Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akizungumza na mwenzake Rais wa Misri, Jenerali Abdel Fatteh El Sisi siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amekabidhi madaraka ya Uratibu wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika ya Mazingira (CAHOSCC) kwa Rais wa Misri, Jenerali Abdel Fatteh El Sisi.
Rais Kikwete alibeba jukumu la uratibu wa CAHOSCC miaka miwili iliyopita baada ya kifo cha aliyekuwa mratibu wa kamati hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais Kikwete alikabidhi jukumu hilo Januari 31 na kuwatahadharisha viongozi wa Afrika juu ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye sekta ya kilimo barani Afrika.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kikwete aliwapongeza viongozi wengine wa Afrika wakati wa mkutano wa 24 wa Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, kwa kupata mafanikio wakati wa uongozi wake.
Kikwete alibainisha changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi na kutaka ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea ambao ndiyo wachafuzi wakubwa wa mazingira na nchi zinazoendelea kutoka Afrika.
Rais alizitaka nchi za Afrika ambazo zinaathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kuongeza kasi katika kuzibana nchi tajiri ili zikubali kuchangia kwa kiasi kikubwa rasilimali za kubabiliana na athari hizo kwa sababu zinachangia asilimia 97 ya uchafuzi wa mazingira.
“Wao wanachangia asilimia 97 kuchafua mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi, sisi tunachangia asilimia tatu. Hivyo, tunawataka wabebe mzigo mkubwa zaidi katika kurekebisha hali hiyo kuliko sisi kwa misingi ile ya wajibu wa pamoja lakini ulio tofauti,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa wakati wa uongozi wake,Bara la Afrika limeongeza uhusiano na washirika mbali mbali duniani katika kusimamia umuhimu wa kukabiliana kwa pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi na hasa kati ya Afrika na Bara la Ulaya.
Rais Kikwete alisema mikutano ya maandalizi iliyofanyika Malabo, Equatorial Guinea, Dar Es Salaam na katika Umoja wa Mataifa mjini New York wakati wa Uratibu wake, ilisaidia kuweka msimamo wa pamoja wa Bara la Afrika na kuliwezesha Bara hilo kuzungumza kwa sauti moja wakati wa Mkutano wa Lima.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment