ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 19, 2015

Mbunge aitaka serikali iongeze kasi kuwasaka wauaji wa albino.

Mbunge wa Viti Maalum, Al Shaymaa Kwegyir (pichani), ameapa kufa akipambana kuwatetea watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kuiomba serikali kuongeza kasi ya kuwasaka na kuwafikisha mahakamani watu wanaojihusisha na vitendo vya utekaji na mauaji hayo.

Alitoa ahadi hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kazi za Jamii iliyofanyika katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Profesa Hubert Hairuki (HKMU) jijini Dar es Salaam jana.

Alisema ipo haja ya kuweka sheria kali hata ikibidi wauaji wa albino wanyongwe hadharani ili iwe fundisho kwa wengine ambao wamekuwa wakidhani kuwa kuua watu hao kutawafanya matajiri.

Aidha, alisema mauaji hayo yameitia doa Tanzania na hata viongozi wanapokwenda nchi za nje kwa ziara za kikazi, wamekuwa wakihojiwa kuhusu mauaji hayo na kukosa majibu sahihi.

“Hii inashangaza sana, ni juzi tu Rais amekutana na watu wenye ulemavu wa ngozi na kuweka mikakati ya kutokomeza tatizo hilo, lakini siku hiyo hiyo mtoto mmoja akakatwa mkono mkoani Rukwa, sasa tufanye kila jitihada ikiwamo elimu kwamba mtu hawezi kuwa tajiri kwa kutumia viungo vya albino,” alisema mbunge huyo.

Alisema imefikia wakati kwenye baadhi ya mikoa wenye ulemavu wa ngozi wamekuwa wakifukuzwa kwenye nyumba walizopanga na wengine kunyimwa haki ya kupanga kwenye nyumba kwa maelezo kuwa watasababisha wenye nyumba hao kufungwa na serikali yanapotokea matukio ya kukatwa viungo vyao.

“Sasa tunajiuliza, sisi tukaishi wapi? Kama hata nyumba haturuhusiwi kupanga tukakae nchi gani, ama tutafutiwe kisiwa tukaishi huko baharini kama imeshindikana kutulinda kwenye ardhi yetu…inafikia wakati huko mikoa ya Kanda ya Ziwa watoto hata wachanga wanapelekwa kwenye kituo maalum kwa hofu ya kuuawa inasikitisha sana,” alisema.

Kwa upande wake, Kokushubira Kairuki, alilaani mauaji yanayoendelea nchini na kushauri serikali isisite kutunga sheria kali itakayowafanya wauaji wa albino nchini kuachana na vitendo hivyo vya kikatili.

Alisema serikali na Bunge zima, wanapaswa kushirikiana na jamii kwa ujumla wake kuhakikisha wanaohusika na vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: