ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 22, 2014

WEWE SIYO MZURI? NANI KAKUDANGANYA!

BINADAMU tumeumbwa kwa namna tofauti sana, ingawa kibaolojia, wote tuko sawa, bila kujali kama ni Wahindi, Waarabu, Wazungu, Waafrika, Wachina na makabila yote, siyo warefu, wafupi, wembamba wala wanene.

Tunatofautiana akili, uwezo wa kuelewa, uwezo wa kukabili changamoto na hata jinsi ya kuishi kwenye jamii inayotuzunguka. Kuna watu wengine hawaamini kama wao wako vile walivyo kwa sababu yao wenyewe, bali wanamsingizia Mungu.

Mungu alituumba wote tukiwa na akili, kinachotokea ni kujiongeza tu, kwa elimu ya darasani na hata ya mtaani, lakini ukifunua kichwa changu, utakuta kina kila kitu ambacho kipo kichwani mwa Steve Jobs, yule bilionea namba mbili duniani.

Ndivyo pia tulivyo hata katika maisha ya uswahilini. Unashangaa watoto wawili wa kiume wamezaliwa kwa wazazi walewale, lakini staili ya maisha yao ni tofauti kabisa, mmoja ni mpole na mtanashati, mwingine ni mtukutu asiyekamatika.

Kuna wengine kutokana na hali ya maisha yao, wanaamini kwamba wao ni wabaya kiasi kwamba hawawezi kupata wenza wenye maana. Hivi, hebu jaribu kufanya utafiti wako mwenyewe mdogo. Mchukulie msichana mwenye sura ya kawaida tu lakini anayeishi katika familia bora anavyokuwa.
Atatumia uwezo wa wazazi wake kufanya shopping ya maana na atajiremba sana kiasi kwamba ataonekana ni mrembo kuliko msichana kutoka familia iliyochoka ambaye ana uzuri wa asili, lakini uwezo wake duni kifedha, unamfanya ashindwe kujifanyia manjonjo.

Vivyo hivyo kwa wavulana, wapo wenye miili iliyopendwa na akina dada, lakini kutokana na ufukara wao, wanashindwa kujitokeza mbele ya wasichana wazuri kwa sababu hawawezi kusikilizwa, hasa katika kipindi hiki ambacho ni cha hapendwi mtu isipokuwa pochi.

Lakini mvulana mwenye sura isiyovutia, aliyetoka familia bora atavaa mavazi ya gharama yatakayomfanya aonekane handsome na wadada watamkimbilia, naye hakika atajiona ni mzuri.
Kitu tunachoweza kujifunza kutokana na hali hii ni kwamba siku hizi mapenzi hayaangalii sana wajihi wa mtu, bali hali yake.

Upande wowote ambao fedha inahusika, ndiyo ambao una nafasi kubwa ya kupata mapenzi yenye uhakika, wakati upande wa pili kidogo hali huwa siyo rahisi. Hapa ndipo baadhi yetu tunapokosa ujasiri hadi kujikuta tunakimbilia kwa binadamu wenzetu, tuliowapa jina la waganga na kuamini kuwa wanaweza kutusaidia kuwapata wenza!

Wapo ambao maisha yao ya kimapenzi yamewafanya wajione kama wenye mikosi, wamejikuta wakiamini kwamba wao ni wabaya na kwamba hawana bahati. Kama wewe ni mmoja wa watu hawa, safu hii ya leo itakuwa ni nzuri sana kwako.

Wapo baadhi ya ndugu zangu, wake kwa waume wamekuwa wakinipigia simu na kunieleza jinsi maisha yao ya kimapenzi yalivyotawaliwa na kile wanachosema kuwa ni mikosi, kwamba kila baada ya muda mfupi, wapenzi wao ama wanageuza njia au lolote ambalo huliweka penzi lao katika hali ya sintofahamu.
Kwanza ni lazima tufahamu kwamba katika mapenzi, hakunaga mtu mzuri wala mbaya.

Wengine wanajidanganya kwamba wao ni warembo kuliko wenzao. Hapana, mapenzi ni hisia. Kila mtu ana hisia na kwa maana hiyo, yeyote anaweza kumpata mwenza. Kinachotufanya tujione kuwa na mikosi ni kwamba achilia mbali matatizo yetu ya kibinadamu, lakini pia huenda wenza tunaowachagua, hawana hisia kwetu. Usidhani urembo wa sura na umbo ni kitu pekee kinachoweza kumfanya mtu avutiwe na wewe. Ni zaidi ya hapo.

Ndiyo maana hushangai kwa nini wenzetu wenye ulemavu, uwe wa viungo au ngozi, mbona na wenyewe wana watu wao? Kama mapenzi yangekuwa siyo hisia, hawa wasingepata wenzao kwa sababu watu wangeogopa ulemavu wao.

Kuna watu wana magonjwa yao, mtu mwingine anapenda matiti makubwa au madogo, akimuona mwanamke aliyenayo, hajali, hata kama hana miguu!

Ndiyo maana nimekwambia, acha kujiona mwenye mikosi, isipokuwa tambua bado hujampata mtu ambaye anaendana na wewe kwa hisia. Ni kujidanganya kumtafuta kwa waganga wa kienyeji!

GPL

No comments: