Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Ujumbe wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) upo nchini kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo, imefahamika.
Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema jana kuwa waamuzi waliosimamishwa na TFF pamoja na watu wengine watahojiwa na ujumbe huo. Matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa na FIFA baada ya shughuli hiyo kukamilika.
"Tunaendelea kuwahimiza wanafamilia wa mpira wa miguu wazidi kuzingatia kanuni za maadili za TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA katika utendaji wao. FIFA itahakikisha kuwa haki inatendeka katika uchunguzi ambao inaufanya.
WASIMAMIZI WA SIRI FDL
Aidha, Wambura alisema TFF itatuma waangalizi wa siri kwenye mechi za raundi ya 21 na 22 ambazo ni za mwisho kwa makundi yote ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakazoanza kuchezwa Februari 10 mwaka huu.
Mwangalizi huyo (match assessor) atatumwa na Katibu Mkuu na baada ya mechi atatuma ripoti kwake kwa hatua zaidi.
Mechi za raundi ya 21 kundi A zitachezwa Februari 10 mwaka huu kati ya KMC dhidi ya African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani), Kurugenzi FC dhidi ya African Sports (Uwanja wa Mufindi), Majimaji dhidi ya JKT Mlale (Uwanja wa Majimaji), Kimondo FC dhidi ya Friends Rangers (CCM Vwawa, Mbozi), Ashanti United dhidi ya Villa Squad (Uwanja wa Karume) na Polisi Dar dhidi ya Lipuli FC (Azam Complex).
Raundi ya 22 itachezwa Februari 16 mwaka huu kwa kuzikutanisha African Lyon na Polisi Dar (Uwanja wa Karume), Kurugenzi dhidi ya Lipuli FC (Uwanja wa Mufindi), Kimondo FC dhidi ya Majimaji (CCM Vwawa, Mbozi), JKT Mlale dhidi ya Ashanti United (Uwanja wa Majimaji), Friends Rangers dhidi ya African Sports (Uwanja wa Taifa), na Villa Squad dhidi ya KMC (Azam Complex).
Kundi B raundi ya 21 ni Februari 17 mwaka huu kati ya Burkina Faso dhidi ya JKT Kanembwa (Uwanja wa Jamhuri), Mwadui dhidi ya Polisi Tabora (Uwanja wa Mwadui), Polisi Dodoma dhidi ya Green Warriors (Uwanja wa Jamhuri), Rhino Rangers dhidi ya JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Panone dhidi ya Polisi Mara (Uwanja wa Ushirika), Geita Gold dhidi ya Toto Africans FC (Geita).
Februari 22 mwaka huu ni JKT Kanembwa dhidi ya Green Warriors (Lake Tanganyika), Mwadui dhidi ya Burkina Faso (Mwadui), Polisi Tabora dhidi ya JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma dhidi ya Panone (Uwanja wa Jamhuri), Toto Africans dhidi ya Rhino Rangers (CCM Kirumba) na Geita Gold dhidi ya Polisi Mara (Geita).
Mechi za viporo za Polisi Mara zitachezwa Februri Mosi dhidi ya JKT Kanembwa, na Februari 5 mwaka huu dhidi ya Polisi Tabora. Mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.
MGOGORO WA ZFA KORTINI
Katika hatua nyingine, Wambura alisema TFF imepokea kwa masikitiko taarifa za kuwapo tena kortini kwa kesi dhidi ya uongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), jambo ambalo linaweza kuathiri ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye Ligi ya Klabu Afrika na Kombe la Shirikisho.
Mwishoni mwa mwaka jana, TFF ilihadharisha juu ya masuala ya mpira wa miguu kupelekwa mahakamani, kwani kwa mujibu wa FIFA, kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.
Alisema kutokana na hali hiyo, TFF iliiandikia barua ZFA kutaka mgogoro huo uondolewe kortini na yenyewe kuridhia kuwa tayari kupeleka ujumbe Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika.
Alisema TFF pia ilisema timu za Tanzania Bara zisingeruhusiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 iwapo kesi hiyo ingeendelea kuwapo kortini na kutaka iondolewe bila masharti yoyote.
ZFA iliithibitishia TFF kuwa kesi hiyo imeondolewa kortini bila masharti, hivyo timu za Tanzania Bara kuruhusiwa kushiriki katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
"Ni muhimu suala hilo likashughulikiwa haraka ili kutohatarisha ushiriki wa timu za KMKM na Polisi kwenye michuano hiyo ya CAF," alisema Wambura.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment