Taarifa ambazo zimesambaa bungeni zinaeleza kuwa, jana Zitto alipanga kuwaaga wabunge wenzake kabla ya kikao cha Bunge kuahirishwa mchana, lakini alishindwa kufanya hivyo baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumwita kwa ajili ya mazungumzo.
Zitto ambaye hata hivyo, amekuwa akisisitiza kuwa ataendelea kuwa mbunge licha ya kuvuliwa uanachama wa Chadema, anahusishwa na mipango ya kuhamia katika chama kipya cha ATC-Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jana, Zitto alisema: “Hizo tetesi zipo tu, ukifika muda mtajua kila kitu.”
“Sasa hivi naenda kuongea na Spika, ameniita, nitakuwa na mazungumzo naye.”
Alipoulizwa ikiwa mazungumzo hayo yanahusu kuwaaga wabunge alisema: “Mbona mna haraka, hakuna jambo linaloweza kutokea bila ninyi kujua, vuteni subira.”
Alisema tetesi za kuwaaga wabunge zitathibitika muda utakapofika.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni Zitto hakupatikana kueleza alichozungumza na Spika.
Wakati msimamo wa Zitto ukiwa hivyo, taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa mbunge huyo zinaeleza kuwa, alikusudia kuaga jana na kwamba baada ya Spika Makinda kutaka kuzungumza naye, atatangaza ‘maamuzi magumu’ bungeni leo.
Azma hiyo ya Zitto imekuja wakati Spika Makinda akieleza kuwa bado hajapata barua ya maamuzi ya Chadema kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Spika Makinda aliwaambia waandishi wa habari nje ya Bunge mjini hapa juzi kuwa, ofisi yake haiwezi kufanyakazi taarifa za kwenye vyombo vya habari na badala yake inasubiri taarifa za kiofisi kutoka Nec ndipo watatangaza hatima ya ubunge wa Zitto.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria, chama kikimvua mbunge uanachama anapoteza ubunge wake.
Naye, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alisema chama hicho hakiangaiki tena na suala la Zitto.
Zitto alitimuliwa Chadema hivi karibuni, baada ya Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali kesi yake dhidi ya chama hicho na kuhoji uhalali wa uanachama wake ndani ya chama.
Baada ya hukumu hiyo ya Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alitangaza kuvuliwa rasmi uanachama wa mbunge huyo aliyekuwa analiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Lissu alisema Katiba ya Chadema inaeleza wazi kwamba, endapo mwanachama yeyote atakishtaki chama hicho mahakamani na iwapo atashindwa atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye chama.
Zitto katika mikutano yake aliyoifanya Jumamosi na Jumapili wiki iliyopita pamoja na mambo mengine kuwaaga wapiga kura wake kutokana na kutogombea tena jimbo hilo mwaka huu, alisema bado ni mbunge na ataendelea kutekeleza majukumu yake yakiwamo ya uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
KUHUSISHWA NA ACT
Zitto amekuwa akihusishwa na ACT- Tanzania kutokana na washirika wake wa karibu aliokuwa nao Chadema, Samson Mwigamba na Prof. Kitila Mkumbo kuwa miongoni mwa waasisi wake.
Mwigamba ni Katibu Mkuu wakati Prof. Kitila ni mshauri.
Ingawa Zitto hajathibitisha kuhamia ACT-Tanzania, lakini habari zinasema kuwa huenda akafanya maamuzi hayo kwa sasa zikiwa zimebakia takribani siku nane kuanzia leo kufanyika mkutano mkuu wa chama hicho. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Machi 27-29, mwaka huu na pamoja na mambo mengine, utachagua safu mpya ya uongozi.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, aliridhia kufanyika kwa mkutano huo wa uchaguzi hivi karibuni, baada ya kuutambua upande wa Mwigamba kuwa ndiyo wenye haki ya kukiongoza kufuatia mgogoro kati yake na aliyekuwa mwenyekiti, Kadau Limbu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment