa na utakapofika wakati wa kupigia kura ya maoni tuseme hapana, hapana, hapana na moto… moto mpaka CCM iungue,” alisema Dk Makaidi huku akishangiliwa kwa nguvu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment