Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akionyesha jeraha la Naibu mkurugenzi wa mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Kambaya alijeruhiwa na polisi wakati wa maandamano Jumanne iliyopita. Picha na Salim Shao
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema anatarajia kwenda Ikulu kumwona Rais Jakaya Kikwete ili kumweleza mambo mbalimbali ikiwamo ubabe na upendeleo unaofanywa na polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Profesa Lipumba alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikifanya mikutano bila ya kubughudhiwa na polisi tofauti na inavyofanyiwa CUF.
“Kinana anafanya mikutano kila siku lakini hatujawahi kuona akibughudhiwa na polisi lakini chama chetu kimekuwa kikiambulia mabomu ya machozi, vipigo na kuzuia mikutano yetu, Rais inabidi aingilie kati hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika uchaguzi mkuu,” alisema.
Profesa Lipumba alisema huko ni kuleta mgawanyiko unaoweza kusababisha machafuko kama hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Jumanne iliyopita, Jeshi la Polisi lilizuia maandamano na mkutano wa chama hicho uliokuwa ufanyike kuadhimisha miaka 14 ya mauaji ya wenzao yaliyotokea Zanzibar Februari 26 na 27, 2001.
Katika tukio hilo, Profesa Lipumba na wafuasi 32 walikamatwa na baadaye kufunguliwa mashtaka mahakamani ya kula njama, kufanya maandamano na kukusanyika bila kibali. Vitendo hivyo vya polisi vilisababisha Bunge la Jamhuri ya Muungano kusitisha shughuli zake na kujadili tukio hilo bila kujali kwamba lilikuwa linaingilia mhimili mwingine wa nchi.
Jana, Profesa Lipumba alisema: “Nataka kuonana na Rais Kikwete ana kwa ana, siwezi kumwandikia barua kwa sababu nafahamu hana muda wa kusoma, hivi sasa nafanya kila juhudi ili kumwona.”
Profesa Lipumba alisema Januari 22, mwaka huu chama chake kilipeleka barua ya kufanya maandamano na mkutano kwenye Uwanja wa Zakhem, Mbagala wilayani Temeke na kiliwatangazia wananchi kwamba maandamano na mkutano huo vingefanyia Januari 27 kuanzia saa 8.00 mchana na maandamano yangeanzia Temeke Mwisho hadi katika uwanja huo.
Alisema Januari 26, saa 12.00 jioni ikiwa imebaki siku moja, ndipo Jeshi la Polisi likatoa amri ya kupinga kufanyika kwa maandamano hayo na mkutano.
“Tulishawatangazia wananchi kuhusu maandamano hayo na mkutano, usiku huo tungewajulisha vipi kufuta mkutano huo, kwa nini hawakutujulisha mapema? Matatizo kama hayo yanasababishwa na Jeshi la Polisi,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema wakati wakisaini makubaliano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kati ya CCM na CUF Zanzibar, alipopewa nafasi ya kuzungumza alisema: “Tusameheane kwa mauaji yaliyotokea Zanzibar lakini tusiyasahau kwa sababu tukifanya hivyo yanaweza kujirudia.”
Alisema ndiyo maana kila mwaka, wamekuwa wakifanya kumbukumbu za mauaji hayo ili yasirudie tena.
Akizungumzia waliojeruhiwa na polisi, mwenyekiti huyo alisema maofisa wake wawili walijeruhiwa kwa vyuma na kuwasababishia maumivu makali.
Hata hivyo, Profesa Lipumba aliwataka wananchi kutolipiza kisasi licha ya wengi wao kusikitishwa na vitendo hivyo.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment