Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akisema kuwa wamekaidi ushauri wa kitaalam uliowazuia wasitumie mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR) katika uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mbowe amedai kuwa baada ya kuona zoezi la kuandikisha wapiga kura haliendi kama ilivyotakiwa, NEC walimtafuta mshauri mwelekezi aitwae Darrell Geusz, mtaalam wa masuala ya BVR kutoka Marekani ambaye baada ya kufanyia utafiti ‘hali’ ya Tanzania kuhusu mfumo huo mpya, aliwaambia wakilazimisha wanaweza kusababisha machafuko ya kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa Mbowe, mtaalam huyo katika ripoti yake aliyoitoa mwezi Januari mwaka huu, aliiambia NEC kuwa kwa sasa Tanzania haiwezi kuandikisha wapiga kura kwa mfumo wa BVR kwa sababu ya ukosefu wa fedha, vifaa, utaalam na muda kwani mfumo huo ili uweze kufanya kazi inayotakiwa unahitaji maandalizi ya takriban mwaka mmoja.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ameyasema hayo jijini Mbeya wakati alipohutubia matukio mawili tofauti, akiwa katika ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Kanda (ya CHADEMA) ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma na Rukwa.
Mapema asubuhi Mwenyekiti Mbowe alihutubia wakati akifungua kikao cha Baraza la Uongozi wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kisha baadae jioni akahutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Dk. Slaa mjini Mbeya. “Mshauri huyo mwelekezi ambaye ni mtaalam wa masuala ya BVR kutoka Marekani, amewahi kuisaidia nchi ya Bangladesh ambako waliandikisha wapiga kura milioni 80, aliwaambia NEC kuwa Tanzania hatuwezi kuendesha hili zoezi kwa sasa, hatuna vifaa, hatuna wataalam, hakuna muda wa kutosha, hatuna wataalam, hatuna maandalizi, akawatahadharisha wakilazimisha wanaweza kusababisha machafuko.
“Lakini katika hali ambayo haijulikani, wakiendeleza ukaidi kwa ajili ya kutaka kuibeba CCM, NEC inaonekana kutaka kuendesha zoezi hili bila kuzingatia ushauri wowote wa kitaalam wala kushirikisha wadau ambao ni vyama vya siasa wala haitaki kutoa taarifa za kutosha kwa wananchi ambao ndiyo wapiga kura wenyewe. “NEC imekuwa ikiendesha suala hili kwa usiri usiri sana, taarifa zao wanapoamua kutoa zimekuwa za kusua sua sana, kwa kushtukiza. Tumekuwa tukidai ushirikishwaji wa kina wa shughuli na mfumo huu bila mafanikio. Tumeomba sana kupata nyaraka ili tuelewe, lakini hawataki. Wanafanya siri kubwa.
“Sasa nasi kwa sababu tunazo njia mbalimbali za kupata taarifa, tumezipata nyaraka ambazo hawataki wadau kwa maana ya vyama vya siasa tuzione. Kwanza tumepata nyaraka ambayo inaonesha kuwa wakati walikuwa wanasema hawana kitu cha kutupatia ili tuelewe mfumo huu wa BVR, wao labda na CCM yao tangu 2013 walikuwa tayari wanajua kitakachofanyika. “Lakini pia tumefanikiwa kupata nyaraka nyingine hii hapa. Hawa jamaa wa NEC baada ya kuzidiwa wakaamua kutafuta mshauri mtaalam kutoka Marekani ambaye anasifika duniani, yaani katika masuala ya BVR ni authority, ameandika ripoti yake yenye kurasa 16, amewapatia hadi ushauri wa tahadhari ya madhara ya kiusalama jamaa wa NEC na Serikali ya CCM hawataki kusikia,” amesema Mbowe.
Mbowe ameongeza kusema kuwa wakati mshauri huyo mtaalam wa BVR akiwatahadharisha NEC kuhusu muda, tume imeendelea kusema kuwa zoezi hilo litafanyika na kufanikiwa kwa kipindi cha ndani ya miezi miwili, jambo ambalo Mwenyekiti wa CHADEMA amesema kuwa serikali inacheza na ‘roho ya amani katika nchi’. Alisema kuwa mazingira yanayoendelea nchini Tanzania katika suala la mchakato wa hatua mbalimbali za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yanatengeneza hali ya kutokuaminiana miongoni mwa wadau, akisema kuwa hali hii husababisha uchakachuaji na katika nchi zingine imesababisha machafuko ya kisiasa.
NEC na ubabaishaji katika ratiba
Mbowe amesema kuwa tangu mwaka jana NEC imekuwa ikitoa taarifa za kukanganya kuhusu ratiba kamili ya kuanza kuandikisha upya wapiga kura nchi nzima, ambapo iliwahi kusema shughuli hiyo ingeanza Septemba 2014, baadae ikaahirisha hadi Desemba, lakini pia haukufanyika, kisha baadae ikatoa ratiba ya kuanza kazi hiyo Februari 16 mwaka huu, ikianza na mikoa minne ya Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara. Kiongozi huyo amesema kuwa baada ya vyama vya siasa kuibana NEC juu ya ratiba na maandalizi muhimu kuhusu shughuli hiyo huku muda ukikaribia, tume ikawaita wadau na kuwaambia kuwa zoezi limesogezwa mbele ili kuvipatia vyama vya siasa muda wa kuandaa mawakala, hivyo litaanza Februari 23, mkoa mmoja pekee wa Njombe badala ya mikoa minne kama ilivyotangazwa awali.
“Tukawaambia mnasema tuwaandae mawakala wetu, tuwaandae kuhusu kufanya majukumu yapi hasa na hamtaki kutupatia nyaraka, bado wakaendelea kutoelewa. Tukawaomba hata ratiba ya mkoa huo mmoja bado hawakuweza kutupatia. Yaani ni ubabaishaji tu. Sisi tukaamua kupeleka watu wetu huko mkoa mzima kuanza maandalizi. Tayari tunavyozungumza tuna watu wako field. “Katika hali ya kushangaza sana, jana tukapokea ratiba yao, wakaongeza maajabu mengine tena. Ratiba yao inaonesha kuwa hata mkoa mmoja wa Njombe pekee wameshindwa kuandikisha mkoa mzima badala yake wataanza na jimbo moja tu la Njombe Kaskazini. Katika jimbo hilo pia hawawezi kuandikisha kata zote kwa wakati mmoja badala yake wataanza na kata mji mdogo wa Makambako.
“Yaani wameshindwa mikoa minne, wakaamua mkoa mmoja, mkoa mmoja hawawezi kuandikisha wilaya zote, hata wilaya moja wameshindwa, wataanza na jimbo moja na katika jimbo hilo wataandikisha kata 12, sio zote kwa pamoja wataanza na kata 9 za mji mdogo wa Makambako, kisha zitafuata kata zingine. Hii ni aibu ya hatari,” amesema Mbowe na kuongeza;
“Yaani wakati mamilioni ya Watanzania wanasubiri kuandikishwa nchi nzima, NEC haiwezi hata kuandikisha wilaya moja kwa wakati mmoja. Halafu eti wameniandikia barua ya mwaliko kwenda Makambako kushiriki hafla ya uzinduzi utakaofanywa na Waziri Mkuu Pinda siku ya Jumanne ijayo, nawauliza viongozi wenzangu niende nisiende.
“Kwa sababu kwenda kwenye uzinduzi huo wa NEC utakaofanywa na Waziri Mkuu ni kubariki uhuni wote huu wanaoufanya.”
Serikali kufilisika, ukosefu wa vifaa vya BVR na kuchezea Sheria
Mwenyekiti Mbowe ameshusha tuhuma nzito kwa Serikali ya CCM akisema kuwa kushindwa kupatikana kwa vifaa vya BVR kwa muda unaotakiwa ili wananchi waanze kuandikishwa kunatokana na serikali hiyo kufilisika, kukosa vipaumbele, kuendekeza ufisadi na matumizi ya anasa huku pia ikilifanya zoezi la uchaguzi kuwa ni tukio la dharura badala ya mchakato wenye maelekezo ya kikatiba. Alisema kuwa kugeuza uchaguzi kuwa tukio la dharura badala ya takwa la kidemokrasia lenye masharti ya kisheria ni kucheza na haki na matumaini ya Watanzania jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani ya nchi. “Ili kuandikisha wapiga kura nchi nzima, NEC ilihitaji vifaa…wanaviita BVR kits vipatavyo 15,000 lakini Serikali ya CCM ikawaambia hapana wapunguze, wakapunguza hadi 8,000, katika hivyo 8,000 hadi sasa vipo 250 pekee tangu wakati wa uandikishaji wa majaribio. Hadi sasa vingine havijafika kwa sababu serikali haijalipia, haijalipa kwa sababu imefilisika.
“Pamoja na mazonge haya yote, juzi nimemsikia Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva akisema daftari hili hili watakaloandikisha litatumika kwenye Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, huyu mzee tunamheshimu sana lakini wamempatia kazi itakayoondoa heshima yake. Huyu ni mwanasheria, Jaji mstaafu. Sitaki kuamini kuwa hajui kuwa kuhakiki daftari kabla halijaanza kutumika ni hitaji la kisheria.
“Sheria inaagiza kwamba baada ya uandikishaji lazima wapiga kura wahakiki daftari lao kisha sasa ndipo tunapata daftari la kudumu la wapiga kura. Sasa kwa ratiba yao wanamaliza kuandikisha Aprili 29 na kesho yake Aprili 30 kura ya maoni inapaswa kupigwa, sasa sijui anataka kutumabia nini. “Pamoja na kwamba sisi kama CHADEMA pamoja na wanachama wenzetu wa UKAWA tumewaomba Watanzania kutoshiriki kupiga kura ya maoni ya katiba ili wasitumike kuhalalisha mchakato haramu, lakini hatutakubali sheria ziendelee kuvunjwa tu waziwazi na akina Lubuva kwa sababu ya maelekezo ya ikulu huku NEC ikitumika tu kama kanyaboya,” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa serikali nyingi duniani hukaribisha machafuko na anguko lake kila zinapoanza kuchezea chaguzi mbalimbali. Alisema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ulijulikana miaka 5 iliyopita kikatiba hivyo maandalizi yake hayawezi kuwa ya zimamoto au dharura. Alisema sheria ya uchaguzi inaelekeza wazi kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linapaswa kuboreshwa mara mbili katikati ya uchaguzi mmoja hadi mwingine, lakini hata takwa hilo la kisheria pia limevunjwa na NEC ambayo imeshindwa kuboresha tangu ilipoandikisha mwaka 2010.
Alisema kuwa serikali inayojua wajibu wake kwa wananchi, ilipaswa kujua vipaumbele vya mwaka huu, ikitambua kuwa kuweka mambo makubwa matatu ndani ya mwaka mmoja, yaani; uandikishaji wapiga kura, kura ya maoni ya katiba mpya na uchaguzi mkuu, ni mambo ambayo haiwezi kumudu kuyatekeleza ndani ya muda mfupi, bila kuwa na fedha.
“Yaani wakati Watanzania wenye sifa wakisubiri nchi nzima, taifa zima linasubiri, katika sintofahamu hii, bado viongozi wetu wanathubutu kudanganya kuwa kura ya maoni itafanyika, huku Waziri Mkuu Pinda akienda kubariki mchezo huu keshokutwa huko Makambako. Hatujui wanapata wapi ujasiri huu wa kuwadanganya Watanzania,”amesema Mbowe.
1 comment:
LONG LIVE FREEMAN MBOWE
Post a Comment